Makonda awapongeza polisi kwa kudumisha amani

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda akizungumza na askari na maafisa wa Jeshi la Polisi alipokuwa akiwapongeza kwa kazi ya kuimarisha hali ya ulinzi na usalama kipindi cha kampeni za uchaguzi Jimbo la Ukonga hadi uchaguzi uliofanyika juzi. Makonda alienda kuwapongeza askari hao jana katika Kituo Kikuu cha Polisi. Kulia ni Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam, Lazaro Mambosasa. Na Mpigapicha Maalum

Muktasari:

Askari hao, walisimamia amani wakati wa kampeni na baada wa uchaguzi wa jimbo la Ukonga uliomfanya Mwita Waitara wa CCM kuibuka mshindi

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewapongeza polisi wa kanda maalum ya Dar es Salaam kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kulinda amani wakati wote wa uchaguzi katika jimbo la Ukonga.

Akizungumza na askari polisi katika kituo kikuu cha polisi cha kanda hiyo leo Septemba 17, 2018, Makonda amesema kwa hali ilivyokuwa wakati wa kampeni, upigaji kura anajivunia kuwa kiongozi wa mkoa huo.

“Ninaona fahari kuitwa mkuu wa mkoa mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama,” amesema Makonda.

Amesema askari hao amewapongeza kwa kuonyesha amani, “Tunakwenda kugonga ‘cheers’ ya kuonyesha ushindi wa kudumisha amani wakati wote wa uchaguzi na wakati wote wa kampeni.”

Amesema amani inapotawala, hata wananchi wanaweza kufanya shughuli zao za kujiletea maendeleo.

Baada ya kugonga cheers, askari hao walimnyanyua juu mithili ya wachezaji wanavyofanya pindi timu zao zinapoibuka washindi katika michuano mbalimbali.