Mambo 10 ya kufanya 2017 iwe ya mafanikio

Muktasari:

Mamilioni ya watu duniani hujiwekea malengo haya kila wanapouanza mwaka. Wapo ambao wanayafanikisha, lakini wengine huishia njiani.

Dar es Salaam. Maneno haya husikika kila mwishoni mwa mwaka; ninataka kununua gari, nitajenga nyumba, nitahakikisha ninapanda cheo au kufunga ndoa.

Mamilioni ya watu duniani hujiwekea malengo haya kila wanapouanza mwaka. Wapo ambao wanayafanikisha, lakini wengine huishia njiani.

Inakadiriwa kuwa katika kila watu milioni moja ambao huweka malengo, nusu yake huwa wanayasahau ifikapo mwezi Machi.

Zipo njia mbalimbali ambazo unaweza kuzitumia kufanikisha malengo uliyojiwekea. Mwandishi wetu amechagua njia 10 ambazo zinaweza kuwa msaada katika malengo ya mwaka 2017

 

Nidhamu ya fedha

Kujifunza kutunza fedha siyo jambo rahisi, lakini huna budi kufanya hivyo kama unataka kupata maendeleo. Wengi hulalamika kuwa hawaingizi fedha nyingi zinazotosha kuhifadhi, yaani kuweka akiba, lakini ukweli ni kwamba unaweza kuwa na kipato cha Sh5 milioni kwa mwezi na kisikutoshe.

Matumizi ya fedha zako lazima yaanzie kwenye maandishi. Jenga tabia ya kuandika mahitaji yako kabla ya kutumia.

Mwandishi wa Marekani aliyebobea katika masuala ya uchumi, Dk Jason Cabler anasema huwezi kutunza fedha kama hutajizoeza kuandika katika daftari matumizi yako.

Hakikisha matumizi yako yanaendana na kipato halisi. Jiulize maswali mawili muhimu kabla ya kununua kitu chochote je, nahitaji kitu hiki na je, ndicho nilichokusudia kukinunua?

 

Matumizi mazuri ya muda

Muda ni bidhaa inayooza haraka na hakuna namna unaweza kuusimamisha. Mafanikio yoyote yanayoonekana leo yalifanyika katika muda sahihi.

Matumizi sahihi ya muda ni ile hali ya kupanga mambo kutokana na umuhimu wake. Ndoto nyingi zimekufa kwa sababu ya tabia ya kuahirisha mambo.

Namna nzuri ya kutunza muda wako ni kuyagawa katika makundi, mambo ambayo unataka kuyafanya. Kwa mfano, unaweza kupanga mambo yako katika makundi ukianza na lile la muhimu kufanyika, lile lisilokuwa na haraka, ambalo ni vizuri kulifanya lakini halina umuhimu na lile ambalo unaweza kumpa mwingine alifanye.

 

Malengo mbadala (Plan B)

Kama huna mpango mbadala ni sawa na kusema huna mipango kabisa. Tabia moja kuhusu maisha ni kwamba yanabadilika kila mara.

Ni rahisi kuiona dunia imefika mwisho pale tumaini lako la pekee linaposhindwa kukupa matunda uliyotarajia.

Kumbuka unachofikiria kukifanya au ujuzi ulionao, huenda yupo anayekuzidi mara 100, kwa hiyo jenga tabia ya kuwa na malengo mbadala, ili moja linaposhindikana uhamie la pili.

Siku zote unapotarajia kufanya jambo weka mpango au ikibidi kuwa na mipango mbadala iwapo ule wa awali hautakwenda kama ulivyotarajia.

 

Kuwa na taarifa sahihi

Unapotaka kujiendeleza kielimu, kufanya kazi au kufungua biashara ni vyema ukafanya utafiti ili kujua kwa undani.

Usikurupuke kufanya biashara ambayo hujui masoko yake, taratibu wala miiko yake. Kazi ambayo huijui misingi yake au kusomea taaluma ambayo hujui utaitumiaje ni sawa na kupoteza muda wako.

Jiridhishe kwa kujisomea mitandaoni, vitabu, majarida na kuuliza kwa wataalamu kuhusu unachotaka kukifanya.

 

Usipoteze mwelekeo

Binadamu sasa anapitia zama ngumu; kutopoteza mwelekeo katika dunia inayoendeshwa na teknolojia, taarifa pomoni, kazi nyingi, majukumu ya familia na mengine mengi.

Lakini kubaki katika mstari ndiyo njia pekee itakayofanikisha safari yako ya mafanikio katika kazi au biashara.

Mwanafalsafa wa China, Conficius aliwahi kusema, “Ukifukuza sungura wawili kwa wakati mmoja utaondoka mikono mitupu.” Vivyo hivyo, katika kutimiza malengo yako, kila jambo inabidi lifanyike kwa wakati wake.

Hapa pia unaweza kukutana na vikwazo vitakavyokutoa njiani, ikiwamo kukatishwa tamaa, fitina na ushindani wa wapinzani wako.

 

Kujali afya

Afya ni mtaji. Afya ni utajiri. Unaweza kutimiza majukumu yako kwa urahisi pale unapofanya kazi zako bila kuhitaji usaidizi kutokana na kuzorota kwa afya.

Mshairi Ralph Waldo Emerson aliwahi kusema utajiri wa kwanza anaoweza kuringia mwanadamu ni afya njema. Bila kuwa na afya njema atashindwa kukamilisha ndoto zake nyingi.

Ni vyema kutunza afya ya mwili na akili kwa kujiweka mbali na vitu vyote vinavyohatarisha usalama wako.

Unywaji wa pombe kupita kiasi, kuendesha gari ukiwa umelewa, kuchelewa kulala na kuuchosha mwili kwa starehe ya aina yoyote ni kuhatarisha afya yako.

Namna nzuri ya kulinda afya ya mwili na akili ni kula mlo kamili, kufanya mazoezi, kupata usingizi wa kutosha kila siku na kupata tiba sahihi na kwa wakati unapougua.

 

Uchaguzi wa marafiki

Mafanikio huja kwa urahisi pale unapokuwa umezungukwa na watu sahihi. Watazame marafiki zako wanaokuzunguka. Je, wanachangia mafanikio au anguko lako?

Jiulize kama watu wote waliokuzunguka wanafikiria kama wewe au uelewa wao ni mdogo kuliko wako? Ni kitu gani unajifunza kwao au wao wanachojifunza kwako.

Marafiki zako lazima wawe watu ambao wanakufanya ukue kila siku, wanakuunga mkono, wanakusukuma kufanikisha jambo na wanakutia moyo.

 

Kujielimisha

Kusoma vitabu, majarida, kutazama filamu, kusikiliza muziki na kusafiri ni namna mojawapo wa kukukuza kimaarifa.

Kuna siri nyingi katika safari, maandishi na filamu ambazo zinaweza kuwa kichocheo cha kukuongezea ujuzi katika kile unachokifanya kila siku.

Mwandishi wa vitabu wa Marekani, Anthony D’Angelo anasema, “Jenga utamaduni wa kujisomea, kamwe hautaacha kuchota maarifa mapya.”

Siyo tu kukuongezea maarifa, kujielimisha ni sehemu ya burudani muhimu katika mwili. Katika maandiko na filamu vipo vitu vinavyofanana na maisha halisi ambavyo husaidia kutoa suluhu ya kuvishughulikia.

 

Kuwa tayari kwa lolote

Binadamu anapanga lakini siyo mwamuzi wa mwisho. Mpangaji mkuu ni Mwenyezi Mungu. Hivyo lolote linaweza kutokea kabla ndoto haijawa halisi kwa maana hiyo ni vizuri kuwa tayari.

Pia, unaweza kupata maradhi, kufiwa na ndugu wa karibu au majanga ya mafuriko au moto yatakayoteketeza kila ulichokiwekeza kwa miaka kadhaa.

Kwa majanga ambayo unaweza kuyawekea kinga kama vile kukatia bima ni vyema ukafanya hivyo ili kupunguza makali pale yatakapotokea.

Kata bima ya nyumba, gari na maisha. Weka vifaa vya kukabiliana na moto nyumbani kwako au ofisini na ujifunze kuvitumia.

 

Kuacha visingizio

Ni kawaida ya wanadamu kutafuta ahueni ya kuutua mzigo kwa namna yoyote pale anapoona mambo hayaendi anavyotaka.

Unapoteleza juu ya ganda la ndizi na kudondoka, akilini mwako kitakachokuja kwa haraka ni kujiuliza nani amekula ndizi na kutupa ganda kiholela. Ukweli ni kwamba kama ungekuwa makini unapotembea kwa kutazama chini, ungeliona na kulikwepa.

Unaposhindwa jambo usitafute sababu ya kujitoa badala yake tafuta njia mbadala ya kuhakikisha kazi hiyo inafanikiwa.