Mambo mazito ya wastaafu kwa Magufuli

Rais John Magufuli akisalimiana na Jaji Mkuu Mstaafu, Barnabas Samatta kabla ya kuanza kikaona viongozi wa juu wastaafu kilichofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, Julai 3, mwaka huu. Kushoto ni Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhani. Picha na Ikulu

Muktasari:

Video mpya zilizotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu kuanzia juzi usiku zinaonyesha jinsi viongozi hao wastaafu walivyotoa maoni yao zaidi, ambayo Rais Magufuli aliahidi kuyafanyia kazi.

Dar es Salaam. Ikiwa ni siku tatu tangu Rais John Magufuli akutane na viongozi wastaafu, mambo mengine yaliyozungumzwa katika kikao hicho yameibuka.

Video mpya zilizotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu kuanzia juzi usiku zinaonyesha jinsi viongozi hao wastaafu walivyotoa maoni yao zaidi, ambayo Rais Magufuli aliahidi kuyafanyia kazi.

Rais Magufuli alikutana na wastaafu hao Jumanne wiki hii Ikulu jijini Dar es Salaam, lakini siku hiyo kurugenzi hiyo ya mawasiliano ilisambaza video fupi na chache jambo ambalo lilifanya baadhi ya maoni ya wastaafu hao kutoonekana.

Lakini, kipindi maalumu cha Rais akizungumza na viongozi hao wastaafu kilichorushwa na Televisheni ya Taifa (TBC1) juzi usiku kilionyesha mazungumzo hayo kwa urefu tofauti na video za awali.

Katika mkutano huo, viongozi hao wanaonekana kuwa huru kutoa maoni yao huku wengi wao wakigusia zaidi suala la utawala bora.

Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, ambaye alimteua Dk Magufuli kwa mara ya kwanza kuwa naibu waziri, alitaka CCM ipewe kipaumbele kuliko watu binafsi.

Ujumbe wa Mkapa

Mkapa alisema amefurahishwa na mkutano huo kwani utaondoa dhana iliyojengeka kwamba, “mtu anayeweza kusikilizwa na Rais Magufuli ni mzee wake Benjamin Mkapa,” lakini leo vyombo (vya habari) vipo hapa vitaeleza waliotoa ushauri.

Mzee Mkapa ambaye ni waziri wa zamani wa Mambo ya Nje alisema, “Ningelipenda kusikia zaidi Serikali yetu inajitambulisha kama ni Serikali ya CCM, hasa kwa mawaziri, ni Serikali ya CCM inayoongozwa na Rais wetu, Rais Magufuli, lakini naye ni Rais wa CCM na CCM ndiyo ilimpa urais.”

Kiongozi huyo mkuu wa nchi wa Awamu ya Tatu aliongeza, “Kwa hiyo hii ya kusema mimi, mimi, aaah ni Serikali ya CCM, itajenga hamasa ya kuchaguliwa tena na kuendelea kutawala.”

Barnabas Samatta

Akizungumza katika kikao hicho, Jaji Mkuu wa zamani, Barnabas alipongeza uamuzi huo wa Rais Magufuli kuwakutanisha kwani kitendo hicho hakijawahi kutokea huko nyuma.

Mwanasheria huyo alisema atazungumzia mambo mawili ikiwamo kuunga mkono alichokuwa amekisema awali mrithi wake wa ujaji mkuu, Augustino Ramadhani kuhusu utawala sheria. “Juhudi zote zinazofanyika kwenye uchumi na kwenye sehemu zingine zote ni lazima ziwe ndani ya utawala wa sheria na nafikiri tukubaliane kabisa katika hilo,” alisema Samatta ambaye alikuwa jaji mkuu kati ya mwaka 2000-2006 kabla ya kumuachia Ramadhani.

“Na utawala wa sheria lazima uambatane na haki. Haiwezekani, unaweza kuwa na sheria lakini ni sheria mbovu, kwa hiyo (miswada) bills tunazozipeleka bungeni lazima tutazame sana je, bill hii ikiwa sheria je, utekelezaji wake unaweza kunyang’anya haki ya mtu.” alihoji.

Jaji mkuu huyo mstaafu alihoji, “Mimi wakati mwingine ninapoangalia TV, ninaposikiliza baadhi ya viongozi amri wanazotoa hasa (wakuu wa wilaya) Ma-DC najiuliza wakati mwingine sheria iko wapi,” alisema Samatta aliyezaliwa Julai 20, mwaka 1940.

Augustino Ramadhan

Awali, Jaji Ramadhan alisema, “Amani ni tunda la haki, kama utakuwa na haki hakuna matatizo, amani itakuwepo lakini kama haki itatetereka kidogo hapo tutakuwa na wasiwasi wa amani. Tukiangalia haki, amani yenyewe itajiangalia, sasa hivi nazungumza hii habari ya haki, Mheshimiwa Rais katika ngazi zote, kuanzia kwako Mheshimiwa Rais tutekeleze haki, uje kwa mawaziri, uje kwa (wakuu wa mikoa) Regional Commissioners uje kwa (wakuu wa wilaya) DC na kila ngazi zote tutekeleze haki,” alisema mwanajeshi huyo wa zamani aliyefikia cheo cha Brigedia Jenerali.

Cleopa Msuya

Waziri mkuu mstaafu Cleopa Msuya alisema, “Nimekaa katika awamu zote na hii ya tano na kabla ya kwanza, nilifanya kazi na wakoloni labda aliyenitangulia ni Mzee (Ali Hassan) Mwinyi.

“Uongozi si kitu rahisi, si kitu ambacho unaweza kutolea (suluhisho) solution iliyoandikwa na kwenda kufanya kazi. Itabidi hao waliokuchagua wanakupa hizo nyadhifa, watumie muda wao mwingi kutathimini matatizo yanayojitokeza na kubuni mbinu za kutuvusha (na) hayo matatizo yanayotokea,” alisema.

Msuya ambaye alikuwa waziri mkuu wakati wa Serikali ya Awamu ya Kwanza na ya Pili alisema, “Kwa kweli tunachotazamia kwa viongozi wetu mliopo madarakani sasa hivi ni hilo, kuwa (na majibu) responsive kwa matatizo yanayojitokezana (kuwa na suluhisho) ku ‘design solution’ ambazo zinaridhisha wananchi.”

Jaji Warioba

Jaji Joseph Warioba, ambaye pia alikuwa waziri mkuu wa kwanza wa Awamu ya Pili, alipongeza jitihada zilizofanywa na Serikali kama utoaji wa elimu bila malipo, upatikanaji wa madawati shuleni, suala la rushwa, mishahara hewa na mapambano dhidi ya dawa za kulevya.

“Haya ni matatizo makubwa na mengine ni ya kihistoria, ukitazama rushwa ni historia lakini lazima tuyawekee utaratibu kwa kujenga taasisi, lazima taasisi zitazamwe mfumo wake, kanuni zake, taratibu zake ili kuwa na uhakika kwamba ukifanya kitu kiwe ni (muendelezo) sustainable,” alisema mwanasheria mkuu huyo wa zamani.

Warioba, ambaye alikuwa mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba alisema, “Unaweza kukuta hili la mishahara hewa, dawa za kulevya yakaja kujirudia huko mbele kwa hiyo lazima kujenga taasisi kwa kuzitazama upya kwani unaweza kukuta miaka mitano sita huko mbele yakajitokeza tena.”

Bilal na Sayansi

Makamu wa rais mstaafu, Dk Mohamed Ghalib Bilal alisema, “Nakupongeza sana kwa juhudi zako kubwa unazozifanya za kuongoza nchi hii. Nakushukuru kwa kuanzisha utaratibu huu wa kukaa na wastaafu na kuwasikiliza walichonacho.”

Bilal aliyekuwa Makamu wa Rais katika Awamu ya Nne, alisema miongoni mwa jitihada zilizofanywa ni kuanzisha vyuo vikuu na kuimarisha mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu. Alisema Tanzania kama nchi nyingine zote zinazoendelea, kazi ya kupambana na kasi ya mabadiliko Sayansi na teknolojia ni muhimu.

John Malecela

Waziri mkuu mwingine wa Awamu ya Pili, John Malecela alisema, “Viwanda vikubwa vilivyojengwa na Serikali za nyuma, vifufuliwe kwanza, kwani vilijengwa kwa madhumini kama uzalishaji mkubwa duniani wa kusokota kamba za mkonge iko Tanzania.”

Malecela, ambaye amewahi kuwa balozi wa Tanzania nchini Uingereza, alisema “Tulivijenga makusudi ili kutokusafirisha mkonge, (ili) tusafirishe kamba na tulinunua kwa bei kubwa na si ajabu hayo yanayosemwa kwamba madeni makubwa yalitokana na viwanda hivyo.”

Malecela alisema Tanzania ilikuwa ndiyo mzalishaji mkubwa wa nguo kwani awali ilikuwa Uganda. “Viwanda vya nguo sisi tulikuwa tunaleta vipya, Mbeya kilikuwepo, Mwanza, kilichopo Musoma na hapa Dar es Salaam. Sasa mimi ningeshukuru sana kama tungejitahidi sana kuvifufua hivi vya zamani na hivi vipya vije visaidie kuongeza mazao.”

Amani Abeid Karume

Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume alisema, “Wewe (Rais Magufuli) ni kiongozi wetu, tumekuchagua sote na tuna mategemeo makubwa kutoka kwako.

“Nakupongeza sana kwa kazi nzuri ambayo umeanza kuifanya tangu umechaguliwa kuwa Rais, wenzangu waliotangulia wamesema umejitahidi sana katika kupambana na rushwa, wizi wa mali za Serikali ambao kwa kiasi fulani ulishamiri,” alisema.

Alisema Rais Magufuli amejitahidi kurejesha nidhamu katika Serikali na kwamba sasa kuna nidhamu ya kazi, barua zinajibiwa na viongozi wa Serikali wanafika mikutanoni kwa muda.

“Zile lugha za zamani za kujiona ni mtawala zimepungua sana, wanajua kuzungumza na watu na Serikali inapaswa kuwa hivyo,” alisema Karume, ambaye ni mtoto wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume.

Magufuli atoa ahadi

Kauli hizo za wastaafu hazikuwa bure, kwani Rais Magufuli alitoa ahadi ya kuzitekeleza.

“Nawashukuru sana wazee wangu, kwa kukubali kwenu kuja. Mimi naamini haya mliyozungumza, mliotoa ushauri nimeyapokea na ndiyo maana siwezi kuyajibu hapa,” alisema Rais Magufuli na kuongeza:

“Ni mawazo mazuri mmeyatoa katika Serikali yetu. Ndiyo maana Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) na katibu mkuu kiongozi (Balozi John Kijazi) walikuwa wanachukua note.

“Nimeyapokea kwa asilimia 100, ushauri tumeupokea na utatusaidia kusonga mbele na niwahakikishie wastaafu kwamba nitaendelea kuwapa heshima zote zinazostahili kwa heshima na upendo mkubwa,” alisema Dk Magufuli.

Rais Magufuli aliwaambia wastaafu hao kuwa wanapaswa kutambua kuwa Serikali anayoiongoza itawalinda na kuwatunza.

“Niwahakikishie wastaafu, mimi sina kinyongo chochote na ninaamini tukienda pamoja na kufanya kazi pamoja tutaijenga nchi,” alisema.

Aliongeza, “Mmesema amani lazima iheshimiwe na itunzwe. Mmekuwa walezi wazuri wa amani, endeleeni kuitunza na kutushauri na kuwashuari wote.”

Pia, Rais Magufuli alitoa sababu ya kutokuwapo kwa mtangulizi wake, Jakaya Kikwete akisema, “Leo wastaafu ambao hawapo ni Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete yuko Marekani.

“Tulikuwa tumemwalika na Mama (Getrude) Mongela ambaye ni spika mstaafu wa Bunge la Afrika naye yuko nje.

Wengine waliohudhuria

Ukiondoa viongozi hao, wengine waliohudhuria ni mawaziri wakuu wastaafu; Dk Salim Ahmed Salim, John Malecela, Edward Lowassa, Frederick, Sumaye na Mizengo Pinda.

Pia walikuwapo maspika wastaafu; Pius Msekwa, Anne Makinda na wa sasa Job Ndugai na jaji mkuu mstaafu, Othman Chande.

Video zilizotolewa baada ya mkutano na kurugenzi ya mawasiliano Ikulu mara baada ya mkutano huo Jumanne iliwaonyesha baadhi ya wastaafu wakizungumza kwa kifupi.

Rais Mwinyi alisema anachokiona ni kuwa kwa sasa kuna nidhamu na wafanyakazi wa Serikali wanafika kazini kwa wakati. “Wakifika wanafanya kazi, hawalipwi kwa sababu wamekwenda kazini, bali kwa sababu wanafanya kazi,” alisema.

Lowassa ambaye ni Waziri Mkuu wa kwanza wa Awamu ya Nne, alizungumzia kuhusu amani na kusisitiza kuwa maneno yasiyopimwa yanaweza kuondoa amani ya nchi.

Sumaye ambaye ni Waziri Mkuu pekee aliyedumu kwa miaka 10, alisema: “Kama mtakumbuka nilichosema wakati nahamia upinzani, nilisema sina chuki na CCM na Rais Magufuli au na Rais Kikwete, lakini nilisema kuwa ninakwenda huko kwa masilahi ya CCM.”

Alisema hata hivyo wapo wanaopotosha ukweli wa hilo, lakini yeye anajua anachofanya. “Ninajua ninachokifanya na nina hakika mngekuwa mnajua juhudi tunazoweka upande wa pili, mngesema tunafanya kazi nzuri kwa ajili ya nchi hii. Kwa hiyo nataka tu niseme hakuna uadui wowote,” alisema.