Mashahidi 10 kuitwa kesi ya Manji

Dar es Salaam. Mashahidi wasiozidi 10 wa upande wa mashtaka wanatarajiwa kutoa ushahidi katika kesi ya kutumia dawa za kulevya aina ya Heroin inayomkabili  mfanyabiashara maarufu nchini, Yusufu Manji.

Hayo yameelezwa leo Alhamisi na Wakili wa Serikali Mkuu, Timon Vitalis mbele ya Hakimu Mfawidhi, Cyprian Mkeha wakati akimsomea maelezo ya awali (PH).

Akisomewa maelezo hayo ya awali, Manji alikubali maelezo yake binafsi na kukana shtaka linalomkabili.

Kwa kujibu wa maelezo hayo ya awali, Vitalis alidai Manji ni mfanyabiashara  na Februari, 2017 alijihusisha na dawa za kulevya na kutumia.

Alidai kuwa siku hivyo aliripoti polisi na kwamba baada ya kuripoti alipelekwa nyumbani kwake Sea View Kivukoni kupekuliwa.

Aliendelea kudai, pia alipelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ambapo alipimwa haja ndogo  'mkojo' na kugundulika una chembechembe za sawa za kulevya aina ya Benzodiazepine  na alifunguliwa kesi ya kutumia dawa za kulevya.

Baada ya kusomewa maelezo hayo, Manji alikubali maelezo yake binafsi ikiwamo majina yake na kuwa yeye ni mfanyabiashara na kukana shtaka.

Wakili Vitalis alidai wanatarajia  kuwaita mashahidi wasiozidi 10 kutuoa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka. Kesi itaanza kuunguruma Agosti 22, 23 na 25, 2017.