Mashtaka ya Hans Poppe yazua mvutano mahakamani

Muktasari:

Dakika chache kabla ya mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Klabu ya Simba Zacharia Hans Poppe kupandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kusomewa mashtaka yanayomkabili, umeibuka mvutano kati ya upande wa mashtaka na upande wa utetezi


Dar es Salaam. Dakika chache kabla ya mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Klabu ya Simba Zacharia Hans Poppe kupandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kusomewa mashtaka yanayomkabili, umeibuka mvutano kati ya upande wa mashtaka na upande wa utetezi.

Upande wa Mashtaka kupitia kwa wakili wa  Serikali Mwandamizi,  Shedrack Kimaro aliomba Hans Poppe kuunganishwa katika kesi inayowakabili rais wa Simba, Evans Aveva  na makamu wake, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ ya madai ya kughushi na utakatishaji fedha.

Hata hivyo,  upande wa utetezi ukiongozwa na wakili Nestory Wandiba alipinga akidai kuwa mahakama ilishatoa uamuzi kuwa kesi iendelee kwa washtakiwa waliopo mahakamani na kwamba kwa maombi hayo,  mahakama ina lengo la kurudisha nyuma kesi hiyo.

Wandiba ameomba mahakama hiyo iendelee na kesi dhidi ya washtakiwa waliopo mahakamani na Hans Poppe afunguliwe mashtaka yake.

Hakimu Mkazi Mkuu anayeshikiliza shauri hilo,  Thomas Simba,  baada ya kusikiliza hoja za pande zote,  anaandika uamuzi ama kukabiliana na upande wa mashtaka wa kumuunganisha Hans Poppe katika kesi ya akina Aveva au kutupilia  mbali maombi hayo ya upande wa mashtaka.

April 30, 2018, mahakama hiyo iliamuru washtakiwa Hans Poppe na mfanyabiashara Franklin Lauwo wakamatwe popote walipo.

Mahakama hiyo ilitoa amri hiyo baada ya upande wa mashtaka kupitia kwa wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru),  Leonard Swai kuieleza kuwa wamewatafuta washtakiwa hao tangu Machi 16, 2018 bila mafanikio.

Hata hivyo, Hans Poppe amepandishwa kizimbani kujibu mashtaka 10 yanayomkabili likiwemo la matumizi mabaya ya ofisi.

Mbali na Hans Poppe, mwingine aliyefikishwa mahakamani hapo ni mfanyabiashara Lauwo.

Soma Zaidi: