Sethi ataka kutibiwa na daktari wa Afrika Kusini

Muktasari:

Korti yaelezwa Hospitali ya Taifa Muhimbili ipo tayari na ina uwezo wa kumfanyia upasuaji huo.

Dar es Salaam. Mawakili wa Harbinder Sethi wameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mteja wao atibiwe na daktari maalumu kutoka Afrika Kusini.

Wamesema baada ya mteja wao kufanyiwa vipimo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alielezwa hawawezi kufanya upasuaji wa puto alilonalo tumboni. 

Kutokana na hilo, wameomba daktari huyo wa Afrika Kusini afike nchini kwa ajili ya kumtibu Sethi au mteja wao asafirishwe kwenda Afrika Kusini kwa matibabu.

Wakili Joseph Sungwa amewasilisha ombi hilo leo Ijumaa Novemba 10,2017 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi baada ya mwendesha mashtaka wa Takukuru, Leonard Swai kueleza kesi ilipangwa kutajwa na upelelezi haujakamilika.

Baada ya maelezo hayo kutolewa, wakili Sungwa aliwasilisha ombi hilo akisema Sethi anahitaji kutibiwa na daktari maalumu kwa kuwa puto hilo muda wake unaisha.

Wakili Swai alipinga ombi hilo akisema Hospitali ya Muhimbili haijashindwa kumfanyia upasuaji wa puto Sethi bali yeye ndiye anajichelewesha kutokana na kutaka uwepo wa daktari wake wa Afrika Kusini.

Alisema Mahakama ilishatoa amri Sethi apelekwe Muhimbili kwa matibabu, amri ambayo ilitekelezwa na hoja kwamba puto lililoko tumboni mwake limeisha muda haijathibitishwa.

Swai alisema ripoti ya daktari ni siri kati yake na mgonjwa, hivyo hawezi kuisemea kwa kuwa hawajaisoma lakini wanapata shaka na maelezo ya wakili wa Sethi kuwa Muhimbili imeeleza kuwa haina utaalamu wa kumfanyia upasuaji wa puto.

Wakili Swai amesema taarifa za Jeshi la Magereza ambako Sethi yupo na ripoti ya Hospitali ya Muhimbili imepitia gereza alilopo.

Alisema Hospitali ya Muhimbili ipo tayari na ina uwezo wa kumfanyia upasuaji huo.

“Mshtakiwa aliieleza Magereza anahitaji daktari wake wa Afrika Kusini aje kumtibu, lakini si kweli kwamba Tanzania hatuna uwezo wa kumtibu,” amesema.

Alisema suala hilo  linahitaji utaratibu kwa sababu linahusisha taasisi tofauti ambazo ni Magereza, Muhimbili na Serikali.

Kuhusu hoja ya Sethi kupelekwa Afrika Kusini, wakili Swai alisema ni ngumu na haiwezekani. Amesema hawaoni sababu ya kupelekwa huko wakati Muhimbili wamethibitisha wana uwezo wa kumfanyia upasuaji wa puto.

 

Akizungumzia upelelezi wa kesi hiyo, wakili Swai amesema wapo katika hatua nzuri na kwamba wanataka kwenda mahabusu kuchukua maelezo ya onyo ya washtakiwa hao.

Swai alidai amri ikitoka wachunguzi wataenda kuchukua maelezo yao.

Akizungumzia hatua ya upelelezi ulipofikia, wakili Michael Ngalo amesema upelelezi umechukua muda mrefu ni takriban miezi mitano sasa haujakamilika na washitakiwa wapo mahabusu.

Baada ya kusikiliza hoja za mawakili wa pande zote husika, hakimu Shaidi amesema Mahakama haina mamlaka ya kutoa amri yoyote kuhusu iwapo Muhimbili wana uwezo wa kumtibu mshtakiwa au la, hivyo amewataka wawasilishe maombi Mahakama Kuu.

Pia, hakimu Shaidi amekubali ombi la wachunguzi kwenda kuchukua maelezo ya onyo ya washitakiwa mahabusu.

Ameagiza Jumatatu ijayo maelezo hayo yakachukuliwe saa nne asubuhi. Kesi imeahirishwa hadi Novemba 24,2017.

Katika kesi hiyo, Sethi na James Rugemarila wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi kwa kula njama, kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kughushi, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kutakatisha fedha na kusababisha hasara ya Dola 22.198 milioni za Marekani na Sh309.461 bilioni.