Mbowe, wenzake waomba kuhamia Mahakama Kuu

Muktasari:

Baada ya kukamilisha hilo wakili huyo aliomba kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali, lakini wakili wa utetezi, Peter Kibatala aliomba shauri hilo kuhamishiwa Mahakama Kuu.

Dar es Salaam. Mbunge wa Bunda Mjini (Chadema), Ester Bulaya ameunganishwa katika kesi inayowakabili viongozi wengine wanane wa chama hicho, huku mawakili wa utetezi wakiomba kuhamishia shauri hilo Mahakama Kuu.

Baada ya kufanya mabadiliko ya hati ya mashtaka kwa kumuongeza Bulaya ambaye ni mshtakiwa wa tisa na kuongezwa mashtaka kutoka 10 hadi 12, Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi aliwasomea upya mashtaka washtakiwa.

Baada ya kukamilisha hilo wakili huyo aliomba kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali, lakini wakili wa utetezi, Peter Kibatala aliomba shauri hilo kuhamishiwa Mahakama Kuu.

Kibatala alisema washtakiwa takriban wote ni wabunge na kwamba, shtaka la pili linakiuka haki yao ya msingi ya kufanya shughuli za kisiasa za chama wanachotoka cha Chadema.

Kutokana na hilo, aliomba kulipeleka shauri hilo Mahakama Kuu ili itoe tafsiri iwapo ni halali kwa washtakiwa kushtakiwa kijinai.

Kwa shtaka la nne hadi la tisa, Kibatala anaomba mahakama iridhie wapeleke shauri Mahakama Kuu kwa sababu yanahusu masuala ya kikatiba juu ya uhuru wa kutoa maoni na hakuna mahali katika hati ya mashtaka inapoelezwa kwamba yaliyotamkwa na washtakiwa ni uongo au ni ya kutungwa.

Wakili wa Serikali Mkuu, Nchimbi alidai kilichowasilishwa na upande wa utetezi kisheria hakina mashiko, hivyo kuomba kujibu hoja hizo leo.

Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu anayesikiliza shauri hilo namba 112 la mwaka 2018 aliliahirisha hadi leo.

Bulaya na wenzake wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama wakidaiwa kati ya Februari Mosi 2018 na Februari 16, 2018 wakiwa Kinondoni, Dar es Salaam walikula njama na kutenda kosa la jinai na kuendelea na mkusanyiko isivyo halali na kusababisha chuki na uchochezi.

Pia, wanakabiliwa na shtaka la kufanya mkusanyiko usio halali kinyume na sheria Februari 16, katika barabara ya Kawawa eneo la Mkwajuni wilayani Kinondoni, Dar es Salaam; kutotekeleza agizo la polisi lililowataka kutawanyika na kusababisha kifo cha Akwilina Akwilini, aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) na kujeruhiwa askari wawili. Bulaya ambaye yupo nje kwa dhamana anakabiliwa na shtaka la peke yake akidaiwa kushawishi kutendeka kosa la jinai.

Washtakiwa wengine ni mwenyekiti wa Chadema na mbunge wa Hai, Freeman Mbowe; Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa; naibu katibu mkuu (Zanzibar), Salum Mwalimu; naibu katibu mkuu (Bara) na mbunge wa Kibamba, John Mnyika; mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko; katibu mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji; mbunge wa Kawe, Halima Mdee; na mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche.