Mbowe, wenzake wasomewa mashtaka 13 mahakamani

Viongozi wa Chadema  wakiongozwa na Mwenyekiti, Freeman Mbowe wakimsikiliza mwanasheria wao, Peter Kibatala (kulia) wakati wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam jana. Picha na Omar Fungo

Muktasari:

  • Mbowe na wenzake walisomewa mashtaka hayo jana na Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake saba wamesomewa mashtaka mapya 13 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Mbowe na wenzake walisomewa mashtaka hayo jana na Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri.

Hatua hiyo imekuja baada ya upande wa mashtaka, Juni 11, 2018 kuamriwa na Mahakama hiyo wafanye marekebisho katika hati ya mashtaka baada ya kuonekana kuna mapungufu ya kisheria.

Akisoma hati hiyo mpya iliyofanyiwa marekebisho katika kesi hiyo namba 112 ya 2018, Nchimbi aliwasomea mashtaka washtakiwa wanane kwa kuwa mwenzao Esther Matiko mbunge wa Tarime Mjini hakuwapo mahakamani kwa kuwa ni mgonjwa.

Waliosomewa mashtaka ni Mbowe, mbunge wa Iringa Mjini Peter Msigwa, naibu katibu mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu na naibu katibu mkuu Bara na mbunge wa Kibamba, John Mnyika.

Wengine ni katibu mkuu wa chama hicho, Dk Vincent Mashinji, mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na mbunge wa Bunda, Esther Bulaya.