Mgombea ubunge Serengeti, madiwani watano wapita bila kupigwa

Muktasari:

  • Wagombea udiwani kwenye kata tano na ubunge wa Serengeti wamepita bila kupingwa baada ya vyama vya upinzani vilivyochukua fomu kutozirudisha

Serengeti. Msimamizi wa uchaguzi jimbo la Serengeti, Juma Hamsini amesema wagombea wa CCM kwa nafasi za ubunge na udiwani wamepita bila kupingwa baada ya wagombea wa vyama vya upinzani kutorudisha fomu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Novemba 5, 2018, Hamsini amesema madiwani watano wamepita bila kupingwa akiwamo Marwa Chacha aliyekuwa mbunge kupitia Chadema ametetea nafasi yake akiwa CCM.

“Marwa Chacha (CCM) amekidhi hitaji la sheria ya uchaguzi ndiyo maana nimemtangaza kupita bila kupingwa, Joseph Magoiga (CUF) mhuri, nembo na barua ya kumtambulisha ni nakala (copy) inakuwa vigumu kuthibitisha uhalali wake,” amesema

Hamsini amesema wagombea wengine Mgaya Bwire (NRA) hakujaza fomu ya maadili na wadhamini aliwapata wanne badala ya 25, mgombea Christina Nyamherya (UDP) hakupata wadhamini wala risiti ya mahakamani hakuwasilisha na kupoteza sifa ya kugombea.

Kwa upande wa madiwani amesema wagombea wote wa upinzani hawakurudisha fomu kwa kata zote tano.

Hata hivyo, Rhobi Magoiga wa CUF amesema licha ya kuwasilisha fomu zote hajapewa sababu za kuenguliwa huku akidai tume ikiendelea kubaki ilivyo ni bora vyama vya upinzani visigombee.