Mgombea udiwani Chadema apatikana akiwa hajitambui

Muktasari:

Vyombo vya dola vinamhoji ili kuendelea na uchunguzi.

Muleba. Mgombea udiwani (Chadema) Kata ya Buhangaza, Mchungaji Athanasio Makoti (28) aliyepotea Februari 2,2018 katika mazingira ya kutatanisha amepatikana akiwa hajitambui.

Makoti amepatikana leo Februari 5,2018 saa moja asubuhi, Katibu wa Chadema wilayani Muleba, Elisha Kabombo akisema alitelekezwa na watu wasiojulikana jirani na Hospitali ya Kagondo.

Amesema wananchi waliokuwa wakipita eneo hilo usiku wa kuamkia leo walimuona akiwa kando mwa  barabara ya kuelekea Bukoba, hivyo kumpeleka hospitali.

“Hali yake si nzuri kwa sababu hawezi kuzungumza vyema wala kuketi. Kawekewa dripu za maji. Tuzidi kumuombea,” amesema.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Isack Msangi amethibitisha kupokea taarifa za kupatikana mgombea huyo. Amesema vyombo vya dola vinamhoji ili kuendelea na uchunguzi.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Kagondo, Dk Humphrey Batungi alipoulizwa afya ya mgombea huyo amesema ni mapema kuzungumza.

“Ninaelekea kwenye kikao nitafute mchana baada ya dawa anazotumia mgonjwa kufanya kazi na huenda akawa na mabadiliko,” amesema Dk Batungi.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Isack Msangi amethibitisha kupokea taarifa za kupatikana kwa mgombea huyo. Amesema vyombo vya dola vitafanya mahojiano naye ili kuendelea na uchunguzi.

Katibu wa uenezi wa Chadema jimbo la Muleba Kusini na mratibu wa chama hicho jimbo la Muleba Kaskazini, Hamisi Yusufu amesema baada ya kufikishwa hospitali alikutwa na majeraha, huku akizungumza kwa shida.

Amesema mgombea huyo wa udiwani aliwaeleza amenyang’anywa fedha, waliomteka walimfunga kitambaa cheusi usoni na kumtaka asigombee uchaguzi utakaofanyika Februari 17,2018 na amekiri  kuwafahamu baadhi ya waliomteka.

Katika uchaguzi huo anachuana na mgombea wa CCM, Jenitha Tibeyenda na wa NCCR-Mageuzi, Grason Anaseti.