Mgomo wa Daladala Tanga washika kasi

Muktasari:

Wamewarushia lawama askari wa usalama barabarani kwamba wanawanyanyasa kwa kuwatoza faini bila kuwa na makosa

Tanga. Wananchi wa Tanga  leo kuanzia asubuhi wamejikuta wakihaha kwa kukosa Huduma ya usafiri baada ya madereva wa mabasi ya daladala kufanya mgomo.

Mwananchi imeshuhudia wananchi wakiwamo wanafunzi wakiwa kwenye vituo vya daladala huku wakishindwa cha kufanya baada ya kukaa vituoni bila kupita daladala.

Wakizungumza na Mwananchi wasafiri hao wamelalamika kuwa mgomo huo umefanyika siku ambayo kwao imesababisha usumbufu wa kuwahi kwenye shughuli zao.

Omari Ayub ambaye amejitambulisha kuwa ni dereva wa daladala inayofanya safari kati ya Magomeni na Raskazone amesema wameamua kugoma wakipinga vitendo vya jeshi la polisi kikosi cha usalama barabarani kuwanyanyasa kwa kuwatoza faini bila kuwa na makosa.

Amesema licha ya kufuata taratibu za usalama barabarani lakini wamekiwa wakinyanyaswa.

Ofisa wa Sumatra Mkoa wa Tanga, Dk Walukani Luhamba amesema mgomo huo uko kinyume na taratibu kwa sababu  madereva hao wa  daladala wamekuwa wakivunja sheria ikiwamo kupandisha na kuwashusha abiria kwenye vituo visivyo rasmi.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba amesema jeshi hilo haliko tayari kuona sheria inavunjwa  hivyo amewasihi kwenda kutoa Huduma haraka ili wananchi wasihangaike.

Nipo njiani naenda kuzungumza nao ili warejeshe Huduma kwa wananchi "amesema Kamanda Wakulyamba.