Mhakiki hewa wa watumishi hewa akamatwa Shinyanga

Muktasari:

  • Nyamhanga Malegesi  aliyekamatwa na taasisi hiyo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama.
  • mtuhumiwa huyo ambaye pia anafahamika kama Ezius Malegesi alijifanya mjumbe wa tume iliyoundwa na rais John Magufuli kufanya uhakiki wa watumishi hewa mkoani Shinyanga.


Shinyanga. Mjumbe feki wa timu ya Rais ya kuhakiki watumishi hewa amekamatwa na  Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Shinyanga akidaiwa kuomba rushwa ya Sh150,000 kutoka kwa mwalimu ili amsaidie kuweka nyaraka  zilizokosekana kwenye jalada lake la utumishi.
Mkuu wa Takukuru mkoa wa Shinyanga, Gasto Mkono alimtaja mtuhumiwa huyo aliyekamatwa jana kuwa ni Dk Nyamhanga Malegesi  aliyekamatwa na taasisi hiyo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama.
Alisema mtuhumiwa huyo ambaye pia anafahamika kama Ezius Malegesi alijifanya mjumbe wa tume iliyoundwa na rais John Magufuli kufanya uhakiki wa watumishi hewa mkoani Shinyanga.
“Kutokana na kitendo hicho, mtuhumiwa huyo ametenda kosa jingine la kujifanya mtumishi wa umma chini ya kifungu cha 100(b) cha sheria ya kanuni za adhabu sura 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 na kuomba rushwa ya Sh150,000,”alifafanua Mkono.
Mkono aliongeza kuwa baada ya mtu huyo kukamatwa na kufanyiwa upekuzi alikutwa na nyaraka mbalimbali zikiwamo CV zilizoambatana na vyeti vya elimu vya watu mbalimbali, CD za hotuba za viongozi wa nchi na vitambulisho mbalimbali.
Alisema uchunguzi unaendelea kutokana na kuonekana kuwa mtu huyo ni mhalifu mzoefu.
Mkono aliwataka watumishi wa umma, wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kuwa makini ili wasirubuniwe na wahalifu hasa katika kipindi hiki ambacho kuna operesheni ya sukari na watumishi hewa.
Alisema hakuna ofisa yeyote wa Takukuru au mjumbe au wa kikosi kazi maalum atakayefanya kazi kwa kificho bila kitambulisho, hivyo atakayetilia shaka watendaji hao atoe taarifa kwa mkuu wa taasisi hiyo, Jeshi la Polisi au kwa kiongozi yeyote wa Serikali mapema iwezekanavyo.