Azam yamtupia virago Omog

Tuesday March 3 2015Kocha wa Azam Mcameroon Joseph Omog 

Kocha wa Azam Mcameroon Joseph Omog  

By Vicky Kimaro, Mwananchi

Dar es Salaam. Hatimaye Azam imemtimua kocha wake Mcameroon Joseph Omog ikiwa ni siku mbili baada ya kutolewa na El Merreikh ya Sudan kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika

Katika taarifa iliyotolewa jana na uongozi wa Azam haikusema sababu za klabu hiyo kumfungashia virago Omog ambaye katika miezi14 aliyokuwa Chamazi aliwasaidia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya kwanza.

Tetesi za kutaka kutimuliwa Omog zilianza baada ya timu hiyo kutolewa katika robo fainali ya Kombe la Mapinduzi na Mtibwa Sugar kwa penalti, lakini uongozi wa Azam ulikanusha taarifa hizo.

Tangu wakati huo Azam imekuwa haina matokeo mazuri katika Ligi Kuu ikiwemo kufungwa na Ndanda 1-0, JKT Ruvu (1-0) pamoja na kutoka suruhu na Ruvu Shooting na Prisons na sasa ipo nafasi ya pili ikiwa kwa pointi 27, wakati Yanga ikiongoza kwa pointi 31.

Hata hivyo, ndoto ya Azam kutaka kufanya vizuri katika mashindano ya Afrika ilivunjika Jumamosi iliyopita baada ya kukubali kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa El Merreikh hivyo kutolewa kwa jumla ya mabao 3-2.

Mbali ya Omog, Azam pia imevunja mkataba na kocha wake msaidizi Ibrahim Shikanda aliyewahi kuwa mchezaji wa kikosi hicho.

Mabingwa hao sasa watakuwa chini ya kocha msaidizi George Best Nsimbe wakati watakapoikabili JKT Ruvu Jumamosi ijayo katika mechi ya ligi itakayochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Kutimuliwa kwa makocha hao ni mwendelezo wa timua timua ndani ya Azam ambayo awali ilimfukuza kocha Neider dos Santos baada ya kufungwa na ikawa chini ya Itamar Amorin.

Itamar aliondoka kwa sababu ya kuzidiwa nguvu na wachezaji wasio na nidhamu mbele ya uongozi na timu akakabidhiwa kocha Stewart Hall, lakini aliondolewa katika mazingira ambayo hayakueleweka na akaajiriwa kocha Boris Bunjak kutoka Serbia.

Mserbia huyo hakudumu baada ya kufungwa na Simba naye akafukuzwa na kurudishwa Stewart na akafanikiwa kuzifunga Simba na Yanga katika msimu wa 2013/14, lakini haikutosha baada ya mzunguko wa kwanza, akaambiwa aondoke. Timu hiyo ikakabidhiwa kwa Omog.

Advertisement