Barnes wa Liverpool kunoa vijana

Mbunge wa Tabora Kaskazini, Almas Maige (kushoto), akikabidhi mchango wa fedha kwa nahodha wa Serengeti Boys, Issa Makamba wakati timu hiyo ilipotembelea Bunge mjini Dodoma jana. Picha na Emmanuel Herman.

Muktasari:

Serengeti Boys imefuzu kwa mara ya kwanza kucheza fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana U17 nchini Gabon

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa zamani wa timu ya Liverpool, John Barnes anatarajiwa kutua nchini Machi mwaka huu kwa ajili ya kuendesha kliniki ya soka kwa vijana wa timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys.

Sambamba na hilo, Barnes pia atahudhuria awamu ya pili ya mashindano maalumu ya Kombe la Standard Chartered, ambayo yatashirikisha timu tatu kutoka nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.

Mtendaji mkuu wa Benki ya Standard Chartered Tanzania, Sanjay Rughani alisema ujio wa Barnes unalenga kuimarisha vipaji vya soka kwa vijana wa Kitanzania.

“Tutahakikisha Barnes anatumia ujuzi kadri atakavyoweza ili kuvinufaisha vipaji vya hapa. Sisi wadhamini wa timu ya Liverpool na iwapo kama ataridhishwa na kuvutiwa na vipaji vya baadhi ya wachezaji, tutaangalia namna ya vipaji hivyo vinapata nafasi ya kujiunga na timu za vijana za Liverpool,” alisema Rughani.

Kuhusu mashindano hayo ya Standard Chartered, Rughani alisema awamu ya kwanza itashirikisha timu 32, ambazo zitacheza kwa mtindo wa mtoano ili kupata timu itakayoiwakilisha Tanzania.

Mshindi wa mashindano awamu ya pili, wachezaji wake watapata fursa ya kwenda kufanya ziara kwenye timu ya Liverpool na gharama zote zitakuwa chini ya benki hiyo.

Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Dioniz Malinzi aliipongeza benki hiyo kwa kuunga mkono harakati za kukuza michezo nchini.

“Mchezo kama mpira wa miguu, unasaidia kutengeneza fursa kwa vijana pia inaweza kuimarisha uchumi wa nchi. Nawaahidi kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano katika juhudi zenu,” alisema Malinzi.

Katibu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Selestine Mwesigwa aliishukuru Standard Chartered huku akiiomba sapoti zaidi ya kukuza soka la Tanzania.

“Kwa sasa timu yetu ya vijana imefanya vizuri na kufanikiwa kufuzu fainali za mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya 17, zitakazofanyika Gabon.

“Tunaamini mtasaidia kuiunga mkono ili iweze kufanya vizuri zaidi na kufika kwenye fainali za dunia,” alisema Mwesigwa.