Ngoma, Chirwa, Bossou ‘wamkwepa’ Lwandamina

Tuesday November 29 2016
ngoma chirwa_1

Dar es Salaam. Wachezaji saba walikosekana wakati kocha mpya wa Yanga, George Lwandamina akishudia kwa mara ya kwanza mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika jana asubuhi kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini, Dar es Salaam.

Katika mazoezi hayo ya jana yaliyodumu kwa saa mbili, wachezaji waliokosa ni kipa, Benno Kakolanya, mabeki Hassan Kessy, Vincent Bossou, kiungo Haruna Niyonzima na washambuliaji Donald Ngoma, Malimi Busungu na Obrey Chirwa.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit alisema kuwa wachezaji ambao hawakuonekana mazoezini, wana ruhusa maalumu ya uongozi.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu wameanza mazoezi kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu utakaoanza Desemba 17. Yanga itaanza raundi ya pili kwa kupambana na JKT Ruvu.

Katika mazoezi hayo, Lwandamina alikuwa nje na mkurugenzi mpya wa ufundi wa Yanga, Hans Pluijm na kumwachia jukumu kocha msaidizi, Juma Mwambusi kuwanoa wachezaji.

Lwandamina alionekana akiandika vitu mbalimbali katika kile alichokuwa akikiona katika mazoezi hayo na baada ya mazoezi aliliambia gazeti hili kuwa kazi yake kubwa katika mazoezi hayo ya kwanza ni kufuatilia ubora wa wachezaji wake.

Advertisement

“Nilikuwa ninaangalia ubora wa wachezaji, lakini kazi rasmi nitaanza kesho (leo) na nimeridhishwa na ubora wa wachezaji nafikiri kidogo nimeanza kupata mwanga wa wapi pa kuanzia,” alisema Lwandamina.

Katika hatua nyingine, Mzee Ibrahim Akilimali alisema wazee wote wa timu hiyo wanamkubali Lwandamina na wanachohitaji kuona kwake ni kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.

Akilimali alisema timu yao imecheza mechi nyingi za kimataifa misimu miwili iliyopita, lakini walikuwa hawafiki mbali zaidi kama wanavyotarajia.

“Ukweli bila ya kuficha, wazee wote wa Yanga nikiwamo mimi mwenyewe hatuna shaka na ujio wa Lwandamina na tuna matumani makubwa kuwa ataleta kitu katika kikosi chetu ambacho tunatamani kuona kinafanya vizuri zaidi kimataifa.”

Advertisement