Aliyefukuzwa Kenya ailalamikia serikali

Muktasari:

Serikali imesema kwamba ilimtimua mwanasiasa huyo mbishi kwa sababu aliasi uraia wake wa Kenya miaka kadhaa nyumai na kwamba wakili huyo hakushughulika kuchukua upya uraia halali.


Nairobi, Kenya. Mwanasheria maarufu aliyejitangaza kuwa jenerali wa Vuguvugu la Kukaidi Amri (NRM) Miguna Miguna amesema kufukuzwa kwake ni ukiukwaji wa haki zake za kikatiba.

Mwanasheria huyo amemlaumu Waziri wa Mambo ya Ndani, Fred Matiang'i kwa kumtimua kwa nguvu na kumsafirisha kwenda Canada kwa kisingizio cha uraia kwamba aliukana, “Sijawahi kamwe kuukana uraia wangu wa Kenya na kamwe sitafanya hivyo. Wala sijawahi hata kufikiria hilo," alisema Miguna.

 

"Hata kama mtu alikuwa na nia ya kunipeleka mahali popote kwa sababu yoyote, kuna taratibu za kisheria zilizopaswa kufuatwa na haki za msingi ambazo zinapaswa kuzingatiwa lakini ambazo Matiang'i amekiuka," Miguna aliongeza.

Serikali imesema kwamba ilimtimua mwanasiasa huyo mbishi kwa sababu aliasi uraia wake wa Kenya miaka kadhaa nyuma na kwamba wakili huyo hakushughulika kuchukua upya uraia halali.

Hata hivyo, kauli hiyo imezua hisia kali huku serikali ikilaumiwa kwa kutoa visingizio duni kujitakasa kwa kukiuka haki za Miguna.

Alisafirishwa usiku kwa ndege ya shirika la KLM kutoka Nairobi kwenda Amsterdam licha ya amri ya mahakama kwamba apelekwe mahakamani Jumatano.

Mwanasheria Donald Kipkorir alipinga kuondolewa huko akisema hatua hiyo ilikuwa ukiukwaji wa katiba. "Kwa mujibu wa Ibara ya 16 ya Katiba, mtu aliyezaliwa Kenya hata kama ana uraia wa mataifa mawili, hawezi kamwe kupoteza uraia wake ... Chini ya Ibara ya 17, mgeni ambaye alipata uraia wa Kenya anaweza kupoteza ... Kuondolewa kwa Miguna ni  uvunjaji wa Katiba yetu."

Jaji Luka Kimaru alimzuia Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) kumfungulia mashtaka yoyote ya jinai.