Mjane anayesomesha rubani kwa kuuza mkaa

Muktasari:

Mama asimulia jinsi anavyopambana kumsomesha binti urubani baada ya mumewe kufariki dunia, mwenye nyumba aizungumzia familia hiyo huku mkuu wa chuo akiusifia uwezo wa binti huyo

Dar es Salaam. Mwanafalsafa Ralph Emerson, aliyeishi duniani kati ya Mei 25, 1803 hadi Aprili 27, 1882 aliwahi kusema, “kila ukuta ni mlango.”

Naye mfanyabiashara maarufu hapa nchini Reginald Mengi kupitia kitabu chake cha I can, I must, I will ameandika katika ukurasa wa sita na saba kuwa; “Kama ukiamini nguvu ya nafsi ya ndani ya ‘nitaweza, ni lazima, nitakuwa’ basi utafanikiwa”.

Maneno ya watu hao wawili waliofanikiwa kimaisha kwa nyakati tofauti yanajidhihirishwa na mwanamama, Bahati Masebu (41), mkazi wa Kunduchi jijini Dar es Salaam anayemsomesha bintiye Nyamizi Ismail (20), elimu ya urubani wa ndege kwa kuuza mkaa.

Ada ya masomo hayo inakadiriwa kuwa Sh100 milioni.

Akizungumza na Mwananchi nyumbani kwake, Bahati anasema anamsomesha Nyamizi katika Chuo cha Tanzania Aviation University (Tauc) kilichopo Tabata.

“Alipokufa mume wangu (2013) niliona ukuta umekuja maishani mwangu, lakini ukuta huo nikaufanya kuwa mlango na leo ninajivunia walau nimekamilisha nusu ya ndoto ya mwanangu,” anasema Bahati.

Anasema tayari mwanaye amehitimu stashahada (diploma) ya masomo ya ofisa mwendeshaji wa ndege na mwakani anatarajia kuendelea na ngazi ya juu.

Mama huyo anasema Nyamizi ataendelea na masomo hayohayo ya mwaka mmoja na nusu ili aweze kupata leseni ya urubani.

“Ada yake ninayotarajia kulipa inakadiriwa kuwa Sh80 hadi Sh100 milioni kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu. Nina imani atasoma na atamaliza, iwe kwa kukopa ama kwa kuomba.”

Alivyomsomesha stashahada

Bahati anasema haikuwa kazi rahisi kwake kumsomesha mwanaye katika ngazi ya stashahada ya urubani hadi akamaliza masomo.

“Nilijitoa kafara baada ya mume wangu kufariki (dunia) kwa ajali ya gari akitokea kazini na kuniachia watoto watatu na mimba ambayo bahati mbaya ilitoka kutokana na mshtuko,” anasema mama huyo.

Anasema awali kabla mumewe hajafariki, Nyamizi alimwonyesha baba yake nia ya kusomea urubani na alimsumbua mara kwa mara, jambo ambalo lilisababisha afuatilie chuo kinachotoa mafunzo hayo.

“Katika kufuatilia wakati huo Nyamizi alikuwa akisoma sekondari kidato cha pili, (baba yake) akapata chuo cha Tauc ambacho alielezwa ili iwe rahisi kujiunga inatakiwa (Nyamizi) awe mwanachama wa masomo ya anga.”

Anasema, “Baba yake alimuunganisha na kuwa mwanachama wa masomo ya anga akiwa kidato cha pili, ambapo alikuwa akimlipia Sh60,000 kwa mwaka.”

“Baada ya mume wangu kufa, binti yangu alilia kwani alifikiri ndoto yake ya kusomea urubani ambayo ni ya muda mrefu itapotea. Aliamini mama yake sitaweza kufanya hivyo kutokana na kuwa nilikuwa mama wa nyumbani.”

Anasema kilio cha mtoto wake kilimuumiza na kufikiria ni vipi atatimiza ndoto zake bila baba yake kuwepo ambaye ndiye aliahidi kumsomesha.

Bahati anasema alichukua fedha za rambirambi ya msiba wa mumewe ambazo zilikuwa Sh500,000 na kuzigawa katika majukumu mbalimbali ikiwamo kununua chakula na zilizobaki, Sh300,000 alianzisha biashara. “Nilichukua kiasi kilichobaki nikaanza biashara ya kuuza sabuni za maji na nikafungua gege la mboga, matunda na mkaa.”

Anasema faida aliyopata katika biashara ya mkaa aliipeleka kwenye vicoba na ya genge na sabuni aliitumia kununua mahitaji ya nyumbani na kuwahudumia wanawe.

“Baada ya mtoto wangu kumaliza kidato cha nne alianza rasmi masomo ya urubani ambapo kwa mwaka wa kwanza nilitakiwa kulipa Sh8 milioni. Sikuwa na kiasi hiki cha pesa. Nilikuwa na Sh550,000 tu,” anasema mzazi huyo.

“Dada (mwandishi) niliamka nikamfuata mkuu wa chuo, nikamlilia niwe ninalipa kidogo kidogo. Bahati nzuri yule mkuu alinielewa na kwa sababu anamfahamu binti yangu uwezo wake darasani akaniruhusu nilipe nusunusu.”

Anasema, “Nilianza kutembea kama kichaa kwenye ofisi za watu, misikitini na barabarani kuomba. Nililazimika kulala porini nikitafuta mkaa wa kuuza, kila nikipata Sh50,000 ninapeleka hadi mwanangu amemaliza awamu ya kwanza ya masomo yake.”

Bahati anasema, ulifika wakati akakosa fedha na mtoto wake akakaa nyumbani wiki mbili bila kwenda chuo kwa kukosa ada, ambapo alilazimika kuuza vitu vya ndani kisha akaenda Ikulu akidhamiria kumuomba Rais amsaidie.

“Sijui nilipata wapi ujasiri wa kwenda Ikulu kumuomba Rais walau anisaidie nilipe ada ya mwanangu, lakini niliishia kuzungushwa na mwisho nikaambiwa na watu wa mapokezi kwamba Rais hana mfuko wa kusomesha watu. Niliumia, nikarudi nyumbani ninalia,” anasema.

Nyamizi anasemaje?

Kwa upande wake, Nyamizi anasema ndoto yake ni kuwa rubani wa mashirika ya ndege ya ndani na nje ya nchi. “Napenda nifike na nitafika (huko) bila kujali hali ya uchumi wa mama,” anasema.

“Najua mama yangu ananisomesha katika mazingira magumu, nina imani machungu yake hayatakwenda bure. Mama yangu analala porini siku mbili aking’atwa na mbu kusaka mkaa ili mimi nisome, huwa inaniumiza na kunipa nguvu ya kusoma kwa bidii.”

Anasema amehitimu elimu ya ofisa mwendeshaji wa ndege ambayo inampa fursa ya kufanya kazi kama msaidizi wa rubani, lakini nia yake ni kuwa rubani.

Ili aweze kufika hapo, anasema anatakiwa kusoma masomo mengine na ili aweze kuhitimu anatakiwa kulipa ada isiyozidi wala kupungua Sh100 milioni. Anasema, “Namuomba Mungu kama alivyonisaidia nikamaliza kozi ya ofisa mwendeshaji wa ndege, naomba Mungu huyohuyo aniwezeshe nimalize kozi yangu ya kurusha ndege na ninaomba wasamaria wema wamsaidie mama ili anilipie ada nikamilishe ndoto yangu.”

Mkuu wa chuo

Mkuu wa Chuo cha Tauc, Challanga William anasema Nyamizi ni mwanafunzi mwenye uwezo mkubwa darasani kiasi kwamba hata chuo kimekuwa kikimtumia kama mwalimu msaidizi wa masomo ya aga. “Kiukweli huyu binti ana uwezo mkubwa wa masomo ya anga, endapo ataendelea zaidi na zaidi kwa hapa nchini tunaweza kuwa na rubani hodari zaidi kuwahi kutokea,” anasema William.

Anasema pamoja na uwezo wake mkubwa, mama yake amekuwa akimsomesha katika mazingira magumu kwa kuuza mkaa na kuna wakati akikosa ada huwa wanamvumilia mzazi huyo.

William anasema, Nyamizi amehitimu mafunzo ya stashahada na kupata daraja ‘A’ ambapo kwa sasa anapaswa kusomea uendeshaji wa ndege, umeneja uendeshaji wa ndege pamoja na leseni ya uendeshaji wa ndege.

Baba mwenye nyumba

Akizungumzia maisha ya familia ya Bahati, mmiliki wa nyumba anayoishi, Mohammed Ngambo, anasema aliamua kumsamehe kulipa kodi mama huyo tangu mumewe alipofariki dunia ili aweze kusomesha bintiye. “Huyu mama ni mpangaji wangu, baada ya mume wake kufa amekuwa akiishi maisha magumu yeye na watoto wake, hakuna ndugu anayemsaidia, kazi yake ni kuuza mkaa anasomesha mtoto wake chuo cha urubani na mwingine anasoma yuko sekondari, mdogo kabisa yuko shule ya msingi,” anasema Ngambo.