Mo azungumza

Muktasari:

Mfanyabiashara huyo kwa mara ya kwanza ameonekana hadharani baada ya kutekwa hivi karibuni, viongozi wa dini wamuangushia dua, mambo mengi yaibuka

Dar es Salaam. Mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji ‘Mo’ jana aliibuka hadharani kwa mara ya kwanza tangu aachiwe na watekaji wakati alipokwenda kuswali katika msikiti wa Shia Ithnasheri uliopo katikati ya jijini Dar es Salaam.

Baada ya kuswali mchana, Dewji aliungana na wajumbe wa Kamati ya Haki na Amani ya Mkoa wa Dar es Salaam inayoundwa na viongozi wa dini kwenye msikiti huo jioni kwa ajili ya kufanya ibada ya kumshukuru Mungu baada ya kuachiwa na watekaji na akatumia nafasi hiyo kutoa ushuhuda.

Kuibuka kwake hakukupita bila ya matukio; taarifa zilienea haraka, watu wakamzunguka wakati akitoka msikitini na walioweza kupenya ulinzi, walibahatika kushikana naye mikono na wengine walipata sadaka kutoka kwa mfanyabiashara huyo anayemiliki viwanda, mashamba pamoja na kuuza vinywaji na nafaka.

Mo Dewji, ambaye ni mtendaji mkuu wa kampuni ya Mohammed Enterprises Limited (MeTL) inayojishughulisha na biashara hizo za uzalishaji viwandani na uuzaji wa vyakula, alitekwa alfajiri ya Oktoba 11 akiwa Hoteli ya Colosseum iliyo maeneo ya Oysterbay ambako alienda kufanya mazoezi.

Alionekana usiku wa Oktoba 20 baada ya watekaji, ambao Jeshi la Polisi limewaelezea kuwa ni watu wanaozungumza kwa lafudhi ya nchi za kusini mwa Afrika, kumtelekeza kwenye viwanja vya klabu ya Gymkhana iliyo katikati ya jiji la Dar es Salaam.

Hadi jana, Jeshi la Polisi halijaeleza kama limefanikiwa kuwakamata watu kwa tuhuma za kuhusika katika tukio hilo la kwanza la aina yake kwa mfanyabiashara mkubwa kutekwa, zaidi ya kuwashikilia kwa mahojiano walinzi wa Colosseum, wafanyakazi na wengine ambao baadhi wameachiwa kwa dhamana.

Jana, Mo Dewji, aliibuka katika msikiti huo, akiwa amevalia shati jeusi la mikono mirefu, sweta nyepesi na chini akiwa amevalia suruali aina ya jeans, akiwa na mtu anayeonekana kuwa ni mlinzi wake aliyekuwa akimtengenezea njia kila alipotaka kwenda kwa kudhibiti watu waliojitokeza mbele yake.

Mo alionekana kuwa na sura tofauti na ile ya siku alipoachiwa na watekaji; alikuwa amevalia miwani ya rangi nyeusi, amenyoa ndevu na kuchana nywele zake katika muonekano wake wa kawaida.

Lakini Mo Dewji, ambaye kwa kawaida ni mchangamfu na muongeaji, hakuonekana kurudia katika hali yake ya kawaida. Alionekana mpole na ambaye alikuwa akijitahidi kuonyesha tabasamu na uchangamfu wakati alipokuwa akisalimiana na watu nje ya msikiti huo baada ya sala, wengi wakitaka kumpa pole kuonyesha upendo kwake

“Hata sisi tulikuwa na kiu ya kumuona ili kumfariji,” alisema mmoja wa walinzi wa msikiti huo ambaye hakutaka jina lake litajwe.

“Amepitia katika kipindi kigumu kwa matatizo yaliyomfika.”

Hali ya ulinzi

Kwa kawaida maeneo ya nje ya msikiti huo, huwa kuna askari wa ulinzi kutoka kampuni binafsi, lakini jana walionekana watu waliovalia kiraia wakizungukazunguka katika magari ya waumini yaliyokuwa yameegeshwa nje kuhakikisha hayazuii mlango, huku wauzaji wa matunda wakitakiwa kusogea upande wa pili wa msikiti huo, tofauti na inavyokuwa siku zote za Ijumaa.

Baada ya ibada kuisha majira ya saa 7:30 mchana, waumini walianza kutoka msikitini na kusimama katika vikundi, wengine wakionekana kutaka kumsalimu tajiri huyo kijana ambaye amejiongezea umaarufu baada ya kufanikiwa kushinda zabuni ya kuinunua klabu ya michezo ya Simba ya jijini Dar es Salaam.

Wengi waliokuwa wametoka msikitini na kusimama nje, walikuwa wameelekeza macho yao kwenye lango la kutoka na majira ya saa 7:45 mchana, sauti za baadhi yao zikasikika zikisema “huyo” kumaanisha mtu waliyekuwa wakimsubiri, anatoka.

Wakati akitoka, alisalimiana na baadhi ya waumini kabla ya kuelekea kwenye gari yake aina ya Range Rover ya rangi nyeusi, ambayo namba zake za usajili ni “Mo1”.

Baadhi walimfuata kwenye gari na alipoona wale ambao husubiri waumini nje ya msikiti kwa lengo la kuomba msaada, alishusha kioo na kuwapa sadaka.

Asimulia alivyofungwa kitambaa

Jioni, Mo Dewji alipata nafasi ya kutoa ushuhuda wakati wa ibada ya shukrani, na alitumia dakika tano kuzungumza.

Alisema waliomteka walimfunga kitambaa usoni na hakuwa akitambua kama ni usiku au mchana, lakini aliendelea kumuomba Mungu na kuiombea familia yake.

Alisema kulikuwa hakuna chochote cha kuweza kumsaidia zaidi ya Mungu na akawashukuru viongozi wa dini, Watanzania, ndugu na marafiki zake kwa kumuombea wakati akiwa mateka.

“Wazazi wangu najua Mungu alikuwa amewapa mtihani mkubwa sana,” alisema Mo.

“Naahidi kuwa nitaendelea kuwa mwanadamu mzuri, kumuabudu Mungu zaidi, kuwa msaada kwenye jamii, kushirikiana bega kwa bega na Watanzania kwa kuwasaidia masikini, yatima, na mambo yanayoleta maendeleo kwa nchi yetu,” alisema Mo, anayetajwa kuwa na utajiri wa Sh3.5 trilioni.

Nyongeza na Kelvin Matandiko