Moto waanza kuwaka kiti cha Mbowe Chadema

Muktasari:

  • Habari zilizolifikia Mwananchi zinasema kumeibuka pande mbili, moja ikitaka Mbowe ang’atuke apishe wengine kukiongoza chama hicho kikuu cha upinzani nchini, huku nyingine ikitaka aendelee na uongozi kwa kuwa hakuna mbadala wake.

Dar es Salaam. Chadema imeanza uchaguzi kuwapata viongozi wake huku kukiwa na minong’ono kwamba kuna wanachama wanaotaka mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe ang’atuke madarakani.

Habari zilizolifikia Mwananchi zinasema kumeibuka pande mbili, moja ikitaka Mbowe ang’atuke apishe wengine kukiongoza chama hicho kikuu cha upinzani nchini, huku nyingine ikitaka aendelee na uongozi kwa kuwa hakuna mbadala wake.

Mbowe aliyeanza kukiongoza chama hicho mwaka 2004 akichukua nafasi ya Bob Makani amekuwa akielezwa kukijenga chama hicho ikiwamo kukiongoza kupata madiwani na wabunge wengi.

Wanaotaka Mbowe ang’oke wana hoja kwamba, muda umefika wa mwenyekiti huyo kupisha mtu mwingine katika nafasi hiyo wakiamini mu huyo atakuwa na mtazamo mpya.

“Ni kweli mwenyekiti ameleta mabadiliko na uongozi mzuri ndani na nje ya chama, lakini wakati umefika kwake kukaa pembeni na kuwaachia wengine waongoze,” alisema mmoja wa mwanachama ndani ya Chadema aliyeomba hifadhi ya jana lake.

Alisema, “Najua ni ngumu hili kutokea lakini kama unavyojua uongozi ni kurithishana na ingawa sijaona nani anaweza kuvaa viatu vyake, ila akijitokeza, mwenyekiti amwachie.”

Upande wanaotaka Mbowe aendelee wana hoja kwamba, kwa sasa ndani ya chama hicho hakuna mbadala labda kwa siku za usoni na wasingependa kuona aking’atuka.

Juhudi za kumpata Mbowe kuzungumzia suala hilo zilikwama jana kutokana na kuwa kikaoni.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema kwamba hawana taarifa za mtu yeyote aliyeonyesha nia ya kugombea uongozi nafasi ya juu ya chama hicho.

“Kama wapo wanapiga ramli, lakini hatujasikia hizo taarifa. Uchaguzi wa ngazi ya taifa unatarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu sasa sielewi hayo maneno yanatoka wapi sasa hivi,” alisema Mrema.

Diwani wa Ubungo, Boniface Jacob alisema ataungana na wale wote watakaotaka Mbowe agombee kwa mara nyingine nafasi hiyo.

Jacob ambaye pia ni mjumbe wa kamati kuu ya Chadema alieleza sababu za kumuunga mkono Mbowe kugombea tena nafasi ya uenyekiti kwamba, ni kiongozi makini na mwenye ushawishi mkubwa.

“Chadema kimepitia hatua ngumu, ikiwamo misukosuko lakini Mbowe amesimama imara na hakuyumba. Kwa hali ilivyo tulidhani Mbowe atasema sasa basi lakini hajakata tamaa mzee huyu,” alisema Jacob ambaye pia ni Meya wa Ubungo.

Alisisitiza kuwa, hakuna ubaya wowote kwa Mbowe kuendelea kubaki katika nafasi hiyo na kwamba, hao wasiotaka agombee wanatoka nje ya Chadema na kwa masilahi yao binafsi.

Katibu wa Baraza la Wazee Chadema, Roderick Lutembeka alisema kwamba hawezi kuzungumzia suala hilo kwa kuwa hajakutana na viongozi wenzake.

“Naomba nisiseme lolote kuhusu hili, kama msimamo wa wazee labda hadi tukutane na wenzangu,” alisema Lutembeka.

Katibu wa Uenezi wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), Edward Simbeye alisema kwamba wakati ukifika watamuunga mkono mwanachama yeyote atakayejitokeza kugombea nafasi hiyo ya juu ya uongozi.

“Hata hivyo, Bavicha bado hatujakaa na kujadili jambo hili. Tukijadili tutatoa msimamo wetu kama vijana,” alisema Simbeye.

Awali, Mrema alisema kwamba mwaka huu ni wa uchaguzi ndani ya chama hicho na tayari wameanza kwa ngazi za msingi, matawi na mashina.

Aliongeza kwamba hatua hiyo ikikamilika, watahamia katika ngazi ya jimbo, wilaya na kanda kisha kwenda ngazi ya taifa itakayofanyika mwishoni mwa mwaka huu.

“Nguvu kubwa imeelekezwa ngazi hii (msingi, matawi na mashina) kwa sasa na ndiyo maana viongozi wakuu akiwamo Mbowe wanashiriki kikamilifu katika mchakato huu,” alisema Mrema.