Mrithi wa Kinana kujulikana leo

Muktasari:

Kuondoka kwa Kinana pamoja na kuwapo uwezekano wa kufanyika marekebisho ndani ya sekretarieti ni mambo yanayotazamiwa kuifanya CCM kuwa na mabadiliko makubwa.

Dar es Salaam. Hayawi hayawi yamekuwa. Hivi sasa ni dhahiri kuwa uongozi wa juu wa CCM utakuwa na sura mpya kuanzia leo, baada ya jana Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana kuwaaga wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).

Kutokana na uamuzi huo, kikao cha NEC kinachoendelea Ikulu jijini Dar es Salaam kitakuwa na jukumu la kuchagua katika mkuu mpya kutokana na mapendekezo yatakayowasilishwa kwake na mwenyekiti.

Jana, kikao hicho kilichagua wajumbe wapya sita, watatu kutoka kila upande wa Muungano kuingia kwenye Kamati Kuu ili kutimiza idadi ya wajumbe 24 wanaotakiwa kwa mujibu wa katiba ya chama hicho.

Kuondoka kwa Kinana pamoja na kuwapo uwezekano wa kufanyika marekebisho ndani ya sekretarieti ni mambo yanayotazamiwa kuifanya CCM kuwa na mabadiliko makubwa.

Magufuli amruhusu

Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli jana alitangaza kuridhia kujiuzulu kwa Kinana.

Hatua hiyo inafuatia maombi ya mara kwa mara ya katibu huyo kutaka kujiuzulu ambapo mara kadhaa amemuandikia barua mwenyekiti huyo wa Taifa akieleza kusudio lake na kuomba apumzike.

Julai 2016, katika mkutano mkuu maalumu wa CCM ambao Rais mstaafu Jakaya Kikwete alikabidhi uenyekiti kwa Magufuli, Kinana aliwasilisha barua ya kujiuzulu nafasi hiyo, lakini kiongozi huyo wa nchi alimkatalia akimuomba aendelee kumsaidia kutokana na uzoefu wake.

Rais Magufuli pia aliwataka manaibu katibu wakuu wawili na sekretarieti nzima ya chama hicho kuendelea na kazi.

Lakini jana wakati kikao cha NEC kikiendelea, mwenyekiti huyo aliridhia ombi hilo akisema kuwa hiyo ni mara ya pili kwa kiongozi huyo kuomba kung’atuka.

“Huyu kweli ameshaomba zaidi ya mara mbili na zile nyingine alikuwa akiomba kisirisiri namkatalia; akiweka neno hilo naanzisha pointi nyingine lakini nikatambua pia juhudi kubwa, kwa kujiuliza ni makatibu wakuu wangapi wamekuwa katika Chama cha Mapinduzi tangu tupate uhuru?

“Nikajua kwamba walikuwapo hata wengine mimi sijaanza shule ya msingi na kila mmoja alifanya kazi yake akamaliza wakati wake lakini nikatambua pia umri wa mheshimiwa Kinana; nikamuita mzee Shein. Mzee Shein akaniambia kwa kweli tumkubalie,” alisisitiza Rais Magufuli.

Hata hivyo, alisema baadaye aliamua kumuita makamu wa mwenyekiti, Philip Mangula kumuuliza kama ni sahihi kwa katibu mkuu kuondoka, naye pia aliridhia.

“Mzee Mangula naye akasema tumkubalie, kuchoka kupo. Nikaona nimuite tena jana (juzi), labda atakuwa amebadilisha mawazo, nikamwambia bwana mimi nataka nibadilishe uendelee tu, akasema hapana naomba uniruhusu. Na mimi nimeridhika na nimejiridhisha na dhamira yangu ya moyo kwa kazi kubwa aliyofanya ndugu yetu lakini ukweli nimeridhia nimkubalie amalize muda wake wa ukatibu mkuu tutafute katibu mkuu mwingine,” alisema mwenyekiti huyo.

Kinana aaga

Akizungumza mara baada ya wajumbe wa NEC kukubali ombi lake, Kinana alisema lazima tukubali kuwa kuna wakati wa kufanya kazi na wakati wa kupumzika.

“Ninaelewa ugumu mnaoupata wa kutonikubalia, mnakubali tu mnaelewa na kila nikiwatazama napata meseji nyingi na hata nyuso zenu nikizitazama, hivi bado mnauliza naweza badili mawazo na hata mwenyekiti amesema tumekuwa na makatibu wakuu wengi tangu Chama cha Mapinduzi kizaliwe.

“Tumekuwa na makatibu wakuu saba, kwa hiyo si ajabu kwa katibu mkuu wa sasa naye akiachia ngazi apishe mwingine. Namshukuru mwenyekiti kwa kukubali, namshukuru makamu mwenyekiti Zanzibar kwa kunikubalia, namshukuru mzee Mangula kwa kunikubalia. Mimi mara nyingi sana ninakwenda nyumbani kwa Mangula nazungumzazungumza naye na ni mmoja wa mtu ambaye huwa namshawishi kwa kuwa najua anazungumza na mwenyekiti wetu,” alisema Kinana.

Alisema mara ya mwisho walikutana na mwenyekiti katika ofisi ndogo za chama hicho zilizopo Lumumba na alimuuliza Mangula kama wamruhusu ajiuzulu na cha kufurahisha kiongozi huyo hakumuangusha.

“Tulipokutana ofisi ya chama pale; mimi, mwenyekiti na makamu kwa kweli mzee Mangula namshukuru tukiwa pale Rais alikuuliza wewe unasemaje? Ulijitoa muhanga ukamwambia mwenyekiti, mimi nadhani tumruhusu apumzike. Mwenyekiti kama alikukasirikia kidogo kwamba mimi nadhani utakuwa upande wangu lakini sasa wewe mbona unakuwa tena upande wa katibu mkuu, kwa hiyo mwenyekiti mimi nakushukuru umeelewa kila lililo na mwanzo lazima liwe na mwisho.”

Kinana anaondoka huku akiwa ameitumikia CCM na Serikali kwa muda mrefu na alifanya kazi na marais wote wa Tanzania.

Ndani ya utumishi wake CCM, hususan katika nafasi ya ukatibu mkuu ambayo ameitumikia kwa takriban miaka saba, alishiriki katika kuasisi na kutekeleza operesheni mbalimbali za kukijenga chama hicho.

Sita wachaguliwa CC

Badaye jioni jana, taarifa ya CCM iliyosainiwa na Katibu wa NEC- Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole ilitaja majina sita ya wajumbe wa Kamati Kuu (CC) waliochaguliwa na NEC.

Kwa upande wa Tanzania Bara walichaguliwa Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda; mbunge wa zamani wa Afrika Mashariki, Makongoro Nyerere na mwanamuziki Khadija Shabani maarufu kwa jina la Keisha.

Kwa upande wa Zanzibar waliochaguliwa ni Afadhari Taiibu Afadhari, Kombo Hassan Juma na Lailah Burhan Ngozi.

Wajumbe hao walichaguliwa kutokana na majina 18, tisa kutoka Bara na tisa kutoka Zanzibar yaliyopendekezwa na mwenyekiti kuwania nafasi hizo.

Awali, kikao hicho kilipitisha majina ya wajumbe wawili wapya wa NEC, Pinda na Makongoro walioteuliwa juzi na mwenyekiti.

Kwa uchaguzi huo, wajumbe wa NEC wametimia 24 wanaotakiwa baada ya kupunguzwa kutoka 34.

Mbali na uchaguzi huo, kikao hicho kinatarajiwa kutoa mwongozo juu ya ripoti ya uchunguzi kuhusu mali za chama iliyowasilishwa hivi karibuni ikieleza kuonyesha ubadhirifu mkubwa.

Nyongeza na Eliasi Msuya