Mteka watoto auawa kwa kupigwa risasi

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo

Arusha. Mtu anayetuhumiwa kuteka watoto na kuua wawili, Samson Petro ameuawa usiku wa kuamkia juzi baada ya kupigwa risasi alipojaribu kuwatoroka polisi wakati akiwapeleka nyumbani kwa mtuhumiwa mwenzake.

Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alisema jana kuwa baada ya mahojiano aliwaambia polisi kuwa mtu aliyekuwa akishirikiana naye yupo eneo la Mkonoo, nje kidogo ya jiji na walipokaribia alijaribu kutoroka.

“Kama mnavyokumbuka jana (juzi) tulikutana nikawapa taarifa ya mtuhumiwa aliyekua akiwateka watoto na aliwaua watoto wawili na kuwatumbukiza katika shimo la maji taka,” alisema Kamanda Mkumbo.

“Tuliendelea na mahojiano na mtuhumiwa huyo na ilipofika majira ya saa 5:00 usiku (Jumatano) alitoa ushirikiano wa kutosha mwenzake na walipofika njiani alijaribu kutoroka na ndipo alipopigwa risasi za miguu.”

Alisema baada ya kumjeruhi miguu yote miwili, polisi waliamua kumpeleka Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru kwa ajili ya matibabu na baadaye alifariki dunia.

Alisema awali kijana huyo alitoa ushirikiano kwa polisi wakati wa mahojiano na ndipo alipowaeleza kuwa angewapeleka sehemu ambayo anaishi mtu aliyekuwa akishirikiana naye.

Kamanda Mkumbo alisema polisi itaendelea na upelelezi ili kuwakamata watu wote waliohusika na utekaji wa watoto ili kuhakikisha matukio hayo hayajirudii.

Kuhusu askari wa Kikosi cha Kuzuia Fujo (FFU), ambaye ni ndugu wa mtuhumiwa, Kamanda Mkumbo alisema baada ya uchunguzi imebainika hahusiki na uhalifu.

Alisema alikuwa akiishi na mtuhumiwa huyo, lakini baada yattabia yake kushindikana, alimtaka arudi kwao Katoro wilayani Geita na ndipo alipotafuta  sehemu ya kuishi kabla ya utekaji.

Watoto waliotekwa ni Moureen David (6) na Ikram Salim (3) ambao miili yao ilikutwa ndani ya shimo la majitaka.