Mtoto wa miaka mitatu aibwa kanisani Dar

Mtoto Beauty Yohana 

Muktasari:

Baba wa mtoto huyo Yohana Isango amesema mwanaye Beauty Yohana alipotea Septemba 23, 2018, walipokuwa kanisani wakisali huku mwanaye huyo akiwa katika ibada ya watoto ‘Sunday School’

Dar es Salaam. Mfululizo wa matukio ya wizi wa watoto umeibuka tena na safari hii umefanyika katika Kanisa la FPCT lililopo Mbezi Mwisho jijini Dar es Salaam baada ya mtoto Beauty Yohana (3) kuchukuliwa na mtu asiyefahamika.

Tukio hilo lilitokea juzi Jumapili wakati mtoto huyo alipokwenda kanisani na mama yake, Lucy Maganga.

Walipofika mama alimpeleka bintiye kwenye ibada ya watoto (Sunday school) naye akaingia kanisani kuendelea na ibada.

Akisimulia mkasa huo, baba wa mtoto huyo, Yohana Isango amesema wakati ibada inaendelea alionekana binti mmoja mweusi akiwa nje ya kanisa na baadaye alikwenda chumba cha watoto na kumtaka Beauty ili akanywe dawa.

“Huyo msichana alikwenda na kumwambia mwalimu kwamba mama Bless (mke wangu) anamuita Beauty ili akampe dawa. Kwa kuwa mwalimu naye ni binti mdogo, hakujiuliza sana, akamruhusu kuondoka naye,” anasimulia Isango.

Isango anasema msichana huyo alimchukua na kuingia naye kanisani, lakini baadaye alitoweka na mtoto huyo.

Anasema baada ya ibada kwisha, mtoto hakuonekana, wakatangaza kanisani na ndipo walipotambua kwamba ameibwa.

Isango anasema siku hiyo saa 12 jioni walipata taarifa kutoka kwa mtu anayefahamiana naye kwamba alimuona mtoto huyo maeneo ya Malamba Mawili kwa kinyozi.

Anasema mtu huyo hakuwa amepata taarifa ya kupotea kwa mtoto, hivyo hakuweza kuuliza alifikaje huko.

Isango anasema baada ya kupata taarifa ya kupotea kwa mtoto, mwanamke huyo alimpigia simu na moja kwa moja wakaenda Malamba Mawili kumtafuta mtoto na kuweka doria hadi saa tisa alfajiri lakini hawakumwona. “Nadhani alitaka kumnyoa ili kubadilisha mwonekano wake lakini tuliambiwa alikuta watu ni wengi kwenye saluni hiyo, akaondoka. Tulikaa maeneo hayo mpaka saa tisa usiku lakini hatukuona dalili zozote,” anasimulia baba wa mtoto huyo.

Anasema msichana huyo alionekana pia akila chakula kwa mama lishe Malamba Mawili akiwa na mtoto lakini mtoto alikuwa hali na alipoulizwa kwa nini mtoto hali alijibu kwamba “hapendi kula”.

“Tulitoa taarifa kituo cha polisi cha Gogoni, Mbezi na leo asubuhi (jana) nimekwenda kuripoti. Wameniambia wanaendelea na uchunguzi wa tukio hili,” anasema mzazi huyo ambaye ana watoto wawili, Bless na Beauty.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Jumanne Murilo alikiri kuwa na taarifa hizo na jeshi la polisi linaendelea na kazi ya kumtafuta.

Atakayemuona mtoto huyo awasiliane na wazazi wake kwa namba 0652316007 au kutoa taarifa katika kituo chochote cha polisi.

Tukio hilo siyo la kwanza kutokea hapa nchini, Februari 4, mtoto wa siku moja aliibwa katika wodi ya wazazi ya Hospitali ya Mkoa wa Mbeya na mwanamke aliyejifanya muuguzi.

Oktoba mwaka jana, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Ashia Ismail alikamatwa mkoani Mwanza akiwa katika harakati za kuondoka na watoto watatu waliokuwa wakiishi katika Mtaa wa Shede eneo la Mkuyuni.