Mugabe, Mangagwa uso kwa uso

Muktasari:

Upande mwingine, chama tawala cha Zanu PF ambacho Mugabe alikiasisi na kukiongoza kwa karibu miongo mine, kilimuondoa Mugabe Jumapili na kikampata muda wa mwisho wa kujiuzulu urais Jumatatu mchana au akabiliwe na mashtaka bungeni. Chama kilisema kuwa kitaanzisha mchakato huo leo bungeni.

Harare, Zimbabwe. Rais Robert Mugabe amekubali kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na makamu wa rais aliyemfukuza Emmerson Mnangagwa wakati mchakato wa kumshtaki bungeni ukianza.

Mnangagwa amekuwa nje ya nchi tangu alipofukuzwa Novemba 6 hali iliyoitumbukiza nchi katika mgogoro wa kisiasa na maelfu ya watu wakaandamana kushinikiza Mugabe mwenye umri wa miaka 93 ajiuzulu.

Mkuu wa majeshi, Jenerali Constantino Chiwenga alieleza jana kwamba ameafikiana na Mugabe kuhusu "njia ya kufuata kuhusu hali ya kisiasa nchini." Mnangagwa anatarajiwa kurejea Zimbabwe kukutana na kiongozi huyo mkongwe aliyetawala kwa miaka 37 tangu uhuru mwaka 1980.

"Taifa litafahamishwa kuhusu matokeo ya mazungumzo ya wawili hao,” Jenerali Chiwenga aliwaambia waandishi wa habari jana.

Upande mwingine, chama tawala cha Zanu PF ambacho Mugabe alikiasisi na kukiongoza kwa karibu miongo mine, kilimuondoa Mugabe Jumapili na kikampata muda wa mwisho wa kujiuzulu urais Jumatatu mchana au akabiliwe na mashtaka bungeni. Chama kilisema kuwa kitaanzisha mchakato huo leo bungeni.

Hatua ya Zanu PF ilifikiwa baada ya Mugabe kukataa wito wa kujiuzulu hata baada ya kupokwa mamlaka ndani ya chama.

Chanzo kimoja cha uhakika kililiambia shirika la utangazaji la CNN kwamba Mugabe alikuwa amekubali kujiuzulu katika mazungumzo na viongozi wa kijeshi wanaoidhibiti Zimbabwe tangu Jumatano iliyopita, na kwamba barua ilishaandaliwa.