Mugabe kutua New York na msafara wa watu 70

Muktasari:

  • Wiki iliyopita kulikuwa na ripoti zilizosema Marekani ilihoji hatua ya kujumuisha familia ya rais huyo kwenye msafara wa zaidi ya watu 70 kwenda kwenye mkutano wa mwaka wa UNGA ulioanza jana.

New York, Marekani. Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe anatarajiwa kuwasili jijini hapo kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UNGA) huku vyombo vya habari vikieleza akiwa na msafara wa watu 70 wakiwemo wa familia yake.

Wiki iliyopita kulikuwa na ripoti zilizosema Marekani ilihoji hatua ya kujumuisha familia ya rais huyo kwenye msafara wa zaidi ya watu 70 kwenda kwenye mkutano wa mwaka wa UNGA ulioanza jana.

Mkutano mkuu wa UN ulioanza jana unatarajiwa kumalizika Septemba 23 utabeba ujumbe usemao: “Kuwajali Watu Wanaopigania Amani na Maisha Bora Kwa Wote katika Dunia Endelevu.”

Ubalozi wa Marekani ulihoji kujumuishwa kwa mke wa Mugabe, binti yake Bona na mjukuu wake Simbanashe katika msafara huo wa Mugabe. Msafara huo pia umejumuisha mtoto wa kiume wa Mugabe, Bellarmine Chatunga pamoja na Russell Goreraza ambaye ni mtoto mkubwa wa Grace.

Gazeti la News Day limeripoti kwamba msafara wa rais huyo mkongwe barani Afrika unatarajiwa kutafuna zaidi ya dola za Marekani 10 milioni kama posho licha ya Zimbabwe kukabiliwa na uhaba wa fedha.

“Hati za kusafiria ziliwasilishwa wiki iliyopita kwa ajili ya kuombea viza kwenye ubalozi wa Marekani, lakini maofisa walihoji idadi ya watu katika msafara na ulikataa kutoa viza kwa mwanahabari mmoja kutoka chombo cha serikali,” gazeti la Business Africa lilinukuu vyanzo vya kuaminika wiki iliyopita.

Mugabe anatarajiwa kuwahutubia viongozi wa dunia keshokutwa Septemba 21. Ripoti ya Sauti ya Amerika imesema kwa kawaida kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 93 hutumia UN kama jukwaa la kuzisema nchi za Magharibi kwa kuweka vikwazo vinavyomlenga yeye pamoja na washirika wa karibu kutokana na rekodi mbaya ya ukiukwaji wa haki za binadamu na ulaghai katika uchaguzi.