VIDEO:Muna atua Dar, azua kizaazaa Uwanja wa Ndege

Muktasari:

Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo lililotokea leo Ijumaa Julai 6, 2018 wamesema msanii huyo baada ya kuwasili aishiwa nguvu 

Dar es Salaam. Msanii wa Bongo Movie, Rose Alphonce maarufu Muna Love amewasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam na kuzua taharuki baada ya kuondoka kuelekea kusikojulikana na kuwaacha ndugu na jamaa wakishikwa na butwaa.

Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo lililotokea leo Ijumaa Julai 6, 2018 wamesema msanii huyo baada ya kuwasili aishiwa nguvu na kulazimika kuondoka eneo hilo bila kutoa taarifa kwa baadhi ya watu waliofika kumpokea.

Muna ni mama mzazi wa Patrick (8) aliyekuwa akiishi kistaa na kuwa na umaarufu wa aina yake kwenye mitandao ya kijamii. Mtoto huyo alifariki dunia Jumatatu Julai 2, 2018 kwenye hospitali moja  jijini Nairibi, Kenya.

Leo mwili wa Patrick ndio ulitakiwa kuletwa nchini kwa shughuli za mazishi.

Tangu kifo cha mtoto huyo kumekuwa na mvutano kuhusu wapi utafanyika msiba jambo ambalo mara kadhaa limetolewa ufafanuzi na baba mzazi wa mtoto huyo, Peter Zakaria na dada wa Muna, Eve kuwa utafanyika nyumbani wa Zakaria anayeishi Mwananyamala kwa Mwakibile.

Akizungumza na MCL Digital leo Julai 6, 2018 Bazo Peter ambaye ni msemaji wa familia amesema wameshindwa kutoa mwili kwa sababu hawakuwa na nyaraka.

“Tumeshindwa kuutoa mwili wa Patrick kwa sababu hatuna document (nyaraka) kwani Muna ameondoka nazo na haijulikani alipoelekea,” amesema.

“Jana alitueleza kuwa mwili utawasili saa nne (leo) lakini tunaona amewasili yeye na kuingia kwenye gari ambalo hatulifahamu, ila inasemekana ni waumini wenzake.”

Ameongeza, “Tulivyoona hivyo ndio tukaamua kwenda kuuliza wanapotolea mizigo na tumejibiwa kuwa hakuna ndege iliyowasili na maiti kwa siku ya leo.”

Muna amewasili kwa ndege leo saa 7 mchana akitokea Nairobi nchini Kenya alikokuwa akimuuguza mwanaye kabla ya kukutwa na mauti.