Mwenyekiti Chadema, Mdee kuikabili Kamati ya Bunge

Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa kuwapata wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki, mjini Dodoma usiku wa kuamkia Jumatano. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Mbunge Kawe, Halima Mdee pia amesema ataibuka mbele ya kamati hiyo leo kujibu tuhuma za kumtukana Spika Job Ndugai.

Dodoma. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema hajui amefanya kosa gani, lakini atafika mbele ya Kamati ya Bunge ya Maadili kujibu tuhuma dhidi yake akisema si mara ya kwanza.

Mbunge Kawe, Halima Mdee pia amesema ataibuka mbele ya kamati hiyo leo kujibu tuhuma za kumtukana Spika Job Ndugai.

Spika alisema wawili hao walifanya makosa yao wakati mjadala wa nafasi za wagombea wa vyama vya Chadema na CUF katika Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (Eala) uliotawaliwa na jazba.

“Nimesikia wito wa Spika Ndugai. Nitafika kwenye kamati kwa kuwa si mara ya kwanza mimi kuitwa,” alisema kiongozi huyo wa kambi rasmi ya upinzani bungeni.

“Nimesikia wito wa Spika Ndugai. Nitafika kwenye kamati kwa kuwa si mara ya kwanza mimi kuitwa,” alisema kiongozi huyo wa kambi rasmi ya upinzani bungeni.

“Lakini sijui ninaitwa kwa tuhuma gani, lakini nitazijua hukohuko nitakapofika.”

Mbowe amefikishwa mbele ya kamati hiyo kwa tuhuma za kulitukana Bunge, Rais, Waziri Mkuu na Spika wakati alipokuwa akizungumza kuhusu uchaguzi wa wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki.

Mbunge huyo wa Hai ndiye aliyeongoza kambi ya upinzani kutetea uamuzi wa Chadema kupeleka wagombea wawili badala ya sita kugombea nafasi mbili, akisema kanuni hazilazimishi idadi kamili ya wagombea.

Mbowe pia alikuwa akijenga hoja kuwa kwa sababu nafasi za Chadema ni mbili, basi wagombea wao wawili, Lawrence Masha na Hezekiah Wenje wapite bila ya kupingwa, lakini Bunge likaamua wapigiwe kura na hivyo kutowapitisha wawili hao.

Mdee pia ametakiwa afikishwe mbele ya kamati hiyo kwa madai kuwa alimtukana spika.

Mbunge huyo wa Kawe pia aliiambia Mwananchi kuwa pamoja na ukweli kwamba yuko nje ya Dodoma kwa ajili ya shughuli za mazishi, matibabu na kimahakama, atafika mjini hapa kama alivyotakiwa.

“Niko nje ya Dodoma nashughulikia mapokezi ya mwili wa marehemu Dk Elly Macha aliyefariki akiwa Uingereza. Pia nilikuwa na kesi Dar na pia nashughulikia matibabu ya mbunge aliyegongwa na pikipiki juzi,” alisema Mdee kwa njia ya simu.

Hata hivyo, alisema atafika mbele ya kamati hiyo kama ilivyoagizwa na Spika Ndugai.

Jana asubuhi, Spika Ndugai alizungumza kwa ukali wakati akitoa maagizo ya kuitwa kwa Mbowe, Mdee na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti mbele ya kamati hiyo.

“Nimewaambieni nyie mnaomzomea Spika, kwa mara nyingine sitachoka kuwaambieni, tuna miezi hii, mitatu. Tutashughulika na kila mmoja anayejifanya ana vurugu hapa,” alisema Spika Ndugai.

“Sasa naanza na Mheshimiwa Halima Mdee ambaye yeye alimtukana Spika juzi. Katika michezo hiihii mnayofanya, Watanzania wengi sana wamesikitishwa sana na jambo hili. Wameniandikia, wamenipigia simu, wamesikitishwa sana, sana na jambo hili na si utaratibu mwema, si utamaduni wetu Watanzania. Hatufikagi hapo.

“Lakini kwa vile wenzetu wamefika hapo, na hii si mara ya kwanza kwa Halima. Hata juzi nilivumilia sana. Yaani nilivuta, nikamuomba Mungu anisaidie, nikanyamaza kimya. Ndio maana nawaambieni mara kwa mara kuwa baadhi yenu tabia zenu na mwenendo si mzuri hata kidogo.

“Kwa hiyo, moja kwa moja suala lake nalipeleka Kamati ya Maadili, iende ikakae na kulipima. Haiwezekani Bunge hili linawashughulikia walioko nje kwa utovu wa nidhamu, halafu lifumbie macho waliomo humu ndani ambao ni watovu wa nidhamu.”

Spika alisema Bunge haliwezi kuendeshwa kwa jinsi hiyo na kutoa amri kali zaidi.

“Kwa hiyo, Halima Mdee, popote pale alipo katika nchi hii. Najua hayuko Dodoma. By saa hizi kesho, yeye mwenyewe awe amejileta hapa bungeni. La sivyo akamatwe na polisi popote pale alipo, aletwe kwa pingu hapa bungeni,” alisema Ndugai huku akipigiwa makofi.

“Hatuwezi kucheza katika mambo ya msingi. Tumekuja mmojammoja na tutashughulikiana mmojammoja.”

Pia alisema Mbowe naye aripoti mbele ya Kamati ya Maadili ambayo aliitaka ianze kukutana mara moja kushughulikia masuala hayo.

Spika Ndugai amesema hayo jana mara baada ya kipindi cha maswali na majibu bungeni.

Alisema Mnyeti alifikishwa jana mbele ya Kamati ya Bunge ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge kuhojiwa kuhusu tuhuma za kuudhalilisha muhimili huo.

Mbali na Mbowe na Mnyeti, Spika Ndugai amemuagiza Mdee kufika katika kamati hiyo kabla ya saa nne leo la sivyo popote alipo atiwe pingu na apelekwe bungeni.

Alisema kamati hiyo pia jana ilikuwa inamuhoji Mnyeti kuhusu tuhuma za kulidharau Bunge.

Kikao cha Jumanne kilitawaliwa na mijadala mikali kuhusu wawakilishi wa CUF na Chadema katika Bunge la Eala, na mara nyingi mbunge mmoja alipokuwa akichangia, wanaompinga waliwasha vipaza sauti vyao na kusema maneno ya kejeli au kumtaka anayezungumza akae.

Kelele hizo pia zilichangiwa na baadhi ya vinasa sauti kutofanya kazi vizuri, hasa vya upande wanaokaa wabunge wa CCM kiasi cha Spika kutuhumu kuwa kuna watu walikuwa wanafanya hujuma.

Kikao hicho kiliisha saa 7:00 usiku baada ya kura kuhesabiwa.

Awali, baadhi ya wabunge wa CCM, Kangi Lugola na Godwin Mlinga kwa nyakati tofauti waliomba mwongozo wa Spika wakitaka Mbowe ashughulikiwe kwa madai kuwa alilidhalilisha Bunge kwa kutoa lugha zenye kuudhi.

Lugola alisema kuwa yako maneno yanayosambaa kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari yakionyesha namna Mbowe alivyowatukana wabunge na Rais kwa kuwaita wapumbavu.

Kauli kama hiyo ilitolewa na Mlinga pia akihoji sababu za Mbowe kutoitwa mbele ya Kamati ya Maadili kwa madai kuwa alidhalilisha Bunge.

“Pamoja na hoja iliyotolewa na mheshimiwa Lugola (Kangi), naomba kuongezea kuwa wakati wa uchaguzi mwaka 2010, Lawrence Masha alimpinga Wenje kuwa si raia. Je, tunachagua mtu wa kuwakilisha nchi gani, na jambo la pili huyu Masha aliposhindwa uchaguzi aling’oa hadi vitasa vya ofisi. Je huyu anafaa kweli, lakini wote hawa walikuwa na sauti pana hivi waliwakilisha jinsi gani,” alihoji Mlinga.