Mwili wa mtoto Moureen ulioopolewa shimoni wazikwa

Muktasari:

  • Wazazi na jamii imetakiwa kuwa karibu na watoto ili kuwalinda

Arusha. Vilio na simanzi vimetawala wakati wa maziko ya mtoto Moureen David (6) aliyetekwa, kuuawa na mwili wake kutupwa ndani ya shimo la maji taka pamoja na mwenzake Ikram Salim (3).

Moureen amezikwa katika makaburi ya Mbauda yaliyopo Kata ya Sombetini jijini Arusha. 

Akiongoza ibada ya mazishi, padri wa Kanisa Katoliki Laurence Boniphace amewataka wazazi wa marehemu kusamehe kila mtu katika tukio hilo na kujitayarisha kuanza maisha mapya bila ya kinyongo.

“Katika maisha yetu tunakutana na watu ambao hawajali maisha ya binadamu, hivyo ninaomba wazazi wa marehemu msamehe kwa sababu mnaposamehe mnaanza maisha mapya,” amesema.

Akizungumza baada ya kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa marehemu, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amesema Serikali inatoa rambirambi ya Sh2 milioni. Pia amewataka wakazi wa Arusha kuwa watulivu.

Gambo aliyeambatana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo amesema Serikali ilifanya jitihada kuwasaka na kuwakamata wahalifu katika tukio hilo.

Amesema jitihada za kumtia nguvuni mhalifu zilifanikishwa na vyombo vya ulinzi vya mkoa kwa kushirikiana na Mkoa wa Geita, hivyo amewaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa polisi kwa kuwafichua wahalifu.

Baba mzazi wa marehemu, David Njau amesema kufiwa na mwanaye kunasikitisha kwa kuwa hivi karibuni mtoto wake wa kwanza, Jenipher David ambaye ni mhitimu wa darasa la saba katika Shule ya Lucky Vincent alinusurika kifo katika ajali ya gari iliyotokea wilayani Karatu.

Amesema polisi walikuwa na uwezo wa kuzuia kifo cha mwanaye kwa kuwa kwa takriban wiki nzima alikuwa akiwasiliana na wahalifu wakimtaka awapatie fedha ili wamrejeshe lakini licha ya kutoa taarifa kwa jeshi hilo hawakuweza kuwakamata wahalifu.

“Nina uhakika kama polisi wangetoa ushirikiano wa kutosha wahalifu wangekamatwa na mtoto wangu asingefariki katika mazingira ya ajabu, nilijitahidi kuwapa taarifa zote za wahalifu lakini sikupewa ushirikiano,” amesema.

Njau.

 

Amesema tukio hilo linapaswa kuwa funzo kwa Jeshi la Polisi ili wanapopewa taarifa kuhusu wahalifu wachukue hatua haraka kabla ya kusubiri majanga yatokeze.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Olkeryan, Daud Safari amesema tukio hilo linapaswa kuwa fundisho kwa wazazi nchini ili kuwakemea watoto kutokubali kupokea zawadi kama pipi mitaani kwa watu wasiowafahamu.

Safari amesema matukio ya utekaji ni mageni ndani ya jamii ya Kitanzania lakini wazazi wana jukumu la kuhakikisha wanakaa karibu na watoto.

Watoto, Moureen aliyekuwa akisoma darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Lucky Vincent na Ikram, miili yao ilikutwa shimoni Septemba 5.

Wakati Moureen alitekwa Agosti 21 saa kumi na moja jioni, Ikram alitekwa Agosti 26, saa 12 jioni.

Kijana aliyehusika na matukio ya utekaji wa watoto hao Samson Petro (18), alikufa Jumatano kwa kupigwa risasi na polisi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Mkumbo alisema kijana huyo aliyekamatwa mkoani Geita alikokuwa amekimbia kabla ya kurejeshwa Arusha alitaka kukimbia alipokuwa anaenda kuwaonyesha polisi watuhumiwa wenzake wa utekaji  saa tano usiku.