VIDEO: Nabii awataka Muna Love, Peter kuishi pamoja

Muktasari:

Ametoa kauli hiyo leo katika ibada ya kuaga mwili wa mtoto wa wawili hao, Patrick aliyefariki dunia Julai 3, 2018

Dar es Salaam. Nabii Triza kutoka nchini Afrika Kusini amesema ipo haja Muna Love na Peter Zakaria kurejesha upendo na kuishi pamoja, kuwataka kutosikiliza maneno ya watu kwenye mitandao ya kijamii.

Ameyasema hayo leo Jumamosi Julai 7, 2018 katika viwanja wa Leaders Club jijini hapa kwenye ibada ya kuaga mwili wa mtoto wa wawili hao, Patrick aliyefariki dunia Julai 3, 2018 Nairobi,  Kenya alikokuwa akipatiwa matibabu.

Amesema maneno yaliyoibuka katika mitandao ya kijamii kuhusu mazishi ya mtoto huyo pamoja na mvutano wa wapi ufanyike msiba, isiwe sababu ya wao kuvunja upendo wao.

“Leo nazungumzia upendo kwa kuwa huyu mtoto alikuwa na upendo, kwa hiyo naomba baba na mama Patrick mrudishe upendo, ni wakati wa kuishi pamoja ili kumuenzi mtoto wenu,” amesema.

“Sijaanza kumfahamu Patrick hapa Dar es Salaam. Mtoto huyu anafahamika katika nchi mbalimbali ikiwemo Afrika ya Kusini, Nigeria na Marekani kutoka na ukarimu wake na jinsi alivyompokea Mungu akiwa na umri mdogo.”

Pia, amewataka watumiaji wa mitandao ya kijamii kuacha kutumia kurasa zao za mitandao kuvuruga familia ya Muna.

"Tunashukuru sana kwa upendo uliotawala hapa kwa kuwa kila mtu alitarajia kutatokea migogoro lakini Mungu amesaidia na kila kitu kinaenda sawa,” amesema.

Akizungumza kwa niaba ya wasanii wa Bongo Movie, Wema Sapetu amesema japo hajabahatika kupata mtoto lakini anatambua maumivu ya kuondokewa na mtoto.

Wema amesema kuwa upendo wa Muna kwa mtoto wake ni mfano wa kuigwa na ndiyo maana kila mtu alimpenda Patrick.

"Pole sana Muna kwa msiba huu mzito, Patrick tulimpenda lakini Mungu kampenda zaidi, pia nikusihi haya ya mitandao uyaache kama yalivyo, yasilete nafasi ya kuleta mkanganyoko wa kifamilia, yaliyopita si ndwele tugange yajayo," amesema Wema.

Patrick atazikwa katika makaburi ya Kinondoni baada ya ibada ya kuaga kumalizika.