Nasa wahamasishana kususa bidhaa za kampuni sita

Muktasari:

Vifaa vyao, huduma na mapato ya masoko yao yanatumika kuwaunga mkono watu wenye damu katika mikono yao.

 

Nairobi, Kenya. Wabunge wa upinzani wamewataka wafuasi wao kususa kununua bidhaa na huduma zinazotolewa na makampuni ya Safaricom, Ilara, Brookside na Bidco kama sehemu ya harakati za kuikwamisha serikali.

Lengo la harakati hizo ni "kushusha makampuni hayo kiuchumi".

"Tutawapatia orodha ya makampuni yote kabla ya wakati kwa sababu kwani hakuna gharama kubwa ya kulipa kwa ajili ya nchi kurejea kwenye hali ya demokrasia,” alisema Mbunge wa Jimbo la Ugunja Opiyo Wandayi.

"Wakenya wamechoka na utamaduni wa wizi wa uchaguzi uliochimbiwa mizizi na utawala wa chama cha Jubilee."

Wanasiasa wengine chini ya kiongozi wa muungano wa National Super Alliance (Nasa) Raila Odinga waliweka msimamo huo jana walipozungumza na wanahabari.

Walisema wanataka ususiaji wa bidhaa kuenea haraka nchini kwa lengo la kuipinga serikali ya Jubilee.

Mwakilishi wa wanawake kutoka Homa Bay, Gladys Wanga alitoa wito kwa wafuasi wa Nasa kuhakikisha wamehama kutoka kampuni ya simu ya Safaricom ifikapo Ijumaa ijayo.

"Safaricom ina damu ya watu wetu waliouawa mbele yao. Walikuwa kizuzi cha demokrasia wakati wa uchaguzi,” alisema.

Watungasheria hao makampuni yanayotoa vifaa na huduma zilizotumika kuwanyima haki Wakenya matokeo yake yalikuwa vifo. "Vifaa vyao, huduma na mapato ya masoko yao yanatumika kuwaunga mkono watu wenye damu katika mikono yao,” alisema Wanga.

"Ushiriki wa Safaricom katika njama za kuzuia matakwa ya Wakenya wakati wa uchaguzi wa Kenya mwaka 2017 umefunikwa kwa kiasi kikubwa."

Raila alitishia kuitisha mgomo nchi nzima wa bidhaa kutoka mashirika ambayo anadai yalikuwa sehemu ya mpango wa kuruga uchaguzi wa Agosti 8.

Makampuni ya Safaricom, Al Ghurair yenye makao yake ambayo ilichapa makaratasi ya kupigia kura na OT-Morpho iliyosambaza vifaa vya utambuzi wa alama za vidole (KIEMS) yamekanusha madai hayo.

Kiongozi huyo wa upinzani alisema “hawataruhusu Kenya itumike kama uwanja wa mchezo kwa nguvu zinazotaka kukwamisha maendeleo ya nchi.

"Makampuni makubwa yenyewe ni sehemu ya kuua demokrasia nchini Kenya. Tuna nguvu ya umma na ikiwa wanataka kuzonga demokrasia, tunaweza kulipa kisasi,” alisema.