Nchimbi, Gulamali waibuka kidedea kura ya maoni

Muktasari:

John Nchimbi ametangazwa mshindi kwa kupata kura 219.

Wagombea 42 wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wamechuana katika kura ya maoni kuomba kuteuliwa kuwania ubunge wa Singida Kaskazini na Songea Mjini katika mikutano iliyofanyika leo.

Uchaguzi katika majimbo hayo unafanyika baada ya mbunge wa Songea Mjini, Leonidas Gama wa CCM kufariki dunia Novemba 24,2017; huku Singida Kaskazini aliyekuwa mbunge, Lazaro Nyalandu akijivua uanachama wa CCM na kujiunga na Chadema.

Katika mkutano wa uchaguzi Songea Mjini uliofanyika leo Desemba 10,2017 Msimamizi wa uchaguzi, Palolet Mgema amesema wagombea walikuwa 20 na wapiga kura walikuwa 605. Amemtangaza John Nchimbi kuwa mshindi kwa kupata kura 219.

John amewashinda wapinzani wake wa karibu ambao ni waziri wa zamani Dk Terezya Huvisa aliyepata kura 181 na  mwanasheria Dk Damas Ndumbaro aliyepata kura 83.

 

Jimbo la Singida Kaskazini, msimamizi wa uchaguzi Athuman Hamad amemtangaza Haider Hussein Gulamali kuwa mshindi baada ya kupata kura 606 kati ya kura 1,010 zilizopigwa sawa na ushindi wa asilimia 60.

Miongoni mwa wengine 21 waliomfuatia Gulamali ni Justine Monko aliyepata kura 133 na Juma Mgoo aliyekuwa mkurugenzi mkuu huduma za misitu amepata kura 46.