Ndugu waukataa mwili, wataka polisi itoe sababu za kifo

Kamanda wa Polisi mkoani Mara, Juma Ndani

Muktasari:

  • Ndugu wamesema hawatauchukua mwili na kwenda kuuzika hadi hapo polisi watakapowaambia sababu za Edward Mahende kupigwa risasi na aliyehusika ni nani na hatua zilizochukuliwa.

Serengeti. Siku moja baada ya Kamanda wa Polisi mkoani Mara, Juma Ndani kukiri askari wake kumuua Edward Mahende (73) mkazi wa kijiji cha Kenyana wilayani hapa, ndugu wamegoma kuuchukua mwili.

Msimamo wa ndugu unatokana na polisi kushindwa kutoa majibu ya maswali ya sababu za mauaji na aliyehusika na mauaji hayo.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Oktoba 15, 2018, Joseph Chacha ambaye ni mdogo wa marehemu amesema kaka yake ameuawa kwa makusudi kwani wanadai walikuwa na wenyeji ambao wanajua nyumba ya marehemu.

"Nimefika polisi wananiambia tuchukue mwili tukazike na wao watatoa jeneza na usafiri, maelezo ambayo yanatia shaka maana kama ni jambazi wanawezaje kumgharamia?" Amehoji.

Amesema wako tayari kukaa hata mwezi bila kuzika mpaka maswali yao yajibiwe.

Amesema mtoto anayedaiwa kuwa ni jambazi  ana umri wa miaka (16) na tukio lake alilofanya ni wizi wa ng'ombe mmoja akauza na mzazi hajawahi kulalamika polisi.

Mkuu wa wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu amesema atalizungumzia suala hilo baada ya uchunguzi wa mwili na kuomba wauchukue mwili wakauzike na mengine yatafuata.

Jana, Kamanda wa Polisi mkoa wa Mara, Juma Ndaki akizungumza na Mwananchi alisema tukio hilo lilitokea Oktoba 12, 2018 majira ya saa 8 usiku nyumbani kwa marehemu.

Alisema Mahende alitoka na mkuki kwa lengo la kumchoma askari polisi aliyebisha mlango na kujitambulisha ndipo polisi waliokuwa pembeni wakampiga risasi sehemu ya nyonga na kupoteza maisha.

Mwisho.