Nyalandu aachia ubunge, ajivua uanchama CCM

Muktasari:

Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu ametangaza kujitoa CCM na kujiuzulu nafasi zote ikiwamo ubunge

Dar es Salaam. Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu amejivua uanachama wa CCM na nyadhifa zake zote, akisema haridhishwi na mwenendo wa siasa nchini.

Nyalandu, ambaye alikuwa Waziri wa Maliasili na Utalii katika Serikali ya Awamu ya Nne, aliiambia Mwananchi  Jumatatu mchana kuwa ameamua kujiondoa CCM na ameiomba “Chadema wafungue malango yao” ili aweze kuungana nao.

"Nimeamua kujiuzulu nafasi yangu ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi CCM, pamoja na nafasi zote za Uongozi ndani ya Chama kuanzia leo, Oktoba 30, 2017," alisema Nyalandu ambaye video ya uamuzi huo imesambaa mitandaoni.

"Hali kadhalika, asubuhi ya leo nimemwandikia Spika wa Bunge, Mheshimiwa Job Ndugai barua ya kujiuzulu nafasi yangu ya ubunge wa Jimbo la Singida Kaskazini kupitia tiketi ya CCM, nafasi ambayo nimeitumikia kwa vipindi vinne mfululizo tangu nilipochaguliwa kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 2000 hadi Sasa.
"Aisha, nimechukua uamuzi huu kutokana na kutorishwa kwangu na mwenendo wa hali ya kisiasa nchini, ikiwa ni pamoja na ukiukwaji wa haki za binadamu, ongezeko la vitendo vya dhuluma wanavyofanyiwa baadhi ya Watanzania."

Kwa uamuzi huo, Nyalandu, ambaye aliomba ridhaa ya kugombea urais kwa tiketi ya CCM katika uchaguzi uliopita, amejivua ubunge na nafasi nyingine zote alizokuwa akishikilia ndani ya CCM, ikiwa ni pamoja na ujumbe wa Halmashauri Kuu.