Nyalandu ajitoa CCM, Chadema wamkaribisha

Muktasari:

  • Nyalandu alisema amemwandikia barua Spika wa Bunge, Job Ndugai, barua ya kujiuzulu rasmi ubunge wa jimbo la Singida Kaskazini nafasi ambayo nimeitumika kwa vipindi vinne mfululizo tangu mwaka 2000.

Dar es Salaam. Aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), Lazaro Nyalandu jana ametangaza kujivua ubunge pamoja na nafasi zake zote ndani ya chama hicho na kuomba kujiunga na Chadema.

Nyalandu alisema amemwandikia barua Spika wa Bunge, Job Ndugai, barua ya kujiuzulu rasmi ubunge wa jimbo la Singida Kaskazini nafasi ambayo nimeitumika kwa vipindi vinne mfululizo tangu mwaka 2000.

Akizungumza jana Nyalandu amesema sababu ya kuchukua uamuzi huo ni kutokulidhishwa na mwenendo wa hali ya kisiasa nchini ikiwa ni pamoja na ukiukwaji wa haki za kibinadamu, ongezeko la vitendo vya dhuluma wanavyofanyiwa Watanzania na kutokuwepo kwa mipaka ya wazi ya mihimili ya dola yaani Serikali, Bunge na Mahakama.

“Nimeamua kujiuzulu nafasi yangu ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), pamoja na nafasi zote za uongozi ndani ya chama kuanzia leo(jana), Oktoba 30, 2017.

Nyalandu ambaye hivi karibuni ameonekana kutofautiana na chama chake, ndiye mbunge wa CCM aliyekwenda Nairobi nchini Kenya kumjulia hali mbunge mwenzake wa Singida Mashariki, Tundu Lissu aliyejeruhiwa kwa risasi akiwa mjini Dodoma Septemba 7 mwaka huu.

“Nimechukua uamuzi huo kutokana na kutokuridhishwa kwangu na mwenendo wa hali ya kisiasa nchini ikiwa ni pamoja na ukiukwaji wa haki za kibinadamu, ongezeko la vitendo vya dhuluma wanavyofanyiwa Watanzania wenzangu na kutokuwepo kwa mipaka ya wazi ya mihimili ya dola yaani Serikali, Bunge na Mahakama,” alisema Nyalandu.

Mbali na kuonyesha kutoridhishwa na matukio ya usalama nchini, Nyalandu pia alitangaza hivi karibuni kupitia ukurasa wake wa Twitter azma yake ya kupeleka hoja binafsi bungeni ya kutaka mabadiliko ya Katiba, jambo ambalo pia amelitaja kama sababu ya kuondoka CCM.

“Mimi naondoka na kukiacha Chama cha Mapinduzi nikiwa nimekitumia nikiwa nimekitumikia kuanzia ngazi ya uenyekiti UVCCM ngazi ya mkoa, mjumbe wa kamati za siasa za wilaya, mkoa, mjumbe wa kamati za mkoa na mwisho kabisa nikiwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa.

“Kwani nimejiridhisha kuwa kwa mwenendo wa hali ya siasa kiongozi wa kisiasa na kiuchumi, CCM imepoteza mwelekeo wake wa kuisimamia Serikali kama ilivyokuwa hapo awali,” alisema Nyalandu.

Nyalandu alisema kama ilivyo kwa mihimili ya Bunge na Mahakama kutokuwa na uhuru kamili, bila kuingiliwa kiutendaji kwa namna moja au nyigine, CCM nayo imekuwa chini ya miguu ya dola kwa kushindwa kushika hatamu na kuikosoa Serikali kama yalivyo maelekezo ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.

“Hivyo basi kwa dhamira yangu na uamuzi wangu mwenyewe, nikiwa haki ya kikatiba, natangaza rasmi kukitangaza rasmi kukihama CCM siku ya leo(jana),” alisema.

“Nakiomba ikiwapendeza Chadema, basi waniruhusu kuingia malangoni mwao niwe mwanachama, ili kuungana na Watanzania wote wanaopenda kuleta mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi nchini kwa kupitia mfumo wa kidemokrasia na uhuru wa mawazo,” alisisitiza Nyalandu.

Nyalandu alisema kwa kujiuzulu kwake ubunge jimbo la Singida Kaskazini, kunaruhusu kufanyika kwa uchaguzi mwingine ili wananchi wapate fursa ya kuchagua itikadi wanayoona inawafaa kwa majira na nyakati hizi zenye changamoto lukuki nchini Tanzania.

“Ni imani yangu kamwe hayatakuwa ya bure maneno haya, wala uamuzi huu niufanyao mbele ya Watanzania leo(jana) ili kwamba, sote kama Taifa tuingie kwenye mjadala wa kuijenga upya misingi ya nchi yetu,” alisema na kuongeza:

“Ni maombi yangu kwa Mungu kuwa haki itatamalaki Tanzania. Upendo, amani na mshikamano wa watu wa imani zote za dini, mitazamo yote ya kiitikadi za kisiasa na makabila yote nchini uimarike. Tushindane kisera na kuruhusu tofauti za mawazo, lakini tubaki kama ndugu na Taifa lililo imara na nchi yenye adili.”