Ofisa elimu atoweka katika mazingira yenye utata

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah

Muktasari:

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah amesema taarifa za kutoweka kwa mtumishi huyo hazijafika ofisini kwake.

Mwanga. Kwa zaidi ya wiki sasa, familia ya ofisa elimu Wilaya ya Mwanga, Yasini Komeja ipo katika majonzi kutokana na kutoweka kwake katika mazingira ya kutatanisha.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah amesema taarifa za kutoweka kwa mtumishi huyo hazijafika ofisini kwake.

Nyumbani kwa Komeja, Mtaa wa Vudoi, Kata ya Mwanga, mkewe Amina Mkwizu aliiambia Mwananchi kuwa Juni 10, mumewe aliaga kwenda kazini lakini hadi jioni hakurudi.

Alisema awali, mumewe alimweleza kuwa angesafiri na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri wilaya hiyo kwenda Dodoma.

Hata hivyo, mkurugenzi mtendaji huyo, Golden Mgonzo alisema mtumishi huyo alipotea kabla hajapata taarifa ya kwenda Dodoma.

“Niko Dodoma kwenye kikao tangu (juzi) jana, sijui kama alikuwa na safari ya kwenda Dodoma, isitoshe yeye alipotea kabla hata sijapata taarifa ya safari,” alisema.

Amina alisema Juni 11 wafanyakazi wenzake na Komeja walikwenda nyumbani kwake baada ya kukuta vitu vyake ofisini, ikiwamo simu, shati, begi na miwani ili kufahamu ilikuwaje vimeachwa ofisini.

“Kwa kuwa aliniambia atasafiri na mkurugenzi ilipofika usiku sikuingiwa na wasiwasi. Nilijua wameunganisha safari lakini ilipofika Jumatano nililetewa taarifa kuwa wamekuta vitu vya mume wangu juu ya meza na hadi leo hajaonekana,” alisema Amina huku akitokwa machozi.

Alisema pamoja na ndugu zake wamezunguka kila mahali kumtafuta lakini hajapatikana.

Ameviomba vyombo vya ulinzi na usalama nchini kuhakikisha mumewe anapatikana akiwa salama.

“Ninaiomba Serikali ihakikishe mume wangu anarudi akiwa hai, kwani alipotea akiwa katika majukumu yake ya kazi na bado familia tunamtegemea na watoto bado wanasoma,” alisema.

Mkuu wa idara ya utumishi na utawala Halmashauri ya Mwanga, Joshua Samweli alisema Juni 11, alipokea taarifa ya mtumishi huyo kupotea katika mazingira ya kutatanisha.

Alisema walifanya mawasiliano na mkewe kutaka kujua aliondoka nyumbani saa ngapi, ndipo alipowaeleza alikuwa na ratiba ya kwenda na mkurugenzi jijini Dodoma lakini baada ya kufuatilia mkurugenzi hakuwa na ratiba ya kwenda huko.

“Baada ya mazungumzo ya simu tulikwenda nyumbani kwake ili kujua kama kuna ugomvi au tukio jingine lakini kwa bahati mbaya yule mama alikuwa analia sana. Tulikwenda kituo cha Polisi Kifaru kutoa taarifa na tunaendelea kumtafuta,” alisema.

Ofisa elimu msingi wilayani Mwanga, Allan Said alisema Komeja katika utendaji wake alikuwa mtu wa kusimamia haki.

Alisema miezi mitatu iliyopita alipongezwa kwa kuwa mtumishi mwadilifu.