Penzi la Diamond, Zari layumba

Muktasari:

  • Uhusiano ulianza kuyumba kwa kipindi cha miezi miwili baada ya Diamond kukiri kuzaa na mwanamitindo Hamisa Mobetto

Dar es Salaam.Ule uhusiano maarufu zaidi Afrika Mashariki wa Diamond Platnumz na Zarina Hassan inaelekea upo katika hatua mbaya ya uhai wake kutokana na yanayoendelea katika mitandao ya kijamii.

Katika kipindi cha miezi miwili uhusiano huo umepamba vichwa vya habari kabla na baada ya Diamond kukiri kuzaa na mwanamitindo Hamisa Mobetto.

Hata hivyo, baada ya sekeseke hilo kupita ilionekana huenda hali imekuwa shwari hasa baada ya Diamond kuhudhuria sherehe ya kuzaliwa Zari, Septemba 23 mwaka huu nchini Afrika Kusini.

Inavyoonekana moto unafukuta ndani kwa ndani kwani tangu juzi wapendanao hao wamekuwa wakifuta picha zao za pamoja katika akaunti zao za Instagram.

Pamoja na kufuta picha, Zari anaonekana kurusha vijembe katika mtandao wa Snapchat akisema hawezi kufanywa mjinga katika mitandao ya kijamii.

Katika kuadhimisha siku ya kuzaliwa Diamond, mashabiki walisubiri kwa hamu kuona atakachoandika Zari kama ilivyo kawaida yake lakini ilipita kimya.

Wengi wametafsiri kuwa pamoja na Diamond kusafiri mpaka Afrika Kusini kutafuta suluhu, mwanamke huyo bado ana kinyongo.