RC Mtwara asainisha mikataba na Ma DC

Muktasari:

Ni ili kuhakikisha udumavu katika mkoa huo unapungua

 

Mtwara. Katika kuhakikisha mkoa wa Mtwara unaondokana na tatizo la udumavu, mkuu wa mkoa huo, Gelasius Byakanwa amesaini mikataba ya utekelezaji wa afya za lishe na wakuu wa wilaya pamoja na makatibu tawala.

Kwa sasa mkoa wa Mtwara unatajwa kuwa na asilimia 38 ya watoto walio chini ya miaka mitano kukabiliwa na udumavu. huku asilimia 58.6 ya walio na umri chini ya miaka mitano wakikabiliwa na upungufu wa damu.

“Suala ni kuona utekelezaji wa huo mkataba lakini huduma za lishe zinafanyikaje katika wilaya, wakurugenzi na wakuu wa wilaya panueni wigo kadri ambavyo mtaona mnarahisisha kutekeleza mkataba wenyewe.”

“Kama tutawatumia vizuri viongozi wetu wa dini kwenye maeneo yetu na wao wakawa wasemaji na watoaji wa elimu ya masuala ya lishe katika nyumba zao za kuhubiria naamini tutawafikia wananchi wengi kwa wakati mmoja kwani wanakutana na waumini wao mara nyingi,” amesema Byakanwa.

Akizungumzia hali hiyo, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu, Dk Furaha Mwakafwila amesema tatizo la wanawake kujifungulia nyumbani na njiani ni moja ya changamoto inayosababisha kuongezeka kiwango cha udumavu kwa watoto kutokana na wazazi kukosa elimu ya lishe pindi wanapohudhuria katika vituo vya afya mbali na kujifungua. 

“Kiwango cha mama wajawazito kujifungulia kituoni bado kipo chini ya asilimia 65 ambayo ndiyo kiwango ambacho walau kinakubalika kitaifa.”

“Kutokana na changamoto hiyo tumeweka mikakati ikiwamo kufanya uhamasishaji kwa viongozi ngazi ya wilaya, madiwani, ngazi ya kata na vijiji na kisha ngazi ya jamii ili kuona tatizo na waliyotueleza ndiyo tunayoyafanyia kazi,”amesema Dk Mwakafwila.

Amesema kati ya mwaka 2013 hadi 2016 jumla ya wakina mama 185 walijifungulia nyumbani na njiani, huku 180 walijifungulia katika vituo lakini kwa sasa hali hiyo imeanza kupungua

Ofisa lishe wa mkoa, Harriet Joseph ameishauri jamii kuondokana na imani potufu za kwenye jamii na kufuata elimu na ushauri wanaopatiwa katika vituo vya afya.

“Wakina mama wengine wana amini wakienda katika vituo vya afya watapasuliwa kama mtoto akiwa mkubwa,” alisema.

Alisema halmashauri wamezielekeza zifuatilie kwenye vituo vya afya kuhakikisha huduma zinatolewa lakini pia mama aelekezwe matumizi sahihi na faida sahihi ambayo anaweza akapata anapotumia dawa za kuongeza damu.