RIPOTI MAALUMU: Uhalifu wa wanafunzi wa sekondari Dar

Muktasari:

Wengi tumezoea kuona ama kusikia matukio makubwa ya uhalifu yakifanywa na vijana wanaoishi katika mazingira magumu na waliokosa fursa ya kuwa shuleni au kukosa ajira.

Lakini mambo yamebadilika. Uchunguzi wa Mwananchi katika shule tano za sekondari jijini Dar es Salaam ukihusisha kushinda na wanafunzi, kuongea na walimu na Jeshi la Polisi unaonyesha kuwa wanafunzi wa shule hizo wamejiingiza katika uhalifu ikiwamo uporaji, uuzaji dawa za kulevya, kubaka na kulawiti wenzao. Yote hayo yapo katika simulizi ya mwandishi wetu aliyefuatilia shule hizo na kuzungumza na wanafunzi, walimu na Jeshi la Polisi.

Dar es Salaam. Pengine ni moja ya sababu zinazochangia baadhi ya wanafunzi wa shule za sekondari za Serikali, hasa zile za kata kufanya vibaya katika mitihani ya kitaifa.

Lakini, hata kama haichangii, tabia za baadhi ya wanafunzi kushiriki katika vitendo vya kihalifu zimekithiri katika shule za wilayani Ilala.

Baadhi ya wanafunzi hao wanapora, kunywa gongo, kutembea na silaha za jadi wanazotumia kutishia au kujeruhi wakati wa kupora, kutumia dawa za kulevya na uovu mwingine, Mwananchi limebaini.

Uchunguzi wetu pia umebaini kuwa wanafunzi wa shule hizo wamefikia hatua ya kutembea na silaha kama vile mapanga, bisibisi, visu, sindano za silinji wanazotumia kutekeleza uhalifu huo. Zaidi ya yote wanacheza kamari na hata kushirikiana na makundi makubwa ya kihalifu nje ya shule.

Uhalifu huo na utovu wa nidhamu uliopitiliza unaelezewa kuwa unachangia wanafunzi wengi kutofanya vizuri katika masomo, hususan wale walioko shule za Serikali.

Uchunguzi wa Mwananchi ulilenga shule tano za sekondari katika Jimbo la Ukonga; Kinyamwezi, Nyeburu, Chanika, Furaha na Charambe. Shule hizi pia zimo kwenye orodha ya shule zinazofanya vibaya katika mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne.

Alichoshuhudia mwandishi

Katika maisha ya kutwa ya vichochoroni, Mwananchi ilifika kushuhudia, licha ya kuvaa sare baadhi ya wanafunzi hao huvuta bangi, sigara na kula ugoro. Wapo pia wanaotembea na viwembe, sindano zikiwa katika silinji na bisibisi ambazo huzihifadhi katika mabegi yao ya shule.

Katika kituo cha mabasi cha Kinyamwezi kilichopo takriban kilomita moja kutoka Sekondari ya Kinyamwezi, mwandishi alishuhudia mara kadhaa baadhi ya wanafunzi wakifanya vurugu kubwa ndani ya daladala na usumbufu kwa abiria wengine. Katika shule za Nyeburu na Kinyamwezi wapo baadhi ya wanafunzi wanaotumia muda wa masomo kucheza kamari vichochoroni.

Wanafunzi waliokubali kuongea na Mwananchi wanathibitisha baadhi ya wenzao kufanya matukio ya kihalifu ndani na nje ya shule.

“Kinyamwezi kuna shida, shule imejaa wahuni wengi,” anasema mwanafunzi mmoja wa Shule ya Kinyamwezi katika kituo cha Kinyamwezi baada ya kutokea vurugu.

“Sisi tunaosoma shule hiyo tunaijua vizuri. Wanafunzi wengi wanaokuja shule hii wanaishia kuharibikiwa kitabia. Wanafunzi wenyewe tu wamepinda (wameharibika kitabia). “Wanafunzi, wanavuta bangi, wanakunywa pombe. Leo tu kuna wawili wamekamatwa na wananchi wakiwa wanakunywa gongo, wakaletwa shuleni wamelewa chakali.”

Mwanafunzi mwingine aliyekubali kuzungumza na Mwananchi, akiwa na wenzake, pia alithibitisha kuwepo kwa ukorofi na uhalifu shuleni kwao.

Mwanafunzi wa kwanza: “Kusema kweli baadhi ya wanafunzi si wema. Wanashirikiana na wahalifu mtaani kupora wanafunzi mabegi na kukaba raia mtaani.

Baadhi wavutaji bangi, sigara na kunywa gongo na wengine wanafanya ukahaba. Mfano, tukipanda daladala tukiwa tunakwenda nyumbani au kwenye michezo baadhi ya wanafunzi wa kike na kiume wanalazimishana kupakatana. Ukikataa wanatishia kukuchoma kwa kiwembe au bisibisi

Mwanafunzi wa pili: Wanafunzi hasa wa kidato cha pili, tatu na nne wanatembea na visu, bisibisi, sindano na nyembe na ndiyo wanaoongoza kwa uhalifu. Mnapokuwa kwenye daladala wanawatafuta wanafunzi wale wapole na wanyonge halafu wanawalazimisha kuwapakata.

Mwanafunzi wa tatu: Kwenye daladala wanatukana matusi, wanalazimisha kutupakata. Ukikataa wanakukaba, na hii inafanywa hata na wanawake wanawalazimisha wavulana wapakatane wakikataa wanawakalia kwa nguvu.

Wakikupakata wanalazimisha kushikwa sehemu zao za siri.

Wanafunzi wa Charambe, hasa wa kidato cha kwanza, walieleza kuwa huwa wananyang’anywa vifaa na wanafunzi wa madarasa ya juu na namna wanavyovuta bangi vichochoroni.

“Muda ambao wenzao wako darasani wao wanakaa vichochoroni wanavizia mwanafunzi wa kidato cha kwanza ambaye ni mpole na kumkamata kwa nguvu na kumpekua,” anasema mmoja wa wanafunzi hao aliyejitambulisha kwa jina la Athuman.

“Wakimkuta na pesa wanamnyang’anya.”

Mwanafunzi mwingine wa shule hiyo aliyeomba jina lake lihifadhiwe, alisema wanafunzi hao wahalifu huuza mabegi wanayopora wenzao.

Utovu wa nidhamu

Alipoulizwa kuhusu hali ya nidhamu, mkuu wa Shule ya Sekondari Furaha, Simon Chumila alisema lipo na kuna tatizo la utovu wa nidhamu uliokithiri.

Alisema kwa kipindi cha miezi sita tangu Aprili, amepokea kesi 16 za utovu wa nidamu, kati ya hizo kesi nne ni za wanafunzi kukamatwa wakivuta bangi, nne za wanafunzi kupiga wenzao na kuwajeruhi na wanafunzi sita wakiripotiwa kwa kosa la kupora ndani na nje ya shule.

“Kesi ya mwisho ya mwanafunzi kupora imefika leo ofisini kwangu, mwanafunzi (anamtaja jina) wa kidato cha kwanza anadaiwa kupora begi la mwanafunzi mwenzake na kutoweka kwa zaidi ya miezi miwili.

Amerudi leo akiwa na mzazi wake,”alisema Chumila.

Anasema katika kipindi hicho cha miezi sita wamepokea pia ripoti ya wanafunzi watatu kukamatwa wakivuta bangi, wengine wanne kwa kosa la kupiga huku mwingine akikamatwa kwa kosa la kuuza bangi shuleni.

“Ninaposema wanafunzi wangu wana utovu wa nidhamu ninamaanisha. Hapa shuleni tuna majalada (files) ya wanafunzi na makosa waliyofanya,” alisema huku akifungua moja ya mafaili.

Katika faili moja alisema barua kuomba msamaha kwa kosa la kukutwa akivuta bangi, kukutwa na ganda la kiberiti, karatasi za kusokotea bangi, karata za kuchezea kamari na kondomu mbili mfukoni.

“Mafaili yanajaa na tunanunua mengine. Wanafunzi wangu hawa unaowaona, wanatembea na visu, mapanga, bisibisi. Wanaficha kwenye mabegi yao, na wengine wanaweka mifukoni.

”Kuna mwanafunzi hapa shuleni aliwahi kukatwa panga na mwanafunzi mwenzake usoni akiwa darasani. Hii inaonyesha ni namna gani wanafunzi hawa ni hatari.”

Inaendelea kesho