Rais Magufuli atoa agizo mjadala wa muda wa urais

RAIS MAGUFULI AZIMA MJADALA WA KUONGEZA MUDA WA URAIS

Muktasari:

Rais amekutana na kufanya mazungumzo na Polepole na kumueleza kuhusu suala hilo.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amemuelekeza Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Hamphrey Polepole amemuelekeza kuwajulisha wanachama wa CCM na umma wa Watanzania kuwa anasikitishwa na hafurahishwi na mjadala unaoendelea juu kuongezwa kwa kipindi cha Urais kutoka miaka 5 iliyowekwa kwa mujibu wa katiba, hadi miaka 7.

Taarifa iliyotolewa leo Jumamosi Januari 13 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa imeeleza kuwa Rais amekutana na kufanya mazungumzo na Polepole na kumueleza kuhusu suala hilo.

Katika taarifa hiyo Polepole amesema Rais Magufuli amewataka wanachama wa CCM na umma wa Watanzania kwa ujumla kuupuuza mjadala huo kwa kuwa haujawahi kujadiliwa katika kikao chochote cha chama na ni kinyume na katiba ya CCM na Katiba ya nchi.

Ameongeza kuwa Rais Magufuli amewataka wana CCM na umma wa Watanzania kutokubali kuyumbishwa ama kupotoshwa na mambo yasiyokuwa ya msingi na badala yake wajielekeze katika ajenda muhimu ya kujenga uchumi na kutekeleza Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Polepole amebainisha kuwa Rais Magufuli hana mpango wowote na hatarajii kuongeza kipindi cha urais wakati wote wa uongozi wake.