Sampuli ya mkojo wa Manji yaibua maswali kortini

Mfanyabiashara maarufu, Yusufali Manji akiwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam jana. Picha na Omar Fungo

Muktasari:

  • Licha ya vilivyobainika katika sampuli hiyo, wakili Hudson Ndusyepo anayemwakilisha Manji, amemhoji shahidi wa tatu wa upande wa mashtaka iwapo ana uhakika kuwa mkojo huo ni wa mteja wake au wa askari aliyesimamia utoaji wa sampuli hiyo.

Dar es Salaam. Sampuli ya mkojo iliyochukuliwa kwa ajili ya uchunguzi kutoka kwa mfanyabiashara Yusufali Manji, imeendelea kuibua maswali mahakamani.

Licha ya vilivyobainika katika sampuli hiyo, wakili Hudson Ndusyepo anayemwakilisha Manji, amemhoji shahidi wa tatu wa upande wa mashtaka iwapo ana uhakika kuwa mkojo huo ni wa mteja wake au wa askari aliyesimamia utoaji wa sampuli hiyo.

Mkemia Domician Dominic, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa dawa aina ya benzodiazepines iliyokutwa kwenye sampuli ya mkojo wa Manji inatumika hospitalini kutuliza maumivu makali au kumpatia mtu usingizi.

Dominic kutoka ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, akiwa shahidi wa tatu wa upande wa mashtaka alieleza hayo jana mbele ya Hakimu Cyprian Mkeha alipotoa ushahidi katika kesi inayomkabili Manji.

Manji anadaiwa kutumia dawa za kulevya aina ya heroini kati ya Februari 6 na 9 mwaka huu katika eneo la Sea View, Upanga wilayani Ilala.Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Timon Vitalis kutoa ushahidi, Dominic alidai uchunguzi wa awali aliofanya kwenye sampuli ya mkojo wa Manji alikuta una dawa aina ya benzodiazepines.

Anadai uwepo wa dawa hiyo kwenye sampuli ya mkojo ulimpa picha kuwa mtu huyo aliitumia kutuliza maumivu makali au kukosa usingizi. Hata hivyo, alisema ina matumizi mengi kulingana na maelekezo ya daktari. Shahidi huyo alibainisha kuwa, kwa uzoefu alionao na utafiti alioufanya nchini, mara nyingi mtu anayetumia benzodiazepines pia hutumia heroini au kokeini.

Dominic alidai katika hatua ya pili ya uchunguzi wa sampuli hiyo ya mkojo kwa kutumia mashine ya HPLS, ulionyesha una dawa aina ya morphine ambayo ni metabolites (metaboli) ya heroini. Shahidi huyo alidai ni vigumu kupata heroini kwenye mkojo kwa sababu inapokuwa mwilini ndani ya dakika 20 au 60 hubadilika na kuwa morphine, dawa aliyosema pia hutumika hospitalini.

Baada ya wakili Vitalis kumwonyesha shahidi huyo ripoti hiyo ya uchunguzi, aliitambua akisema ina mihuri miwili ya ofisi, saini yake na mtiririko wa kazi aliyoifanya.

Mahakama iliipokea ripoti hiyo kama kielelezo baada ya upande wa utetezi kutokuwa na pingamizi. Baada ya kumaliza ushahidi huo, wakili Hudson Ndusyepo anayemwakilisha Manji alimuuliza maswali shahidi huyo kama ifuatavyo:-

Wakili: Kabla mtu hajafikishwa kwenu, ni utaratibu gani uliopo?

Shahidi: Ile ni maabara, kuna fomu maalumu zinatakiwa kujazwa na kwa sampuli za jinai, Jeshi la Polisi linapaswa kufanya hivyo.

Wakili: Fomu hiyo inatakiwa kuambatana na barua?

Shahidi: Fomu hiyo ni lazima ijazwe kwa mujibu wa sheria, pia inatakiwa kuwa na barua. Maombi ya Manji yalipokuja kwangu yalikuja na fomu pekee.

Wakili: Wewe unajipangia kazi au unapangiwa na Mkemia Mkuu wa Serikali?

Shahidi: Amekasimu madaraka kwangu ili niweze kufanya kazi.

Wakili: Manji na Askofu Gwajima waliletwa kwako jioni?

Shahidi: Manji na Gwajima waliletwa saa 5:15 asubuhi.

Wakili: Kuna barua kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwenda kwa mawakili ya Aprili 12, 2017 umeona mtu aliyeisaini?

Shahidi: Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Manyele.

Wakili: Inawezekana kweli kama ulikasimishwa madaraka na Mkemia Mkuu wa Serikali, halafu asijue kama Yusufali Manji alifika pale na kufanyiwa uchunguzi wa mkojo?

Shahidi: Alifika na nikamfanyia uchunguzi.

Wakili: Katika uchunguzi wa sampuli ya mkojo wa Manji ulipata dawa ya benzodiazepines ambazo hutolewa na madaktari kwa wagonjwa?

Shahidi: Ni kweli zinatolewa na madaktari au kununua duka la dawa kwa kuwa zinatumika kutuliza maumivu na hazijakatazwa.

Wakili: Pia, ulisema zinaweza kutumika kumpatia mtu usingizi na zinatolewa na daktari?

Shahidi: Ni kweli zinaweza.

Wakili: Unaweza kujua kuna dawa tofauti mtu anaweza kuzitumia zikasababisha katika uchunguzi wenu kuonekana anatumia heroini?

Shahidi: Morphine ambayo ni metabolites ya heroini inaweza kukutwa kwenye baadhi ya dawa za kupunguza maumivu.

Wakili: Umesema wakati wa kuchukua sampuli ya Manji wewe ulikuwapo?

Shahidi: Niliwaandalia mazingira na kumkabidhi kikontena kidogo askari Sospeter wakati wa uchukuaji wa sampuli ya mkojo. Nilikuwa nje nasubiri, Manji na askari huyo waliingia chooni ili atoe sampuli na akatoa.

Wakili: Wewe una uwezo wa kusema huo mkojo ni wa Yusufali Manji au ni wa askari?

Shahidi: Sina uhakika na hiyo sampuli ya mkojo niliyoletewa ambayo niliipa namba ya usajili wa maabara 367/2017 kama ni wa Manji au ni wa askari.

Wakili Vitalis alifunga ushahidi wa upande wa mashtaka. Hakimu Mkeha alisema kesho atatoa uamuzi iwapo mshtakiwa ana kesi ya kujibu. Manji aliyekana shtaka la kutumia dawa za kulevya yupo nje kwa dhamana baada ya kukamilisha masharti ya kuwa na mdhamini mmoja aliyesaini bondi ya Sh10 milioni.