Serikali yavunja ukimya suala la Lissu

Muktasari:

  • Lakini wakati Serikali ikisema hayo na uongozi wa Chadema ukieleza kwamba utalizungumzia suala hilo leo, Mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), Lazaro Nyalandu ambaye amekuwa akifanya mipango ili Lissu apelekwe kutibiwa ng’ambo, amesema madaktari wa Nairobi alikolazwa wamesema hawezi kusafirishwa katika kipindi hiki.

Tanga/Dar. Baada ya kushutumiwa kwamba imekaa kimya katika suala la matibabu ya Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, Serikali imejitokeza na kueleza kwamba iko tayari kugharamia tiba yake popote pale ikiwa itaombwa na familia au kwa ushauri wa madaktari.

Lakini wakati Serikali ikisema hayo na uongozi wa Chadema ukieleza kwamba utalizungumzia suala hilo leo, Mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), Lazaro Nyalandu ambaye amekuwa akifanya mipango ili Lissu apelekwe kutibiwa ng’ambo, amesema madaktari wa Nairobi alikolazwa wamesema hawezi kusafirishwa katika kipindi hiki.

Jana akiwa Tanga, Waziri wa Afya, Ummy Mwaimu aliitisha mkutano na wanahabari na kusisitiza kuwa Serikali haijashindwa kuchangia gharama za matibabu ya Lissu huku akisema tangu mwanzo wa tukio la kushambuliwa kwake kwa risasi Septemba 7 huko Dodoma, viongozi wamekuwa wakishirikiana na familia katika kunusuru maisha yake.

Alisema amesikitishwa na namna ya suala la matibabu ya Rais huyo wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), linavyochukuliwa kisiasa huku akitahadharisha kwamba michango inayoendelea kuhamasishwa kusaidia kumtibu inaweza kutumiwa na matapeli kuwaibia wanaochanga.

“Serikali ina mpango wake katika kushughulikia matukio kama hayo, njia hiyo ndiyo iliyofanyika awali baada ya mbunge huyo kushambuliwa. Alifikishwa hospitalini na baadaye kukawepo na mpango wa kumpeleka Muhimbili,” alisema Ummy.

Baada ya shambulio hilo, Lissu alipelekwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kwa matibabu ya awali kabla ya kusafirishwa kwa ndege ya kukodi hadi Nairobi, Kenya anakoendelea na matibabu.

Kabla ya kupelekwa Nairobi, Serikali kupitia Bunge ilieleza kwamba kwa utaratibu wake, mgonjwa anapopata rufaa hupelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili na ikishindikana anahamishiwa Apollo, India na si kinyume cha hapo. Utaratibu huo ulipingwa na viongozi wa Chadema ambao wakiongozwa na mwenyekiti wake, Freeman Mbowe waliamua kumpeleka Nairobi kwa walichoeleza kuwa ni kwa usalama wa mgonjwa.

Tangu alipopelekwa huko, Chadema imekuwa ikisema kwamba Serikali haijachangia chochote katika matibabu hayo ambayo tayari kiasi cha Sh160 milioni kimeshatumika ambazo zimetoka katika chama hicho na michango ya wananchi.

Lakini jana, Waziri Ummy alisema Serikali inasubiri familia iseme nini inataka kifanyike na wapi inataka mgonjwa wao akatibiwe na kwamba itakuwa nayo bega kwa bega kuhakikisha anatibiwa popote duniani na kwa gharama yoyote ile na si kwa michango ya wasamaria wema.

Alisema lengo la Serikali ni kuondoa dhana kwamba imejitenga katika matibabu ya Lissu hadi jukumu hilo kuonekana kuwa limebebwa na jamii na jambo linaloweza kuleta taswira mbaya ndani na nje ya nchi kutokana na ukweli kuwa aliyehusika ni kiongozi na Mtanzania.

Pamoja na hayo, aliwashukuru watu wote walioshiriki kwa njia moja au nyingine wakiwamo madaktari na wahudumu wa Hospitali ya Dodoma kutoa huduma kwa Lissu.

Baadaye jana jioni, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Chadema, Tumaini Makene alisema walikuwa wakitafakari kauli hiyo ya Serikali na kwamba leo Mbowe atazungumza na vyombo vya habari.

Hawezi kutibiwa nje

Awali jana, Nyalandu aliandika katika mitandao kwamba madaktari wa Kenya wamesema Lissu hawezi kusafirishwa kwenda nje kwa ajili ya kupatiwa matibabu kwa sasa.

Nyalandu ambaye alifanikisha matibabu ya watoto watatu wa Shule ya Lucky Vincent ya Arusha huko Marekani baada ya kunusurika katika ajali iliyoua wenzao 32, walimu wawili na dereva, aliandika katika kurasa zake za Instagram, Facebook na Twitter kwamba mipango hiyo itasimama kwa sasa hadi atakapokamilishiwa huduma za tiba ambazo tayari ameanzishiwa.

“Tunafahamu kwamba, tangu Alhamisi, Septemba 7, siku ambayo Mh Tundu Lissu alishambuliwa kwa kupigwa risasi mjini Dodoma, Watanzania wengi wamesononeshwa na kulia sana, na kubwa zaidi, wote wameungana katika kuomba sala na dua ili mkono wa mkombozi, aliye Mungu wetu, upate kumgusa tena na kumponya dhidi ya majeraha, maumivu na mateso anayoyapitia.

“Mapema leo (jana), baada ya kutembelea Nairobi Hospital asubuhi, nimefanya mazungumzo mchana wa leo na Mh Freeman Mbowe, ambapo kwa pamoja tumeelezwa kuwa madaktari wameendelea na kumtibu ikiwa ni pamoja na kuanza upasuaji, na huduma zingine za kitabibu walizomwanzishia tangu awasili Nairobi. Imeelezwa vilevile kuwa kwa sasa ataendelea na tiba hospitalini hapo kutokana na kile kilichoelezwa kuwa hali yake bado ni “Critical but stable” na kwamba mwili wake unaendelea kuitikia vyema matibabu lukuki anayofanyiwa kwa wakati mmoja.

“Kwa sasa, mipango ya kumsafirisha nje itasimama, kutokana na ushauri wa madaktari ili kuruhusu kukamilishiwa huduma za tiba ambazo tayari ameanzishiwa, hadi hapo itakavyoshauriwa vinginevyo, ama endapo kutatokea umuhimu wa kufanya hivyo katika siku zijazo. Aidha, sote tuzidi kumwombea Mungu na kushiriki katika changizo za kusaidia gharama za matibabu yake.

“Ni dhahiri kwamba Wana Singida na Watanzania wote tumeumia, tumekwazwa na tumesononeshwa sana kwa uonevu na dhuluma aliyotendewa ndugu yetu Mh Tundu Lissu.

Wanasheria Uingereza wamwandikia Rais barua

Taasisi tatu za juu za wanasheria za Uingereza zimeungana na kumwandikia barua ya wazi Rais John Magufuli zikiomba mamlaka kufanya uchunguzi wa kina juu ya tukio la kupigwa risasi kwa Lissu na kumfutia kesi zote zinazomkabili ambazo zimekosa ushahidi wa kutosha.

Barua hiyo imeandikwa juzi na kusainiwa na vigogo wa Chama cha Mawakili Uingereza (LS), Kamati ya Haki za Binadamu ya Wanasheria Uingereza (BHRC) na Baraza la Wanasheria (BC).

Vigogo hao, Rais wa LS, Joe Egan; Mwenyekiti wa BHRC Andrew Langdon na Mwenyekiti wa BC, Kirsty Brimelow wamesema wanaguswa na matukio yanayoendelea dhidi ya Lissu ikiwamo ya matukio ya kukamatwa na polisi na kufunguliwa mashtaka mara kwa mara huku pia ikiorodhesha matukio mengine ya kihalifu yaliyowakumba wanasheria wengine likiwamo la kulipuliwa ofisi ya kampuni ya uwakili ya Immma ya jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

Pia, wamesema wameguswa na vitisho dhidi ya TLS kikiwemo cha kukifuta chama hicho kilichotolewa na Dk Harisson Mwakyembe mapema Februari wakati akiwa Waziri wa Katiba na Sheria iwapo ingeendelea kujihusisha na “uanaharakati wa kisiasa.”

Kutokana na mwenendo wa matukio hayo, barua hiyo inaomba ufanyike uchunguzi wa kina na huru utakaoibua ukweli juu ya kupigwa risasi kwa Lissu na matukio mengine ya uhalifu yaliyowakumba wanataaluma wengine wa sheria na kuwachukulia hatua wote wanaohusika kwa mujibu wa sheria na taratibu za kimataifa.

“Tunazisihi mamlaka kumfutia mashtaka yote yanayomkabili Lissu vinginevyo kuwe na ushahidi wa kutosha na uwe wa wazi na kuwe na fursa ya kukata rufaa,” inasomeka sehemu ya barua hiyo na kuongeza;

“Tunaisihi Tanzania kuheshimu matakwa ya kimataifa, iwalinde wanasheria ili kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao vyema bila vitisho, vikwazo, unyanyasaji wala kuingiliwa majukumu yao.”