Mahakama yatengua uamuzi wa msajili wa vyama dhidi ya DP

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetengua uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa uliobatilisha Mkutano Mkuu wa mwaka wa Chama cha Democratic (DP), kilichoasisiwa na Mchungaji Christopher Mtikila (kwa sasa ni marehemu), uliofanyika Mei 26, 2017.

Pia, mahakama hiyo imebatilisha uamuzi wa msajili huyo wa kuwatambua baadhi ya viongozi wa chama hicho akiwemo aliyekuwa Katibu Mkuu, Feruz Msambichaka, walioondolewa madarakani kutokana sababu za kinidhamu.

Uamuzi huo ambao Mwananchi umeona nakala yake, ulitolewa na Jaji Benhajj Masoud, Julai 22, 2019, kufuatia shauri la maombi lililofunguliwa na bodi ya wadhamini wa chama hicho dhidi ya msajili na mwanasheria mkuu wa Serikali (AG), kikipinga uamuzi huo wa msajili.

Msajili katika barua yake ya kubatilisha mkutano huo ya Julai 3, 2017, iliyosainiwa kwa niaba yake na Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, alidai kuwa haukufuata katiba na kanuni za chama hicho na Sheria ya Vyama vya Siasa.

Alichukua hatua hiyo kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa kwake na baadhi ya waliodai kuwa wanachama na viongozi wa chama hicho.

Kupitia mawakili wake Daimu Halfani na Juma Nassoro, chama hicho kiliiomba mahakama itengue uamuzi huo wa msajili na amri ya kumzua kuingilia mambo ya ndani ya chama hicho, kikidai kuwa kiko huru, kina mshikamano na haki.

Wajibu maombi katika kiapo chao na majibu ya madai pamoja na hoja za maandishi walizoziwasilisha mahakamani, walipinga madai yeye wakidai kuwa msajili alitekeleza majukumu yake kwa mujibu wa mamlaka aliyopewa na Sheria ya Vyama vya Siasa, na kwamba hakukiuka sheria yoyote.

Mahakama baada ya kusikiliza hoja za pande zote kurejea vifungu mbalimbali vya sheria na Vyama vya Siasa, sheria nyinginezo, Katiba ya nchi, katiba ya DP na uamuzi wa kesi mbalimbali zilizokwishaamuriwa zenye mazingira kama hiyo na vielelezo mbalimbali, ilikubaliana na hoja za DP.

Jaji Masoud alisema kuwa msajili alizingatia malalamiko yaliyotolewa na watu ambao wengine hawajulikani, kwamba mkutano huo haukutishwa kwa mujibu wa katiba na kanuni za chama hicho, lakini masharti hayo ya katiba na kanuni yaliyodaiwa kukiukwa hayakuwekwa wazi wala maelezo taratibu yalivyokiukwa.

Aliongeza pia kuwa msajili alizingatia madai kuwa akidi ya mkutano huo haikuwa imetimia na kwamba wawakilishi wengine waliohudhuria hawakuwa wawakilishi halali wa mkutano, ambao hata hivyo hawakuoneshwa kwenye kiapo kinzani (cha wadaiwa) wala kumbukumbu nyingine za mahakama.

Jaji Masoud alisema kuwa zaidi sana hakuna hata moja ya malalamiko hayo yaliyodaiwa kuwasilishwa kwa msajili ambayo yalioneshwa mahakamani na taratibu uliotumiwa na msajili kuyapokea malalamiko hayo kwa namna ambayo inahakikisha haki kwa wote.

“Kwa haya, sidhani kuwa mjibu maombi wa kwanza (Msajili) alitenda kimantiki na mujibu wa kanuni mwenendo unaohakikisha haki kwa pande zote kabla ya kupitisha uamuzi.”, alisema Jaji Masoud na kuongeza:

Alisema kuwa kwa uchunguzi wake wa hoja na taarifa kwenye kumbukumbu za mahakama, si tu kwamba msajili alitenda zaidi ya mamlaka yake kubatilisha mkutano huo kwa kuzingatia malalamiko, aliyoyapokea, bali pia katika mazingira hayo uamuzi wake haukuwa na mantiki.

“Alitenda bila mantiki na zaidi ya mamlaka yake alipozingatia mambo ambayo hakupaswa kuyazingatia na kupuuza mambo ambayo alipaswa kuyazingatia,.”, alisema Jaji Masoud.

Alibainisha kuwa wakati msajili katika uamuzi wake alizingatia malalamiko yaliyowasilishwa kwake, alipuuza maelezo ya taarifa ya mkutano ambao miongoni mwa malalamiko mengine yaliamuriwa; na uchaguzi wa viongozi wa kitaifa wa chama.

Jaji Masoud alisema kuwa msajili alipaswa kuzingatia orodha ya wawakilishi wa mkutano, masharti ya katiba ya chama hicho na kanuni zinazohusiana na mikutano na kama malalamiko hayo ya maandishi ya mkono yalikuwa yanafahamika kwa upande wa chama.

“Nashangaa kwa nini walalamikaji waliaminiwa kwa kila walichokilalamikia kuhusu uhalali wa mkutano. Kimantiki naweza kusema uamuzi huo ulishawishiwa na malalamiko matupu ingawa hapakuwa na ushahidi malalamiko hayo yalithibitishwa kwa namna inayohakikisha haki kwa pande zote.”, alisema Jaji Masoud na kuongeza:.

“Maombi haya yana mashiko. Kwa hiyo ninayakubali na kutoa amri iliyoombwa, kutengua uamuzi uliobatilisha Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Democratic wa Mei 26, 2017 na uamuzi mwingine ulioainishwa.”

Hata hivyo Jaji Masoud alikataa mambo ya chama hicho kumzuia msajili kuingilia mambo yake ya ndani.

Alisema kuwa kama ofisi yenye dhamana ya kusajili, kuhifadhi kumbukumbu, kupokea na kusajili taarifa na mabadiliko ya viongozi wa vyama vya siasa, msajili anategemewa kuwa mamlaka kuangalia ushahidi wa mabadiliko na taarifa hizo za kila mkutano zinazowasilishwa kwake.