Maumivu ya kuzamia uzamivu

Eeeh, Makengeza, sisi wasanii tuna shida sana. Watu hawajui kwamba ubunifu ndio msingi wa maendeleo. Hebu tuanze hata huko nyuma. Kwanza kuna wale ambao walipoona wanasiasa wanasema uongo sana, wakaanza kuwaita wasanii. Eti sisi wasanii ni waongo. Sikatai kwamba tunapoanza hadithi, tunasema:

Hadithi hadithi...

‘Hadithi njoo na uongo njoo utamu kolea’

Lakini usishushe hadhi yangu kwa kuniweka kapu moja na wanasiasa. Ndiyo. Bila uongo hakuna sanaa. Tangu lini sungura aongee kama binadamu? Lakini msanii anasema uongo ili kufichua ukweli, wakati mwanasiasa anasema uongo ili kuficha ukweli. Ndiyo tofauti yenyewe. Na ndiyo maana wanasiasa hawawapendi wasanii kwa sababu wanafichua walichoficha wao.

Haya sasa, wengine wanatwambia kwamba tukitaka kupata maslahi kwenye muziki tuachane na mambo ya siasa. Nasema tena, tafadhali usishushe hadhi yangu. Au hawa wanaopenda kutudhalilisha hivyo kwa kuwa ndivyo walivyo wao? Wanachotafuta ni maslahi tu!

Sikatai kuna wasanii ambao ni kazi yao kutafuta maslahi tu. Tunawajua. Wako radhi kuimba chochote ili mradi maslahi. Sifa, matusi, ufuska ili mradi maslahi. Na wakisifiasifia tu, elimu yao, wazazi wao, maisha yao havihojiwi. Ndivyo wanavyotaka hawa wasanii, sawa, siwezi kupinga, wamechagua maslahi.

Lakini katika historia, wako wasanii wengi hawakujali maslahi. Walijali jamii zao, walisukumwa na dhamira ya kutoa hisia zao na za jamii zao kwa njia ya sanaa. Angalia wanamuziki maarufu enzi za ubaguzi wa Afrika Kusini. Wengi walilazimishwa kuhama hata nchi, na wengine walikufa. Walikuwa wanaangalia maslahi binafsi?

Lakini upande wa pili, historia ya dunia imejaa mifano ya wasanii tunaowaenzi kutokana na sanaa zao zenye msimamo mkali, sanaa zinazotuamsha na kufukuza tongotongo zetu, sanaa zinazovisha sauti zetu za unyonge. Tena wapo walio na digrii na wasio na digrii na ninavyojua suala kuu halikuwa digrii. Lilikuwa msimamo wao. Waliweka mbele maslahi ya jamii zao, si maslahi yao binafsi.

Hata enzi za utoto na ujana wangu, tulikuwa na wasanii wengi wa aina hii. Siasa na muziki vilikula pamoja, vililala na kuamka pamoja. Bob Marley na Miriam Makeba, pamoja na wasanii wetu wa Bongo. Hadi Bob Marley tulimtaifisha na mwenzie, Bob Mallya na Pete Tesha. Katika hali halisi, msanii gani wa kweli ataweza kujiepusha na siasa. Siasa ni maisha na sanaa ni maisha.

Na sasa, kumbe ukitaka kusifia, hamna shida. Hata ukiwa umemaliza darasa la pili, au hata huna madarasa, ili mradi umesifia, ruksa. Lakini kukosoa ha ha ha ha ha. Jamaa anaishi uswazi, anaona hali halisi ya maisha kule, mwenye digrii nne ataiona wapi. Msanii wa Uswazi anaona na anasema. Msichana kabakwa, kafukuzwa shule, kapambana na maisha kwenye mazingira magumu sana, mwenye digrii nne ataiona wapi? Lakini msichana huyu atakuwa sauti ya wenzie wote walionyanyaswa kijinsia hata walionyanyaswa na wenye digrii nne.

Tatizo ni kwamba ukishafika hali fulani, wala huishi ndani ya nchi yetu. Anayesafiri ndani ya magari yenye viyoyozi, vyoo vya ‘tinted’ na ving’ora mbele ili apite haraka ataona nini, tena akisafiri ya ndege haoni kabisa.

Anaangalia chini na kuona mambo yote ni shwari, tulivu. Hata watu hawaoni. Kumbe huko chini kuna matatizo kibao, huyu hana chakula nyumbani kwake, yule anaugua na hana pesa za kununua dawa, yule mwingine ametiwa ndani kwa kumpinga mwenyekiti wa kijiji n.k.

Wasanii wanaoishi ndani ya jamii wanaona haya. Na sifa mojawapo ya msanii ni kuweza kusikia mambo ya watu wengine, ndoto zao, kero zao, mapambano yao, vikwazo vyao, kusikia vyote hivi ndani ya damu yake. Anaweza kusikia vya watu na kuvigeuza kuwa sanaa. Hana haja ya digrii kufanya hivyo lakini wanasiasa wenye akili watasikiliza na kujifunza kutoka kwake.

Yawezekana watakereka na ukali wa sanaa yake, yawezekana wataona kwamba huyu msanii amezidi lakini wakiamua kusikiliza na kuelewa watajua kwamba wamepewa kitu cha maana sana.

Lakini, Makengeza, hali hii haiwahusu sisi wasanii tu. Mara nyingine tunasukumwa kusema, tunasukumwa kutumia jukwaa lolote kupaza sauti kwa sababu tunajua ndugu zetu, bibi zetu, vijana wenzetu, wapenzi wetu, watoto wetu, wagonjwa wetu, wahanga wetu hawasikilizwi.

Kumbe ni kwa sababu hawana digrii nne. Ndiyo maana wanasiasa wenye madigrii yao wakienda kijijini, au uswazini, wanasikiliza kweli maoni na kero za wananchi? Wakielezwa hali halisi, au wakikosolewa, wanajimwambafai tu na digrii zao.

‘Huyu kijana ataniambia nini wakati mimi ni madigrii?’ Mwisho kijana anaambiwa akae chini na kufunga lidomo lake. Na hasira zake na za wenzake zinazidi kuongezeka, zinazidi kusambaa.

Ndiyo maana, kwa kweli, nawashangaa wenye madigrii. Namkumbuka Lawino alivyolalamika kuhusu mume wake mwenye madigrii yote yale. Akaaomboleza kwamba mume wake amepotea kwenye msitu wa vitabu, na kusoma sana kumeharibu kichwa chake mpaka anashindwa kuona, na kusikia, na kufurahia, na kujifunza kutokana na maisha ya watu walio wengi. Bahati mbaya sijazamia uzamivu lakini mimi ningekuwa mwanasiasa, ningewashukuru hawa wasanii wanaothubutu kubeba maoni na machungu ya watu, wanaoanika wazi ili nione maana ingenisaidia kujua mahali pa kujikita zaidi katika kuboresha sera, mipango na utekelezaji wangu. Ndiyo. Wao si tunu la taifa tu, ni tunu kwangu maana wanatumia sanaa kunisaidia nielewe.

Nikimaliza kisanii, bila digrii, hali na sasa ni kama mtu anavuka barabara. Hajui kuna gari linakuja mbio. Sasa mtu wa pembeni aliyevaa hovyohovyo anapiga kelele.

‘Angalia Bwana, kuna gari linakuja kwa kasi.’

Atauliza iwapo huyu mtu ana digrii ngapi kabla ya kuchukua hatua? Tuache hizo jamani, tuache hizo.