MAKALA ZA MALOTO: Ndugai amefanya vizuri kutetea bandari lakini simuungi mkono

Spika wa Bunge, Job Ndugai amekosoa kitendo cha Serikali kusuasua kujenga Bandari ya Bagamoyo. Amesema faida za ujenzi wa bandari hiyo ni nyingi kwa Taifa.

Ndugai amesema alipata maelezo ya ujenzi wa Bandari hiyo kutoka kampuni iliyosaini mkataba wa kuijenga. Kutokana na maelezo hayo, anashangaza kusuasua kwa Serikali.

Spika alifananisha kitendo cha Serikali kuanza ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kabla ya Bandari ya Bagamoyo, kwamba ni sawa na mkokoteni kukukota punda.

Kwanza tukubali; ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo ni wa aina yake Afrika. Itawezesha meli kubwa za mizigo ambazo haziwezi kufika popote Afrika kutia nanga Tanzania.

Kwa maana hiyo, Bandari za Mombasa, Kenya, Beira, Msumbiji na nyingine Afrika, zitakuwa zinapokea mizigo kutoka Bagamoyo.

Tofauti na dhana kuwa Bandari ya Bagamoyo itaua Bandari ya Dar es Salaam, Tanga na Mtwara, ukweli ni kuwa itazichangamsha. Maana shehena nyingi itabidi ziwe zinatoka Bagamoyo kwenda Bandari ya Dar es Salaam, Mtwara na Tanga.

Kwa sasa China imeushika uchumi wa Afrika. Na malengo ya China ni kuihudumia Afrika kupitia Bandari ya Bagamoyo.

Hiyo ni kuonesha kwamba Tanzania kupitia Bandari ya Bagamoyo, itakuwa wakala wa uchumi wa China Afrika. Mzunguko wa kibiashara nchini utakuwa mkubwa, ajira nyingi zitazalishwa na uchumi wa viwanda unaonadiwa utapata kasi nzuri.

Kwa nini Tanzania?

Kwa Afrika, Bagamoyo imeonekana ina ufukwe wenye kina kirefu kufaa ujenzi wa bandari inayokusudiwa kuliko popote pale. Hii ndiyo sababu China inaitamani Tanzania.

Je, Bandari inajengwa kwa mkopo? Jibu ni hapana. Inajengwa chini ya mfumo wa ushirikiano kati ya Sekta Binafsi na Umma (PPP).

Chini ya utaratibu huu mwekezaji anakuja na fedha zake, Serikali inatoa eneo kwa makubaliano ya namna ya kuiendesha bandari kwa kipindi fulani na kila upande unanufaika kulingana na makubaliano.

Wawekezaji wanapewa muda wa kukusanya mapato ili kurejesha gharama zao, baada ya hapo bandari inakuwa mali ya Serikali kwa asilimia 100. Inaelezwa kuwa makubaliano ni wawekezaji kupewa miaka 30 ya makusanyo. Kwa maana hiyo, Serikali haina hasara.

Eneo la ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo liliandaliwa tangu Serikali ya awamu ya nne. Fidia ikalipwa. Bandari ya Bagamoyo imo ndani ya Ilani ya CCM iliyomnadi Rais John Magufuli.

Hivyo, mradi uliuzwa kwa wapigakura. Serikali ya awamu ya tano, iliwakabidhi wawekezaji eneo. Ghafla imekuwa kinyume. Ujenzi haupo tena!

Serikali inasema masharti ya uwekezaji ni magumu sana. Hilo ndilo jibu. Serikali imeshindwa kurudi mezani na wawekezaji kuyapitia hayo masharti magumu? Rais Magufuli alikuta mradi wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo umeshaiva, ilitarajiwa sasa hivi ungekuwa umefika hatua kubwa. Miaka minne ya utawala wa Magufuli, jawabu linatoka kuwa imeshindikana sababu ya masharti.

Ukitazama faida za ujenzi wa Bandari ya Bagomoyo kwa nchi, utaona kuwa Ndugai amefanya vizuri kuutetea.

Hata hivyo, ukimulika muda ambao amekosoa SGR na kutoa wazo la umuhimu wa bandari kabla ya reli, hapo ndipo unaona hayupo sahihi.

Ndugai ni Spika wa Bunge. Chombo anachokiongoza ndicho chenye wajibu na mamlaka ya kuisimamia Serikali. Miaka minne Serikali ipo madarakani, bandari haijajengwa, Bunge lilikuwa wapi? Ndugai mbona alikuwa kimya?

Ujenzi wa SGR unaendelea kwa mwaka wa tatu sasa. Bunge lilikuwa wapi kuukataa mradi huo kabla ya bandari? Mbona Ndugai hakusema wakati huo kuwa Serikali kujenga reli kabla ya bandari ni kujaribu kuufanya mkokoteni ukokote punda?

Kulingana na mkataba wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo, Serikali ingeweza kujenga SGR kama hali halisi ilivyo, kwani hakuna shuilingi yake ingetumika kwenye bandari. Wawekezaji wangekuja na fedha zao.

Kwa maana hiyo, Bunge lingekuwa linatimiza wajibu wake sawasawa, ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo ungekuwa unaendelea, vilevile SGR ingejengwa kwa kasi iliyopo.