HOJA ZA KARUGENDO: Changamoto ni nyingi za mabadiliko tuyatakayo

Wednesday July 10 2019

 

By Padri Privatus Karugendo

Ukweli wa wazi ni kwamba Watanzania wengi wanayatamani mabadiliko katika nyanja zote; kwenye tamaduni, siasa, elimu na hata kwenye imani zetu za jadi na zile za kigeni.

Mabadiliko si uchaguzi, ni kitu ambacho kinakwenda na nyakati. Pamoja na kutamani mabadiliko, kuna changamoto nyingi katika kuyaelekea.

Inawezekana changamoto hizi zikawa kizingiti, lakini kama tulivyoona juma lililopita ni kwamba mabadiliko ni lazima yatakuja tunataka tusitake na muda si rafiki tena.

Mbele yetu kuna changamoto ya Serikali na vyama vya siasa vinavyotamani kuingia madarakani ili kupambana na umasikini, ujinga na maradhi.

Mapambano ya kuondoa maadui hawa yanakwenda mbali zaidi ya kaulimbiu za kisiasa. Na wala hayapaswi kuwatupilia mbali wazee na kuwakumbatia vijana, maana kuna wazee wanaotembea na wakati na kuna vijana walio nyuma ya wakati.

Mapambano haya yataongozwa na wale wanaotembea na wakati. Yanakwenda mbali zaidi ya kufikiri kwamba mtu mmoja anaweza kuleta mabadiliko au kwamba mapenzi binafsi kwa mtu au kiongozi yanaweza kusaidia kuleta mabadiliko.

Advertisement

Wengi wetu tunapenda kuwatukuza watu binafsi tunapoyatamani mabadiliko, lakini hii ni kinyume na ukweli ulivyo. Hata tukiwatukuza ni lazima kutambua kwamba mchakato wa kuleta mabadiliko ni zaidi ya mapenzi binafsi, ni zaidi ya sura ya mtu au chama.

Tunahitaji shule nzuri na vyuo ili kufikia mabadiliko ya kweli. Vyuo vyetu vikuu viwe chachu ya mabadiliko na tafiti zisisubiri wahisani au serikali, zisukumwe na bidii ya kutaka mabadiliko.

Ni bahati mbaya kwamba viongozi wetu wamebaki kuimba kaulimbiu na kutoa ahadi; wapinzani nao wameelekeza nguvu zao katika kulaumu na kukosoa. Wote kwa pamoja wamemezwa na misemo ya ghiliba za mabeberu: utawala bora, kurekebisha uchumi, ubinafsishaji na utandawazi.

Tunashindwa kuibua hoja zetu na kuzishughulikia mpaka tusubiri kuletewa. Hii ni hatari na changamoto kwa mabadiliko tuyatakayo.

Hakuna mwanasiasa hata mmoja anayesimama na kueleza msimamo wa Tanzania juu ya ubeberu na athari zake. Bila kuwa na msimamo dhabiti dhidi yake hatuwezi kupiga hatua ya kweli kuelekea mabadiliko tuyatakayo.

Ubeberu ni ubepari kandamizi ambao hauongozwi tena na mtaji pekee, bali pia na shinikizo na hila za mashirika ya kimataifa na nguvu za kijeshi. Ni ubepari kandamizi uliovuka mipaka na kuenea dunia nzima.

Ni ubepari usioangalia utu wa watu, uharibifu wa mazingira, bali faida. Ni ubepari ambao Mwalimu Nyerere alisema ni unyama.

Kukumbatia siasa za kibeberu ni kuruhusu wageni kuhodhi njia kuu za uchumi. Kama njia kuu za uchumi wa nchi zinahodhiwa na makampuni na mashirika ya kibeberu, maana yake dola inakuwa wakala wa mabeberu. Hili likitokea ni aina nyingine ya ukoloni.

Kwa kufanya hivyo, nchi inakuwa na uhuru wa bendera, lakini uchumi wake unaendeshwa na mabeberu.

Bila kubadili sura ya uchumi wa kibeberu si rahisi kuwa na mfumo wa kisiasa wa kidemokrasia. Maana kazi ya siasa ni kulinda maslahi ya kiuchumi ya tabaka lililohodhi njia za uzalishaji.

Advertisement