Breaking News

Maandamano Malawi aina nyingine ya demokrasia Afrika

Wednesday July 10 2019

 

By Peter Elias, Mwananchi [email protected]

Wimbi la maandamano ya wananchi dhidi ya viongozi wao limezidi kupamba moto barani Afrika.

Katika baadhi ya nchi, waandamanaji wanashinikiza viongozi hao wa muda mrefu kuondoka na kuipisha ‘damu changa’ kuiongoza nchi zao. Lakini kwingineko, ni kupinga kile baadhi ya wananchi wanaita wizi wa kura.

Wimbi hilo lilianzia kwenye nchi za Kiarabu kama vile Tunisia, Misri, Algeria na Sudan lakini sasa limeanza kuenea kwenye nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ambako pia kuna ukandamizaji wa demokrasia.

Malawi ni miongoni mwa nchi zinazokabiliwa na maandamano hayo kwa sasa. Wananchi wake wameingia mitaani baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika Mei 21, mwaka huu na Rais Peter Mutharika kuibuka kidedea kwa ushindi mwembamba wa asilimia 38.57. Uchaguzi huo ulikuwa na wagombea saba lakini mchuano mkali ulikuwa kwa wagombea watatu; Mutharika kupitia chama chake cha DPP, makamu wake, Saulos Chilima (UTM) na Lazarus Chakwera kutoka chama cha MCP.

Mutharika alikuwa akiwania muhula wake wa pili wa miaka mitano na kwenye uchaguzi huo akishindana kwa karibu na Chakwera. Uchaguzi huo ulikuwa na hamasa kubwa na wagombea hao walipishana kwa kura chache. Chakwera akipata asilimia 35 ya kura zilizopigwa.

Hata hivyo, wananchi wanadai kwamba Mutharika alishindwa uchaguzi huo, hivyo, wanamtaka aondoke madarakani mara moja huku wakiishutumu pia Tume ya uchaguzi ya Malawi. Wananchi hao wamefanya maandamano makubwa katika miji ya Lilongwe, Blantyre na Mzuzu nchini humo.

Advertisement

“Haya ni maamuzi ya kila mwananchi wa Malawi anayetaka kuona haki inatendeka nchini. Ninaungana na Wamalawi wenzangu kwa sababu mimi pia ni mmoja wao kwenye msiba huu,” alisema Chakwera kama alivyonukuliwa na Shirika la Habari la Al Jazeera.

Hata hivyo, vyombo vya habari vya ndani nchini humo vilimnukuu Rais Mutharika akisema maandamano hayo ni batili na amewataka wapinzani kukubali matokeo ya uchaguzi huo na kuendelea na majukumu mengine ya kujenga nchi.

Maandamano haya ni ya kwanza kwa Rais Mutharika tangu alipochaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2014 na kushinda uchaguzi kwa asilimia 36.4. Hata hivyo, uchaguzi huu umekuwa mgumu kwake kutokana na madai kwamba afya yake haiakuwa nzuri.

Julai 6, Rais Mutharika alinukuliwa akisema waandamanaji wanataka kuifanya nchi hiyo kama haina sheria zake. Amesema hatakubali suala hilo litokee wakati akiwa hai na kwamba atahakikisha nchi hiyo inakuwa salama.

“Vurugu mnazoziona zimetengenezwa ili kuifanya nchi ionekane haina sheria,” alinukuliwa Rais Mutharika wakati wa mkutano wa hadhara wa maadhimisho ya miaka 55 ya uhuru wa nchi hiyo.

“Wanataka kutengeneza hali ya kutokuwa na sheria ili waipindue serikali hii, lakini ninawaambia nikiwa hai hawawezi kuipindua,” alisema Mutharika.

“Kuifanya Malawi nchi isiyo na sheria zake haikubaliki. Tutamwajibisha kila mmoja wao, nguvu itakutana na nguvu na upuuzi huu utafikia mwisho,” alinukuliwa Rais huyo bila kutaja chama au kundi linalohusika.

Maandamano hayo ya wananchi yamefikisha miezi miwili sasa tangu uchaguzi ulipofanyika huku waandamanaji wakishinikiza pia Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Jane Ansah kujiuzulu nafasi hiyo.

Wapinzani, Chakwera na Chilima wamekuwa wakishiriki kwenye maandamano hayo ya wananchi yaliyoandaliwa na Muungano wa watetezi wa haki za binadamu nchini humo na kuitikiwa na wananchi zaidi ya 20,000.

Makamu Mwenyekiti wa muungano huo, Gift Trapence aliliambia Shirika la Habari la AFP kwamba maandamano hayo hayana lengo la kuipindua serikali, bali kushinikiza mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Jane Ansah kujiuzulu.

Wapinzani wanadai kwamba uchaguzi wa Mei ulitawaliwa na vitendo vya udanganyifu ikiwemo baadhi ya karatasi za kura kubainika zimefutwa kwa wino kusahihisha kilichokuwa kimeandikwa kabla.

Hatua zaidi

Wapinzani wamefungua kesi katika Mahakama ya kikatiba nchini kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi Mutharika. Mahakama hiyo inasubiriwa kutoa uamuzi wake juu ya uhalali wa matokeo hayo.

Maandamano kama yanayoendelea Malawi yalifanyika pia Sudan mapema mwaka huu na kuhitimisha miaka 30 ya utawala wa Omar al-Bashir ambaye aliingia madarakani kwa njia ya mapinduzi mwaka 1989.

Sababu za kuondolewa kwake zilikuwa ni pamoja na kupanda kwa bei ya mkate nchini humo na mfumuko wa bei ambao uliwaumiza wananchi wa hali ya chini.

Pamoja na kuondolewa kwa Bashir, mpaka sasa bado hali ya usalama nchini humo haijaimarika kutokana na mvutano kati ya jeshi na waandamanaji.

Vuguvugu la maandamano lililoanza mwaka 2011, Aprili mwaka huu limefika Algeria ambako kiongozi wake, Abdelaziz Bouteflika ameondolewa kwa nguvu ya wananchi.

Advertisement