Makundi ya ‘tangatanga’, ‘kieleweke’ yaivuruga Jubilee

Wednesday May 22 2019

 

By Noor Shija, Mwananchi

Msemo kwamba ‘hakuna rafiki au adui wa kudumu kwenye siasa’ umedhihirika kwa wanasiasa Rais Uhuru Kenyatta, Naibu Rais William Ruto na Raila Odinga na umekivuruga chama tawala cha Jubilee na kuibua makundi mawili ya ‘tangatanga’ na ‘kieleweke’.

Kenyatta na Ruto waliunda chama cha Jubilee na kushinda Uchaguzi Mkuu wa Kenya mara mbili. Kenyatta akiwa Rais na Ruto naibu Rais.

Lakini, adui yao mkubwa na hasa kwa Rais Kenyatta kwa sababu alishindana naye kwenye sanduku la kura mara mbili ni kiongozi wa upinzani, Raila Odinga.

Ushindi wa Uchaguzi Mkuu uliopita uliomrejesha madarakani Kenyatta ulipingwa na Raila mahakamani na matokeo yakafutwa, lakini Raila na washirika wake waliususia uchaguzi wa marudio.

Mbali na kususia uchaguzi huo uliompa tena ushindi Kenyatta, kambi ya Raila ilitangaza kutomtambua na baadaye kiongozi huyo wa upinzani alijiapisha kuwa ndiye rais halali wa mamlaka ya Kenya.

Lakini, kama wasemavyo wahenga hakuna rafiki au adui wa kudumu kwenye siasa, Machi 9, 2018 katika hali ambayo haikutarajiwa na wengi, mahasimu hao wawili Rais Kenyatta na Raila walikutana faragha katika ofisi ya rais iliyopo kwenye Jumba la Harambee jijini Nairobi.

Advertisement

Walipotoka, wawili hao walionekana kuwa na sura za bashasha, na kupeana salamu ya mikono ambayo ndio imekuwa jina la mkutano huo, kwa Kingereza unafahamika kama ‘The handshake’.

Raila aliyejilisha kiapo cha ‘urais’ aliwashangaza wengi kwa kumuita mtu ambaye alikuwa hautambui uongozi wake kuwa ni ‘ndugu’ na kuongeza kuwa: “Ndugu yangu na mimi tumekutana na kusema yamefikia kikomo. “

“Tumekuja pamoja na ndugu yangu Kenyatta, tumeongea kwa kirefu na kukubaliana kwamba tunataka kuunganisha Kenya iwe taifa moja. Mgawanyiko ambao umekuwepo tangu uhuru utakwisha hapa na sisi. Tutembee pamoja,” amesema Raila.

Wawili hao wakakubaliana kufanya kazi pamoja katika kufanikisha maboresho hayo na kuwaletea maendeleo Wakenya wote.

Kilichofuata ni pongezi kwa ‘handshake’ ambapo Naibu Rais Ruto alitumia akaunti yake ya twitter kuwapongeza Kenyatta na Raila kuwa wameonyesha utaifa kwa kuuepusha Kenya dhidi ya vurugu, ubaguzi na mgawanyiko. Kwamba umoja, mshikamano na mabadiliko ndio msingi kuliko masilahi ya vyama.

Tofauti na matarajio ya wengi salamu za heri kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani, Raila Odinga, imebadilika na kuibua mgawanyiko ndani ya chama cha Jubilee. Sasa kuna makundi mawili ‘tangatanga’ na ‘kieleweke’.

Kwa tafsiri ya kawaida ‘tangatanga’ ni tembeatembea au zurura, wakati ‘kieleweke’ ni kuhakikisha jambo husika linafika tamati.

Hata hivyo, Ruto amekitetea chama tawala Jubilee kuwa kiko imara licha ya kuibuka makundi mawili yanayokinzana, ‘kieleweke’ na ‘tangatanga’.

Kundi la ‘tangatanga’ linamuunga mkono Ruto na harakati zake za kugombea urais mwaka 2022 na lile la ‘kieleweke’ lenyewe linampiga. Licha ya hali hiyo, Ruto bado ameshikilia kuwa hakuna mpasuko ndani ya chama.

Pia, Ruto amewakosoa baadhi ya viongozi wa Jubilee kwa madai ya kujiunga na upinzani ili kuvuruga azma yake ya kuwania kiti cha urais kwenye uchaguzi mkuu ujao, huku akisema kuwa hata hivyo Jubilee iko imara licha ya kuibuka makundi mawili yanayokinzana.

Mbali na kauli ya Ruto, kadri siku zinavyoenda cha Jubilee kimeonekana kikisuguana juu ya mkutano wa Kenyatta na Raila.

Wakati wafuasi wa Kenyatta wakisifu hatua ya kiongozi wao katika kumaliza mzozo uliokuwa unatishia usalama wa nchi, wafuasi wa Ruto wamekuwa wakitilia shaka mapatano hayo.

Mpaka sasa wapo wanaoamini kuwa mapatano ya Kenyatta na Raila yatakuwa na nguvu ya kuamua nani atakuwa rais wa Kenya mwaka 2022.

Akiwa nchini Uingereza Kenyatta akihutubia kwenye jumba linalokusanya watafiti na wanazuoni wa siasa wa kimataifa la Chatham jijini London alisema mapatano yake na Raila hayalengi uchaguzi wa 2022.

Anasema wamekubaliana na Raila kwamba taifa la Kenya ni muhimu kuliko mtu binafsi na kwamba lazima viongozi washirikiane.

Rais huyo amesema siku za usoni za Kenya haziwezi kuongozwa na uchaguzi ujao bali “uthabiti wa taifa.”

“Demokrasia si mwisho wa kila kitu. Ni shughuli na nia ya wananchi lazima iongoze. Tumekubaliana tutaleta pamoja wananchi na kujadiliana kuhusu matatizo yanayoathiri taifa letu na wananchi, na kuunda taifa lenye umoja na lililo imara ambapo hakuna raia anayehisi ametengwa.

“Huu ni mwanzo mpya kwa taifa letu. Tunaweza kutofautiana lakini kusalia tukiwa tumeungana kama Wakenya.

Licha ya kauli hizo, kuendelea kwa mgawanyiko huo sasa umemwacha njia kisiasa panda gavana wa Nairobi, Mike Sonko.

Gavana huyo ambaye yuko karibu na Ruto, amedai msimamo wake haungi mkono makundi yote mawili; ‘kieleweke’ na ‘tangatanga’, ambayo yamechipuka ndani ya chama cha Jubilee.

Wiki mbili zilizopita, Sonko aliwashambulia hadharani aliyekuwa mgombea wa nafasi wa gavana wa jiji la Nairobi, Peter Kenneth na mbunge Maalumu Maina Kamanda huku akiwataja kuwa mafisadi mbele ya waumini wa Kanisa la Mtakatifu Stephens ACK Nairobi.

Kenneth na Kamanda ni miongoni mwa wanasiasa wa kundi la ‘kieleweke’ linalompinga Ruto kuwania urais 2022.

Kamanda ni miongoni mwa wanasiasa kutoka eneo la Kati waliopoteza kura za mchujo za Jubilee kabla ya uchaguzi wa Agosti 8, 2017 na wamekuwa wakimshutumu Ruto kwa ‘kuwaangusha’.

Katika hotuba yake kanisani, Sonko pia alishambulia kundi la ‘Nairobi Regeneration’, lililobuniwa na Rais Uhuru Kenyatta kusafisha na kupangilia upya jiji la Nairobi.

Sonko alisitisha shughuli ya kubomoa vibanda na majumba yaliyojengwa katika hifadhi ya barabara au eneo la serikali hadi pale atakaposhauriana na Rais. Sonko na Waziri wa Utalii Najib Balala ndio wenyeviti wa kamati ya ‘Nairobi Regenaration’.

Mwaka jana, Sonko alidai kuwa baadhi ya mabwanyenye kutoka eneo la Mlima Kenya walikuwa wakifanya vikao vya usiku kupanga njama ya kumzuia Ruto kuwa rais 2022. Sonko aliapa kukabiliana na yeyote ambaye angethubutu kumzuia Ruto kumrithi Rais Kenyatta.

Advertisement