Sumaye ametimiza nilichotarajia

Waziri Mkuu  mstaafu, Frederick Sumaye akifurahi na Katibu Mkuu wa CCM  Dk Bashiru Ally baada ya kutangaza kurejea katika chama hicho jijini Dar es Salaam jana, ikiwa ni siku chache baada ya kujivua uanachama wa chadema. Picha na Ericky Boniphace

Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye ametimiza kile ambacho nilidhani kinapaswa kutokea, amejiunga na chama chake cha CCM kilichomlea na kumfikisha hapo alipo. Mwaka jana nilipoandika kuhusu mwelekeo wake wa kisiasa nilitilia shaka msimamo wake wa awali kwamba angeweza kuachana na siasa au kuwa mshauri wa kisiasa wa jumla; nilisisitiza kuwa msimamo wake hautekelezeki kwa sababu ambazo nilizianisha.

Watu wengi na hasa wenye misimamo ya kiupinzani wanamuona Sumaye kama myumbaji, ndimi mbili, asiye na msimamo, msaliti na kigeugeu. Watu hao wamekataa kuvaa viatu vyake na wamekataa kuwa yeye kabla hawajasema mambo yote hayo. Nukuu za niliyoyasema kuhusu mwelekeo wa Sumaye zilisisitiza mzee huyu anazo sababu nyingi za kuondoka upinzani na kujiunga na CCM kuliko kuachana na siasa; kuwa mshauri wa vyama vya siasa; na kujiunga na chama kingine cha siasa, nitachambua zaidi!

Chadema hakukukalika

Hapa nazungumza kama mtu ambaye nina uzoefu na siasa za ndani kabisa za vyama vya upinzani, ambaye anavijua vyama vya upinzani vya Tanzania na nini vinafanya ndani kabisa ya utendaji wake na ufanyaji maamuzi wake. Uwezekano wa Sumaye kukaa Chadema ulikuwa mdogo kwa sababu hakuwa na nafasi tena, hata kama alikuwa na matamanio ya kufanya mabadiliko na kuviimarisha vyama vya upinzani asingeweza, sisi tuliokaa huko miaka 10 na baadaye kuondoka tunalijua hilo! Vyama vya upinzani vya Tanzania ukiingia ukabahatika kukaa ndani kabisa kunapokopikwa mambo, baadaye utaondoka tu!

Chadema hakukukalika kwa sababu ya mifumo ya ndani ya chama hicho, kama vilivyo vyama vingine vya upinzani. Maamuzi mengi ndani ya chama hicho yamekuwa yakifanywa na watu wachache kimkakati, wako vijana wengi ndani ya chama hicho ambao unawaona hadharani wakikipigania kwa nguvu zote lakini tuliokaa upinzani tunajua kuwa hawakuwahi kufurahia namna chama kinavyoendeshwa kwa nguvu za watu wachache ambao wamejijenga na wana nguvu za kipekee.

Kipute cha 2015

Mathalani, mwaka 2015 wakati Edward Lowassa anapokelewa na kuwa mgombea pekee wa urais, maamuzi ya awali yalifanywa na watu wachache sana wenye nguvu huku walio wengi wakiyapinga lakini wenye hoja wakaja kuzidiwa na wachache wenye nguvu.

Wakati huo nilikuwa mjumbe wa kamati maalum ya ushauri ya UKAWA ambayo ilichakata masuala mbalimbali na kuyakabidhi kwa viongozi wakuu wa vyama, wajumbe walio wengi wa kamati ile waliona haikuwa sahihi kumkaribisha Lowassa na kumfanya mgombea urais, lakini nguvu ya kikundi cha watu wachache ndani ya Chadema ililisimamia jambo hilo kwa nguvu, na ikapata sapoti kubwa ya Prof. Lipumba ambaye baadaye alikuja kunishangaza alipojiuzulu uenyekiti wa CUF kwa hoja kuwa chama hicho kimempokea Lowassa na amekuwa mgombea wao.

Siasa za upinzani kwa waliokulia huko na wanaoyajua ya huko wanajua zinavyoweza kukubwatusha. Siku moja ntaandika kumbukizi zangu kuhusu masuala haya ya ndani ya vyama ili kuendelea kujenga uelewa wa wananchi kwamba vyama hivyo vimegoma kukomaa na kuwa na uwezo au kujionesha kama mbadala wa kusaidia katika uongozi wa nchi na kwa hiyo ndoto za baadhi ya watanzania (nikiwamo mimi zamani) kwamba vinaweza kuongoza dola ni ndoto isiyowezekana ikiwa vinaendelea kujiendesha kama ilivyo sasa.

Mbadala ungelikuwa ACT Wazalendo?

Ninafahamu kuwa viongozi wakubwa wa ACT Wazalendo kimkakati na ndani kwa ndani walifanya kazi kubwa ya kutaka Sumaye ajiunge ACT alipoondoka Chadema (wachache tunalijua hili). Japokuwa taarifa iliyotolewa na kiongozi wa ACT ilionesha masikitiko yake makubwa kwa Sumaye kuondoka Chadema lakini ndani kwa ndani ACT walikuwa shereheni, kama fisi asubirivyo mkono wa mwanadamu udondoke.

Siasa hizi za uzandiki na unafiki zilifanywa pia wakati profesa Lipumba alikuwa anaongoza mgawanyiko mkubwa ndani ya CUF, ACT pamoja na kiongozi wake wa sasa walimuunga mkono na kumsaidia usiku na mchana, hawakujua kesho yao iko namna gani.

Baadaye upande wa Maalim Seif, ndiyo umejikuta uko ACT na siyo ule wa Lipumba na hiyo haijalishi kuwa ACT walitumia muda wao wote kumtetea na kumsaidia Lipumba, walipoona mambo yakiharibiwa zaidi na Lipumba, wakawa watu wa kati “neutral persons”. Walipoona yanaharibika kabisa wakajidai wanatetea upande wa Maalim Seif na mwisho wa siku ukajiunga na chama hicho, siyo kwa kupenda bali ni kwa sababu ulilazimika kutojaribu kujiunga Chadema kwa kufahamu aina ya siasa ngumu za ndani ya chama hicho ambazo zinaongozwa na kundi maalum la watu wachache na kwa hiyo kujiunga nao kulikuwa na maana ya kuuzika upande wa Maalim Seif katika ufanyaji maamuzi.

Sababu hizi hizi za kugeukageuka na uzandiki unaoendelea kwenye vyama vya upinzani ndizo zimefanya Sumaye kutokaa Chadema na kutokwenda ACT pia, kwa sababu siasa za ndani ya ACT nazo ni ngumu mno, na kwa hiyo asingelijaribu kwenda CUF .

Jaribu kuwa Sumaye

Mtu yeyote mgeni kama Sumaye asingeliweza kuhimili aina hizo za siasa kwa sababu imewashinda vijana wengi walioko huko ambao wanaonekana kuupigania upinzani lakini ndani ya nafsi zao wamekata tamaa na mifumo yenyewe.