VIDEO: Upinzani utatoboa uchaguzi 2020 - Lucy Magereli

Umewahi kufikiria hali itakuwaje katika siasa za upinzani, hususani kwenye uchaguzi mkuu ujao?

Kama umefanya hivyo na kukosa jibu. Usijali, lipo jibu rahisi kutoka kwa Lucy Magereli, mbunge wa viti maalumu (Chadema), kwamba “upinzani utatoboa kwenye uchaguzi wa 2020”.

Katika mahojiano na Mwananchi, Magereli anasema licha ya kuwapo “mbinyo wa siasa”, hana shaka kwa kuwa wananchi ndio wataamua.

“Kuna mbinyo wa kisiasa ukihusisha hofu dhidi yetu wapinzani, ikiwamo wanasiasa wa upinzani kupata mateso, kufungwa magereza, kupigwa risasi, jambo linalotishia ustawi wa demokrasi,” anasema Magereli.

Anasema mambo yanayotokea wananchi wanayaona. Hali ya kiuchumi ambayo haiathiri upinzani peke yao bali na wananchi inaonekana, kubinywa kwa demokrasia kunaonekana, hivyo watafanya maamuzi sahihi.

“Licha ya kuwapo viapo vya kutotaka kuuona upinzani 2020, na sisi tupo kikatiba, hilo halitutishi, tupo imara. Tunaendelea kuwa sauti ya wasiokuwa na sauti kwa morali na hali ileile kwa sababu wanaoamua ni wananchi.

“Tunaamini kama wananchi wanavyotuamini siku zote, hivyo tutatoboa na tutafanya siasa zenye upinzani kuliko mwaka 2015. Kutokana na kubinywa kwa miaka mingi wananchi watataka kuisikia sauti kutoka nyikani inasema nini, na itafanya nini kuwatetea,” anasema Magereli.

Mbunge huyo anasema wasiwasi uliobaki ni juu ya Tume huru ya uchaguzi, lakini majibu ya kesi ya kuwapinga wakurugenzi kusimamia uchaguzi yanaonyesha ni kwa namna gani giza nene linaanza kufunguka.

Kuhusu usawa wa kisiasa, Magereli anasema siasa za ushindani hazina usawa.

Anasema watawala wanakuwa waoga wa demokrasia kwa sababu demokrasia ikikua inatazama mambo mengi ikiwamo kusimamia jinsi rasilimali namna zinavyotumika na umuhimu wa kupatikana maendeleo.

“Dhima kuu ya kuanzisha upinzani ni kuwa na watch dog, mtu wa kufuatilia mienendo mizima ya watawala, matumizi ya fedha, mgawanyo wa rasilimali na kukosoa pale pasipokuwa sawa kwa ujumla.

“Kinachowakera watawala ni kukosolewa, kuonywa pale wanapotumia vibaya rasilimali na wanapowakandamiza wanyonge, sisi hatutarudi nyuma hadi lengo litimie,” anasema Magereli.

Kuhusu ushiriki wa wanawake katika siasa, Magereli anasema kuwa mfumo wa kiutawala wa jamii ya Tanzania kwa maana ya tamaduni, bado una vizingiti vingi kwa mwanamke.

Anasema tamaduni zimemchukulia mwanamke kama mzalishaji mali, mlezi wa watoto, muuguzi wa wagonjwa, mama wa familia na mke, hivyo tayari jamii imempa majukumu mengine.

Anazungumzia hata uwezo wa kifedha, akisema wengi hawana kipato cha kueleweka kwa sababu tangu awali hawakupewa nafasi ikiwamo hata ya kupata elimu.

“Hivyo hata kipato cha wengi wao kimekuwa cha kuungaunga na fedha wanazozipata wanaona bora wafanye matumizi kwa ajili ya familia, badala ya kuziingiza kwenye masuala ya siasa,” anasema.

Anasema jamii bado imeelemewa na mfumo dume, ambapo kukiwa na vijana wawili wa kike na kiume waliofikia kidato cha nne na rasilimali za kuwasomesha zikawa ndogo, wa kike atabaki na kusomeshwa wa kiume.

Anaeleza kuwa hali hiyo inawakosesha kujiamini na kushindwa kusimama mbele za watu kutetea hoja zao, wakiamini hawajui vitu vingi kwa sababu hawajasoma.

Anashauri ili kumkomboa mwanamke na kuingia kwenye nafasi za kisiasa tangu wakiwa wadogo, waambiwe wao ni sawa na wanaume na wajengewe misingi ya kutafuta fedha na kujiamini.