Siku ngumu kwa wabunge Kubenea, Komu Chadema

Baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu ya Chadema wakitoka ndani ya ukumbi wakati wa mapumziko. Kikao hicho kilifanyika katika Hoteli ya Bahari Beach, Dar es Salaam jana. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

  • Wabunge hao wawili wa Chadema hatima ya uanachama wao inatarajiwa kujulikana leo baada ya Kamati Kuu ya chama chao kufanya kikao jana

Dar es Salaam. Jana ilikuwa siku ngumu kwa wabunge wawili wa Chadema, Saed Kubenea (Ubungo) na Anthony Komu (Moshi Vijijini) baada ya kuhojiwa na kikao cha Kamati Kuu cha chama hicho kikuu cha upinzani nchini.

Kikao hicho cha dharura kilichofanyika katika Hoteli ya Ledger Plaza kilikuwa na ajenda moja tu ya kuwajadili wabunge hao.

Kubenea na Komu katika siku za hivi karibuni wamezua mjadala ndani na nje ya chama hicho kwa kile kinachodaiwa ni sauti yao inayosikika wakipanga mpango hasi dhidi ya Meya wa Ubungo, Boniface Jacob.

Wabunge hao kwa nyakati tofauti wamekana kuhusika na sauti hiyo kwa kile walichoeleza ni ya kutengeneza huku Jacob ambaye ni Diwani wa Ubungo (Chadema) naye akieleza kupeleka suala hilo ndani ya chama.

Jana, baada ya Komu kumaliza kuhojiwa na kumpisha Kubenea, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa chama hicho, John Mrema alisema wangetoa maazimio mara baada ya kikao hicho.

“Tumekuwa na kikao tangu saa tano asubuhi. Kikao hiki ni cha dharura na ajenda yake ni moja. Ni kuhusu clip (sauti) inayosambaa ikiwahusisha wabunge wetu Komu na Kubenea,” alisema Mrema.

“Tumewaita wabunge hawa ili waieleze Kamati Kuu nini kinaendelea. Komu ameshamaliza kuhojiwa (jana 11:32 jioni), mahojiano yanayoendelea sasa (jana saa 12 jioni) ni kati ya kamati na Kubenea.”

Alisema baada ya kikao hicho ambacho ni chombo cha nidhamu kwa wabunge, watatoa maazimio ambayo yatawekwa wazi.

“Hadi sasa (jana jioni) kikao kinaendelea. Ni mapema mno kuelezea tutarajie nini ndani ya kikao hiki ila Kamati Kuu yetu ina watu wenye weledi, tumewapa nafasi wabunge hawa waeleze kuhusu hii clip (sauti) na ilikuwaje” alihoji.

Alisema katika sauti hiyo, kuna viashiria vya kijinai na kwamba kulingana na maelezo yao kamati itaamua cha kufanya.

“Siwezi kuingia kwenye vichwa vya wajumbe (wa kamati kuu) kila mmoja ana mawazo yake ila naamini uamuzi utakaotolewa utakuwa ndani ya katiba ya chama,” alisema Mrema.

Awali, Kubenea na Komu walionekana nje ya ukumbi huo saa 8:01 mchana wakisubiri maelekezo.

Komu ndiye aliyeanza kuhojiwa kuanzia saa tisa alasiri na kumaliza saa 11:32 jioni na kufuatiwa Kubenea.

Komu alipotakiwa kueleza nini alichohojiwa alisema hana mamlaka ya kuzungumzia lolote.

“Kwa mujibu wa katiba ya chama changu sina mamlaka ya kuzungumza chochote suala hilo lipo ndani ya kikao,” alisema Komu.

Chadema waonyesha magari

Sambamba na kikao hicho, chama hicho kilionyesha kwa waandishi wa habari magari yake aina ya Ford Ranger kikisema yatatumika katika shughuli za kukiimarisha na kukirejesha kwa wananchi.

Msemaji wa chama hicho, Tumaini Makene alisema magari hayo yatatumika katika chaguzi na utekelezaji wa programu yake ya ya Chadema msingi.