Tandahimba warejesha Sh12 mil za watumishi hewa

Muktasari:

Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Twaribu Mzenga alisema hayo wakati akisoma taarifa katika kikao kilichofanyika hivi karibuni.

Tandahimba. Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara imefanikiwa kurudisha Sh12.3 milioni kati ya Sh12.8 milioni zilizokuwa zimepotea kwa watumishi hewa watano.

Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Twaribu Mzenga alisema hayo wakati akisoma taarifa katika kikao kilichofanyika hivi karibuni.

Alisema katika kutekeleza agizo hilo la Rais John Magufuli, kazi ya uhakiki imefanyika kwa watumishi wa kada zote ikiwamo kujaza fomu maalumu.

“Halmashauri yetu tumefanya uhakiki na kufanikiwa kuwabaini watumishi hewa watano ambao walikuwa ni walimu wastaafu na kati yao mmoja wao alifariki, lakini bado walikuwa wanalipwa mshahara kinyume na utaratibu,” alisema Mzenga.

Aliwataka madiwani wa halmashuri hiyo kushirikiana na watendaji wa kata ili kubaini watumishi hao na kuwafuta katika malipo yao ya mishahara.

Mtwara una watumishi hewa 107 kati ya hao, watumishi 20 wana vyeti vya kughushi na kuisababishia Serikali hasara kwa kulipwa mishahara Sh300 milioni.